27.1 C
Dar es Salaam
Thursday, January 2, 2025

Contact us: info@mtanzania.co.tz

Pinda aonya matumizi ya rushwa uchaguzi mkuu

Waziri Mkuu Mizengo Pinda
Waziri Mkuu Mizengo Pinda

Na Mwandishi Wetu

WAZIRI Mkuu, Mizengo Pinda, amewaonya Watanzania kuwa makini na watu wanaotumia rushwa ili kupata nafasi za uongozi na hasa kwenye uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika mwaka 2015.

Waziri Mkuu Pinda ametoa onyo hilo jana alipokuwa akizungumza na mamia ya waumini na viongozi mbalimbali waliohudhuria ibada ya uzinduzi wa Dayosisi mpya ya Ruvuma ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) na kuwekwa wakfu Askofu Amon Mwenda aliyeteuliwa kuongoza dayosisi hiyo.

“Ninawasihi wananchi wawe makini na viongozi wanaopenda kutoa rushwa hasa katika kipindi hiki cha kuelekea kwenye uchaguzi mkuu. Kama mtu ana nia ya kweli ya kuongoza ni kwanini atumie fedha ili kupata nafasi ya uongozi?

“Tatizo ni kwamba, hata wananchi hivi sasa wanakubali kupokea kile kinachotolewa na wagombea. Atakuja huyu atakupa hiki na mwingine naye atakupa kile, lakini ujue akiingia madarakani anaanza kurudisha haraka vile alivyowagawia,” alisema Waziri Mkuu.

Aliwaonya wananchi kuwa makini ili wasije wakageuzwa mtaji wa kuwanufaisha watu binafsi. Tukikubali kutumika tutapata viongozi wakati wa uchaguzi, lakini viongozi hao watakuwa ni wale wasiokuwa na hofu ya Mungu bali hao watakuwa ni wenye kujali masilahi yao kuliko ya wananchi waliowachagua,” aliongeza.

Aliwaomba viongozi wote wa dini waliohudhuria sherehe hizo pamoja na waumini wote, waendelee kuliombea taifa ili Mungu aliepushe na janga la watu kupenda rushwa. Alitumia fursa hiyo pia kuwaomba wazidi kuuombea mchakato wa kupata Katiba Mpya ili wabunge wote warejee ndani ya Bunge na kuikamilisha kazi waliyoianza.

Pamoja na hayo, alimuomba askofu huyo mpya apokee jukumu hilo kwa mikono miwili na kumuahidi kuwa kama Serikali watakuwa naye bega kwa bega kuwaongoza Watanzania walioko kwenye dayosisi yake.

Awali akitoa hotuba yake ya kwanza baada ya kusimikwa rasmi, Askofu Mwenda alisema Dayosisi mpya ya Ruvuma imeanzishwa katika kipindi chenye changamoto nyingi za kidunia na utandawazi ukiwemo mmomonyoko wa maadili.

Hata hivyo, akiainisha malengo ya dayosisi hiyo ambayo anakuwa Askofu wake wa kwanza, Askofu Mwenda alisema mbali ya kufundisha neno la Mungu, dayosisi hiyo itahimiza ufanyaji kazi ili wakazi wake wawe na akiba ya chakula cha kutosha.

Alisema watashirikiana na Serikali na wadau wa ndani na nje ya nchi, katika kutoa huduma za kijamii hasa elimu na afya. Aidha, alisema atakabiliana na changamoto za sasa ambazo alizitaja kuwa ni mmomonyoko wa maadili, rushwa, mauaji ya albino, unyanyasaji wa wanawake na watoto pamoja na ubakaji.

Akitoa shukrani kwa niaba ya waumini wa kanisa hilo, Askofu Mkuu wa KKKT, Dk. Alex Malasusa, alisema kanisa lingependa kupata viongozi ambao ni wacha Mungu na kuonyesha mshangao kwa baadhi ya watu wanaogombea uongozi wakati hawana mapenzi na Mungu.

“Bila kujali imani ya mtu, tungependa kupata kiongozi mcha Mungu ambaye atakuwa akihudhuria ibada na awe anampenda Mungu kwani hapo ndipo atakapokuwa akiwapenda watu anaowaongoza.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
593,000SubscribersSubscribe

Latest Articles