LEO zikiwa zimebaki siku 50 kabla ya kufanyika Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani kuna jambo ambalo linapaswa kupongezwa.
Kampeni hizi ambazo zinaingia wiki ya pili sasa, zimeendelea kufanyika kwa amani na utulivu maeneo mbalimbali ya nchi yetu.
Hili ni jambo kubwa la kujivunia kwa sababu wanasiasa na wapambe wao wanazingatia sheria, taratibu na kanuni zinazowaongoza.
Tumelazimika kusema haya kutokana na ukweli kuwa miaka yote kampeni zinapozinduliwa huwa kunakuwa na matukio madogo madogo ya uvunjifu wa amani, lakini mwaka huu imekuwa tofauti, jambo ambalo ni jema.
Hii inatokana na miongozo mizuri iliyowekwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kwa kutoa elimu kwa wagombea na vyama vyao.
Tume ilifanya mikutano mingi iliyoshirikisha viongozi wa vyama vya siasa, viongozi wa dini na taasisi zingine kutambua umuhimu wa kuzingatia sheria za nchi.
Tumeshuhudia kampeni zikiendelea kwa amani kwa wagombea kunadi sera zao kwa wapigakura ambao watafanya uamuzi wao Oktoba 28.
Jambo la pili ambalo tumeona tuligusie ni utulivu mkubwa ambao umeonyeshwa na Jeshi la Polisi tangu kuanza kampeni hizi.
Utulivu na ukomavu ambao umeonekana mwanzoni mwa kampeni hizi ni jambo zuri linalopaswa kuendelea.
Tunasisitiza hili kwa sababu polisi ambao ndio wasimamizi wakuu wa usalama wa raia na mali zao, wameonyesha tofauti kubwa tofauti na chaguzi nyingi ambazo zimewahi kufanyika.
Tangu kuanza kampeni uchaguzi wa mwaka huu, hatujashuhudia lawama za wagombea wawe wa urais, ubunge au udiwani kwamba wanaonewa au kushushwa kwenye majukwaa ya kampeni ama kwa makosa ya kupitiliza muda au vitendo vingine.
Hii ni heshima kubwa kwa chombo hiki ambacho kinaonekana kimejiandaa vizuri kuanzia hatua za utimamu. Tunatambua polisi wana wajibu wa kuchukua hatua zozote dhidi ya wavunjifu wa amani sehemu yoyote.
Tunasema ukomavu huu uendelee hadi siku ya kuhitimisha kampeni na uchaguzi mkuu na kushuhudia historia mpya ikiandikwa.
Lakini haya yote yanatokea kwa sababu pia wagombea na wananchi wanatii sheria bila shuruti jambo ambalo ni la msingi.
Tunatumia nafasi hii kumpongeza Mkuu wa Jeshi la Polisi pamoja wasaidizi wake kwa utulivu na usimamizi huu mzuri.
Pamoja na kazi nzuri hii, tunasema IGP aendelee kutoa elimu siku hadi siku kwa askari, si vizuri kutumia nguvu pasipo na sababu ya msingi, kwani kinyume na hapo uzuri wote unaweza kufutika na kutia doa.
Mafanikio yaliyoonekana sasa, yawezekana ni maelekezo mazuri ambayo yanatolewa na kusimamiwa vizuri na wakuu wa vikosi.
Sisi MTANZANIA tunasema taifa letu lazima lilindwe na Watanzania wenyewe kwa sababu hatuna pa kukimbilia pindi ulivu ukivurugika.
Kwa msingi huo, tunawasihi wanasiasa kipindi hiki kuendelea na kampeni za kistaarabu ambazo zinaambatana na ilani zao ili kuwaeleza wananchi watawafanyia nini pindi watakapoingia madarakani.
Utaratibu huo huo, uendelee kwa kutii sheria badala ya kusubiri kupambana na vyombo vya dola pasipo na sababu yoyote ya msingi. Hili ni taifa letu wote.
Tunamalizia kwa kusema polisi wameonyesha uwezo mkubwa mwaka huu, tunawasihi wasitibue rekodi hii nzuri ambayo wameanza nayo.