23 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

Marekani kujenga kiwanda cha kuchakata madini ya Nikel

Na Beatrice Kaiza, Mtanzania Digital

Serikali ya Marekani imetoa ahadi kwa Serikali ya Tanzania, kujenga kiwanda kikubwa nchini Tanzania, ambacho kitakuwa cha pekee barani Afrika, cha kuchakata madini ya Nikel yanayotumika kutengenezea betri za gari zinzotumia umeme kwa ajili ya soko la Marekani na duniani ifikapo mwaka 2026.

Mradi huo unatarajiwa kutekelezwa na kampuni za Life Zone Metals na TechMet zinazomilikiwa kwa ubia na Serikali ya Marekani kupitia Shirika la Fedha la Maendeleo ya Kimataifa la Marekani (DFC) ambapo utachochea ongezeko la ajira kwa watanzania, na kuchangia katika pato la Taifa.

Hayo ameyabainishwa Aprili 6,2023, jijini Dar es Salaam na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dk. Stergomena Tax wakati akizungumza na Waandishi wa Habari juu ya mafanikio ya ziara ya Makamu wa Rais wa Marekani nchini, Kamala Harris ambayo amekuwa kuwa imekuwa na mafanikio makubwa katika kuimarisha na kufungua maeneo mapya ya ushirikiano kati ya Tanzania na Marekani.

Aidha, Dk. Tax amesema katika ziara hiyo hati mbalimbali za makubaliano zilisainiwa ikiwemo mkataba wa msaada wa Maendeleo kati ya Tanzania na Serikali ya Marekani kupitia USAID na Hati ya Makubaliano kati ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Marekani.

“Mkataba wa Msaada wa Maendeleo kati ya Tanzania na Serikali ya Marekani kupitia USAID wa kiasi cha dola bilioni 1.1 kwa ajili ya miradi mbalimbali ya kijamii na kiuchumi ulisainiwa.

“Hati ya Makubaliano kati ya Tanzania na Marekani ilisainiwa. Kupitia Makubaliano hayo serikali ya Marekani itatoa ushauri wa kitaalam na kujenga uwezo kwa wataalam kuhusu usimamizi wa bandari za Tanzania, hususan katika upanuzi wa bandari, vifaa vya kisasa na uendelezaji wa Bandari,” amesema Dk. Tax.

Mbali na hayo amesema mkataba huo na Hati za Makubaliano hizo zilizosainiwa, Tanzania itanufauka kupitia ahadi mbalimbali zilizotolewa na serikali ya Marekani.

“Mpango huo unalenga kusaidia wakulima nchini, hususan wanawake na vijana katika kukabiliana na changamoto za usalama wa chakula.

“Aidha, mafanikio mwengine ni Serikali ya Marekani kutoa zaidi ya dola bilioni 1.0 kwa ajili ya kuwawezesha wanawake wa Afrika walio katika sekta ya Umma, na sekta binafsi kushiriki shughuli za kiuchumi na kijamii.

“Tanzania pia itanufaika na serikali ya Marekani kupitia Shirika la Msaada la Marekani USAID kwa kupata dola 600,000 kwa ajili ya kushirikiana na kampuni za mawasiliano na teknolojia ya sekta binafsi na serikali ili kupanua huduma za nishati safi na kutoa umeme kwa takriban vituo 100 vya afya katika maeneo ya magharibi, kati, na kusini mwa Tanzania,” amesema Dk. Tax na kuongeza kuwa:

“Mradi huo utawezesha kampuni za mawasiliano ya simu kuimarisha huduma za takwimu na kuwezesha vituo vya afya kutumia mifumo ya kidijitali katika utoaji wa huduma,”.

Amesema eneo jingine ambalo Tanzania itanufaika nalo ni kuanzisha majadiliano ya kuongeza muda wa ukomo wa visa (Visa ya miaka mitano).

“Serikali ya Tanzania itanufaika kuendelea kuwekeza katika Mpango wa Dharura wa Rais wa Kusaidia UKIMWI (PEPFAR) ambapo Marekani inapanga kuwekeza dola milioni 433 katika kipindi cha miaka miwili ijayo,” amesema Dk. Tax.

Tax amesema Tanzania itanufaika pia kwa Serikali ya Marekani kuingia makubaliano na Tanzania yatakayowezesha Marekani kuuza bidhaa za usafirishaji, uchukuzi, teknolojia ya digitali na nishati safi zenye thamani ya dola milioni 500.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles