26.2 C
Dar es Salaam
Friday, November 15, 2024

Contact us: [email protected]

Polisi Ruvuma wachunguza vifo viwili vya kutatanisha

Amon Mtega, Songea

KAMANDA wa polisi wa Mkoa wa Ruvuma, Simon Maigwa, amesema jeshi hilo linafanya uchunguzi wa vifo viwili vya kutatanisha vilivyotokea wilayani Mbinga, ambapo katika tukio la kwanza walikuta mifupa ya mtu anayedhaniwa kuwa ni mwanafunzi na tukio la pili msichana alikutwa kwenye nyumba ya wageni akiwa amefariki dunia.

 Akizungumza ofisi kwake jana, alisema tukio la kwanza ni kuokotwa kwa mifupa inayodhaniwa kuwa ni ya mwanafunzi wa kidato cha pili katika Shule ya Sekondari ya Mkwaya wilaya ya Mbinga, Luth Ndunguru.

 Alisema tukio la kuokotwa mifupa hiyo lilitokea Mei 17 mwaka huu saa saba mchana katika kitongoji cha Tungutu Kata ya Kilimani Wilaya ya Mbinga.

Kamanda huyo alisema pembeni mwa mifupa hiyo kulikuwa na nguo pamoja na daftari zilizoandikwa jina la Luth Ndunguru.

Alisema taarifa za awali zilionyesha marehemu huyo aliondoka nyumbani kwao Aprili 24 mwaka huu kuelekea Kijiji cha Mkwaya kuchukua madaftari yake aliyoyaacha katika chumba alichokuwa amepanga kabla ya shule kufungwa kutokana na tatizo la ugonjwa wa Covid 19 unaosababishwa na virusi vya corona.

 Alisema marehemu huyo ambaye alikuwa ni mwanafunzi wa kidato cha pili katika  shule ya Sekondari ya Mkwaya tangu alipotoka nyumbani kwao, hakuonekana hadi mifupa na daftari zenye jina lake zilipopatika.

Kamanda Maigwa alilitaja tukio la pili kuwa ni la Saada Athuman aliyekadiriwa kuwa na miaka 25 hadi 30 kukutwa kwenye moja ya nyumba ya wageni iliyopo Mbinga mkoani Ruvuma  akiwa amefariki dunia .

 Alitaja tukio hilo kuwa lilitokea Mei 30 mwaka huu  saa saba mchana katika moja ya nyumba za wageni na kuwa marehemu alikuwa ni muhudumu wa bar iitwayo waungwana Pub.

 Alisema marehemu alienda kwenye nyumba hiyo akiwa na mwanaume aliyejiandikisha kwenye kitabu cha wageni kuwa ni Jakson Duma anayedaiwa kuwa ni dereva kutoka Tanga.

Alisema wakalala na ilipofika saa 12: 00 asubuhi, mwanaume huyo alirudisha funguo kwa muhudumu huku mlango ukiwa umefunga kwa nje.

Kamanda huyo alisema mwanaume huyo alidai anaenda kituo cha mabasi cha wilayani kuchukua gari lakini hakurudi tena.

 Alisema baada ya mtuhumiwa kutokomea, muhudumu wa nyumba wa nyumba hiyo aliingiwa na hofu baada ya kuona msichana hatoki chumbani hadi ilipofika saa saba mchana ndipo akaamua kutoa taarifa katika kituo cha polisi.

Alisema polisi walipovunja mlango walimkuta msichana akiwa amefariki dunia huku mwili wake ukiwa kitandani na mdomoni kunatokwa na mapovu.

Kamanda alisema kufuatia matukio hayo jeshi la Polisi mkoani humo linaendelea na uchunguzi ili kubaini vyanzo halisi vya vifo hivyo pamoja na kuwasaka wahusika .

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles