Na THERESIA GASPER -DAR ES SALAAM
KOCHA Mkuu wa Yanga, Hans van der Pluijm, amesema timu yake bado ina nafasi ya kusonga mbele kwenye hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho barani Afrika, licha ya kukosa ushindi katika michezo mitatu waliyocheza.
Yanga ambayo imepangwa Kundi A kwenye michuano hiyo, juzi ililazimishwa sare ya bao 1-1 dhidi ya Medeama ya Ghana katika mchezo uliochezwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Matokeo ya juzi yaliiwezesha Yanga kuambulia pointi moja na kuendelea kushika nafasi ya mwisho katika kundi hilo, baada ya awali kuchapwa bao 1-0 dhidi ya Mo Bejaia ya Algeria ugenini kabla ya kupata kipigo kama hicho nyumbani walipocheza na TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).
Akizungumza jijini Dar es Salaam baada ya mchezo wa juzi, Pluijm alisema walikuwa na malengo ya ushindi lakini bahati haikuwa upande wao hivyo kazi kubwa iliyobaki ni kuongeza umakini katika mechi zijazo ili kupata pointi tatu muhimu.
Kocha huyo raia wa Uholanzi, alisema baada ya kufungwa nyumbani na TP Mazembe walielekeza hesabu zao katika mchezo unaofuata dhidi ya Medeama, lakini mambo yamekwenda tofauti na matarajio yao.
“Mpira wa miguu ni mchezo wa makosa, tulipata nafasi nyingi za kufunga lakini wachezaji walishindwa kuzitumia vyema hali iliyosababisha kupatikana matokeo ya sare.
“Leo (juzi) wachezaji wamecheza kwa kiwango tofauti kabisa na mchezo uliopita, nitaendelea kurekebisha makosa yaliyojitokeza na kuwapa mbinu mpya za kupambana uwanjani ili tufanye vizuri zaidi na kujiweka katika mazingira mazuri,” alisema.
Matokeo ya juzi yamezidi kuiweka Yanga pabaya, huku ikiendelea kushika nafasi ya mwisho katika Kundi A ikiwa imejikusanyia pointi moja.
Yanga sasa inajipanga kuwakaribisha MO Bejaia katika mchezo wa marudiano utakaochezwa uwanja wa Taifa.
Hata hivyo matumaini ya Yanga kusonga mbele yalitegemea matokeo ya mchezo wa jana kati ya TP mazembe na Mo Bejaia uliotarajiwa kuchezwa nchini Algeria.