25.8 C
Dar es Salaam
Sunday, November 24, 2024

Contact us: [email protected]

Polisi kuchungunza vyama vya siasa

IGP Ernest ManguNa Patricia Kimelemeta, Dar e Salaam
JESHI la Polisi nchini limetangaza kuanza uchunguzi dhidi ya vikundi vyote vya ulinzi na usalama vinavyoanzishwa na vyama vya siasa nchini.
Pamoja na hili limesema kuwa litachunguza kwa kina mafunzo yanayotolewa na vyama hivyo kama yanahusiana na shughuli za kijeshi au laa.
Hatua hiyo ya Jeshi la Polisi imekuja siku moja baada ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kuzindua kikundi cha Ulinzi na Usalama (Red Brigade) katika mikoa ya Kanda za Nyanda za Juu Kusini.
Akizungumza na MTANZANIA jijini Dar es Salaam jana, Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP), Ernest Mangu alisema kuwa, sheria za nchi zimeweka wazi namna ya kuwapo kwa vikundi vya ulinzi na usalama na si kila mtu anaweza kuanzisha kikundi chake.
Alisema licha ya baadhi ya vikundi kutambulika lakini vingi hufanya kazi kwa utaratibu na kwa mujibu wa sheria za nchi.
IGP Mangu alisema hatua ya kila chama kuanzisha kikundi chake inaweza kusababisha vurugu hasa katika kipindi hiki cha kuelekea Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba mwaka huu.
Alisema kutokana na hali hiyo ni lazima Jeshi la Polisi liwe makini wakati wote kwa kuhakikisha wanafuatilia mwenendo vya vikundi hivyo na madhumuni ya kuanzishwa kwake.
“Tutachunguza vikundi hivyo ili tuweze kubaini mafunzo wanayopewa kama yanafanana na mafunzo ya vikosi vya ulinzi na usalama vinavyofanya kazi kwa mujibu wa sheria za nchi. Katiba ya nchi inavitambua vikosi vya ulinzi na usalama ambavyo vinafanya kazi kwa mujibu wa sheria.
“Kuanzishwa kwa vikundi vidogodogo ndani ya vyama vya siasa ambavyo vinafanya kazi ya ulinzi na usalama vinaweza kuhatarisha amani ya nchi, lazima tuchunguze ili tuweze kubaini mafunzo wanayopewa kama yanafanana na vikosi vya ulinzi na usalama au la, hapo tutajua ukweli zaidi,”alisema IGP Mangu.
Mkuu huyo wa Jeshi la Polisi alisema katika kipindi hiki cha kuelekea Uchaguzi Mkuu wa rais, wabunge na madiwani jeshi la polisi limejipanga kudhibiti vitendo vyote vya uvunjifu wa amani ambavyo vinaweza kuhatarisha hali ya usalama wa nchi na watu wake.
Alisema kutokana na hali hiyo, watahakikisha kuwa vikundi vinavyoanzishwa havifanyi kazi ya ulinzi na usalama kwa sababu siyo jukumu lao.
“Lazima tuwe makini hasa katika kipindi hiki cha kuelekea Uchaguzi Mkuu kwa kuhakikisha kuwa vikundi hivi vinavyoanzishwa haviwezi kuhatarisha amani ya nchi,” alisema.
Msajili aonya
Akizungumzia suala hilo, Msajili wa Vyama Vya Siasa nchini, Jaji Francis Mutungi alisema kuwa, sheria ya vyama vya siasa hairuhusu kuanzishwa kwa vikundi vya ulinzi na usalama, ila wanasiasa wamekuwa wakitafsiri tofauti.
Alisema kuna mambo mengi yanayofanywa na wanasiasa ambayo wanavunja sheria za nchi, lakini wanashindwa kujirekebisha na kujiona wako sahihi.
Alisema kutokana na hali hiyo, suala hilo ni nyeti sana, hivyo wanatakiwa kuelimishwa kwa kina ili waweze kujua majukumu yao ya chama na shughuli nyingine ambazo haziwahusu.
“Unajua hili suala ni nyeti sana, huwezi kulizungumzia ki uwepesi wepesi, kwa sababu lina upana wake, lakini wanasiasa wanalichukulia kikawaida bila ya kuangalia athari zake baadaye,”alisema Jaji Mutungi.
Aliongeza kuna matatizo mengi ya upotoshaji wa kisheria ndani ya vyama vya siasa, jambo ambalo linaweza kusababisha migongano ya wenyewe kwa wenyewe.
Alisema kutokana na unyeti wa suala hilo hawezi kulizungumzia kwa ufupi kwa sababu kuna masuala ya kisheria ambayo yanapaswa kufafanuliwa kwa kina zaidi ili jamii iweze kutambua ukweli kuhusu suala hilo.
“Lazima ifike kipindi vyama vya siasa vifuate matakwa ya sheria ya nchi kwa sababu ndiyo sheria mama inayoongoza nchi, bila ya kufanya hivyo tutakuwa tunavunja sheria kila siku,”alisema Jaji Mutungi.
Kwa muda mrefu vyama vya siasa hasa vya CCM, Chadema na CUF vimekuwa vitoa mafunzo kwa vijana wake kwa lengo la kuimarisha ulinzi na usalama hasa katika kipindi cha kuelekea Uchaguzi.
Mbali ya Chadema inayomiliki Red Brigade, CCM inamiliki kikundi cha Green Guard, huku cha CUF ikimiliki kikundi cha Blue Guard.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles