Na PENDO FUNDISHA-MBEYA |
KATIBU wa Itikati na Uenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Humphrey Polepole, amewataka wanachama wa chama hicho kuacha kutafuta uongozi kwa kutumia makundi na ukabila.
Kauli hiyo aliitoa jana jijini Mbeya, alipokuwa akizungumza na wajumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM ya mkoa huo, ambapo alisema kuwa moja ya mambo ya ovyo yanayokitesa chama hicho ni baadhi ya watu kutafuta uongozi kwa makundi na ukabila jambo linalotoa fursa kwa wapinzani kushinda uchaguzi.
Alisema suala la ukabila na makundi limesababisha vijana wa Mkoa wa Mbeya kukosa mwelekeo na kuyumba hivyo viongozi wa chama hicho wanapaswa kubadilika.
“Kama kuna jambo la ovyo kabisa kwenye chama chetu ni hili la kuendelea kucheka na makundi pamoja na kuukumbatia ukabila, mambo haya yanaturudisha nyuma.
“Makundi yanatugawa, yanadhoofisha umoja wetu, yanaleta chuki, yanapunguza upendo na kutuacha tukiwa dhaifu mbele ya adui,” alisema Polepole
Alisema CCM inatafuta na kuweka kiongozi atakayehudumia wananchi kwa usawa na haki badala ya kuwagawa watu kwa makundi na ukabila.
“Msitupe viongozi kazi ya kuja kuvunja makundi, hatuwezi kupoteza muda na kama mtafanya mchezo wengi wetu tumewaona vijana wanavyoumia kwa kuwanyima haki yao ya uongozi na kwamba kabila za Mbeya si za nchi nzima,” alisema
Alisema makabila hayana faida yoyote zaidi ya kuwakumbusha watu walipotoka, hivyo viongozi wa CCM Mkoa wa Mbeya, wanapaswa kubadilika na kufanya kazi kwa bidii kama Mwenyekiti wa CCM, Rais Dk. John Magufuli alivyoelekeza.
Alisema watu wa Mbeya wanamwamini Rais Dk. Magufuli kwa sababu ya kazi ya kuleta maendeleo kwa nchi na watu wake, inayofanya na Serikali anayoiogoza.
Aidha, aliwataka viongozi na watendaji wa Serikali kufanya kazi kwa bidii pamoja na kutekeleza ilani ya CCM huku akionya kuwa viongozi dhaifu watachukuliwa hatua za kinidhamu kwa mujibu wa utaratibu na sheria za nchi zinavyoelekeza.