Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital
JESHI la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam limetahadharisha wale wanaofikiria kufanya uhalifu siku ya Sikukuu ya Pasaka waache mara moja nakwamba watashughulikiwa ipasavyo kwani jeshi liko imara kuhakikisha hali ya usalama inakuwa shwari
Akizungumza na Waandishi wa Habari Aprili 6,2023 jijini Dar es Salaam, Kamanda wa Kanda Maalumu wa Dar es Salaam, SACP Jumanne Muliro amesema Polisi hawatasita kufuatilia watu watakaotaka kupanga njama za kufanya uhalifu.
“Jeshi la polisi halitalala kwani kila sikukuu kumekuwa na baadhi ya watu wanaotumia siku hizo vibaya, hivyo jeshi litaendelea kufanya doria kila mahali,” amesema.
Hata hivyo, amewaomba Wazazi,Walezi siku ya sikukuu kuwa karibu na watoto katika siku hiyo kwani kunakuwa na kupotea kwa watoto hivyo amewasihi ni bora wasiwaruhusu kwenda kwenye kumbi za starehe wakiwa wenyewe bora wawazuie.
Akizungumzia hali ya usalama katika Kanda Maalum ya Dar es Salaam amesema ni shwari ikilinganishwa na miaka ya nyuma ambapo kulikuwa na matukio mbalimbali ikiwemo mtu kuporwa fedha akitokea benki bila kukamatwa lakini sasahivi jeshi hilo linapaswa kupongezwa kwa operesheni kali inayofanyika kila siku chini yake.