25.8 C
Dar es Salaam
Sunday, November 24, 2024

Contact us: [email protected]

Polisi hawa sita wachukuliwe hatua

Mwandishi wetu

KARIBU mwezi mmoja sasa umepita, tangu askari polisi sita wa Kituo cha Polisi Wilaya ya Igunga kukamatwa kwa tuhuma za kuomba rushwa ya Sh milioni 8 kwa mzee wa umri wa miaka 95.

Askari hao wanadaiwa kutenda kosa hilo katika Kijiji cha Isakamaliwa kwa mzee Ngaka Mataluma.

Inadaiwa kuwa siku ya tukio Juni 12, mwaka huu saa 2 asubuhi, askari hawa wakiwa na gari aina ya Toyota Land Cruiser yenye namba za usajili PT 1825, wakiwa na silaha za moto, walifika Isakamaliwa na kufanya mambo ambayo yako kinyume na sheria.

Lakini kibaya zaidi katika suala hili, askari hawa wanadaiwa kumbambikizia kesi Mataluma kuwa ni mganga wa kienyeji ambaye hana leseni ya uganga, jambo ambalo alilikana.

Baada ya kutoridhika waliingia ndani na kuanza kupekua nyumba nzima, huku wakiwa hawana hati ya upekuzi, na walipata rasta, kipande cha mifupa, kipisi cha msokoto wa bangi, ngozi ya kenge, kinyesi cha chatu na bunduki aina ya gobole.

Inadaiwa kuwa askari hao waliomba rushwa Sh milioni 20, lakini wakajadiliana hadi Sh milioni 8 ambazo wanadaiwa kupewa.

Baada ya kupewa fedha hizo, baadhi ya wasamaria wema wakaamua kukimbilia vyombo vya dola, hasa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kutoa taarifa za askari hao.

Baada ya taasisi hiyo kupata taarifa hizo, iliwasiliana na aliyekuwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora, Emmanuel Nley na kuagiza askari hao wakamatwe kwa mahojiano.

Askari hao walihojiwa kwa kina na kuonekana dhahiri wamehusika katika tukio hili, lakini kuanzia hapo hawajachukuliwa hatua zozote za kisheria, licha ya kuwapo na mazingira ya rushwa. 

Tunasema hivyo kwa sababu Kamanda Nley kabla ya kuhamishwa mkoani hapo alikiri kuwapo tukio hilo.

Baada ya kuhojiwa, walipelekwa Takukuru ambako nako walihojiwa na sasa kilichokuwa kinasubiri ni mwajiri wao awaondoe kazini ili wafikishwe mahakamani kujibu tuhuma zinazowakabili.

Askari hao, ni Inspekta Frank Matiku, PC Raphael Maloji, D.1 Koplo Paul Bushishi, PC Lome Laizer, DC Lucas Nyoni na Koplo Charles ambao wote wanafanya kazi Kituo cha Polisi Igunga.

Lakini pia katika tukio hili, walikuwapo viongozi wa Serikali  ambao ni Ofisa Mtendaji wa Kijiji cha Isakamaliwa, Edward Kitenya na Mwenyekiti wa Kitongoji cha Zahanati, Maulid Hamisi.

Kibaya zaidi askari hawa, inaelezwa siku ya tukio hawakutumwa na mamlaka yoyote kwenda Isakamaliwa, bali walitumwa kwenda Kata ya Itumba ambako kulikuwa kunafanyika uchaguzi wa diwani.

Jambo hili linatia doa kubwa Jeshi la Polisi ambalo limekuwa likilalamikiwa kwa baadhi ya askari wake kujihusisha na vitendo vya rushwa.

Pamoja na kazi nzuri inayofanywa na jeshi hili, tunategemea kuanzia sasa hatua zitachukuliwa ili kuondoa doa hili.

Sisi MTANZANIA, tunamshauri Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola ambaye kwa kweli anafanya kazi nzuri usiku na mchana, kuchukua hatua mara moja juu ya askari hawa ili haki itendeke.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles