Na KHAMIS SHARIF- ZANZIBAR
GIZA nene limetanda Visiwani Zanzibar baada ya kukosekana petroli na dizeli kwa wiki ya tatu sasa.
Hali hiyo imesababisha baadhi ya wananchi wanaotumia vyombo vya moto kulazimika kuviegesha majumbani kwao.
Licha ya kuingizwa tani 900, ambazo ni sawa na lita milioni 1,700,000 ambazo zinatosha kwa siku saba, bado misururu ya magari imetamalaki kwenye vituo vya mafuta.
Wakizungumza na MTANZANIA jana, baadhi ya wananchi mjini Unguja, walisema suala la uhaba wa mafuta kwa kipindi hiki limevunja historia huku wakiamini kuwa huenda kuna uzembe kwa watendaji waliopewa mamlaka ya kusimamia sekta hiyo.
“Hali ya ukosefu wa mafuta ni mbaya sana, wiki ya tatu sasa bado foleni ni kubwa na kuhitaji mafuta unalazimika kuamka asubuhi sana au jioni.
“Nimeweka mafuta ya Sh 30,000 nimezunguka sasa yamekwisha nimekuja kuweka hapa sheli lakini sijui kama nitapata maana mtu fedha huduma hakuna.
“Na bahati mbaya hata vidumu havitakiwi hapa sheli,” alisema Said AbdallaH Mohamed mkazi wa Bububu.
Naye Simai Ali Makame, alisema suala la ukosefu wa mafuta linatakiwa kuangaliwa na serikali.
Alisema kwa sasa baadhi ya shughuli zimesimama na kama hatua hazitachukuliwa nchi inaweza kuathirika uchumi.
“Hivi kwa hali hii ni nani anaweza kwenda kufanya shughuli zake hasa kwenye maeneo ya nje ya hapa mjini?
“Sasa badala ya kwenda kwenye uzalishaji mtu unakaa foleni kusubiri mafuta sheli, jambo hilo linatakiwa kuangaliwa kwa makini sana,” alisema Makame.
Juzi, Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi, Nyumba, Maji na Nishati Ali Khalil Mirza, alilazimika kufanya ziara katika Kituo Kikuu cha kuhifadhia mafuta kilichopo Mtoni nje kidogo ya mji wa Unguja.
Akiwa katika kituo hicho, alifanya kikao na uongozi wa Kampuni za Zanzibar Petroleum (ZP) na kuelezwa kuwa meli ya kampuni hiyo imeshawasili Zanzibar na jana yangeaanza kusambazwa mafuta katika vituo vyote vya Zanzibar.
Pamoja na hilo Katibu Mkuu Mirza, pia alitembelea Kampuni ya United Petroleum (UP) inayomiliki meli ya M.V. United Spirit ambayo kwa sasa ipo katika hatua za mwisho kufanyiwa matengenezo baada ya kupata hitilafu wiki mbili zilizopita ikiwa njiani kuleta mafuta visiwani Zanzibar.
Viongozi wa United Petroleum walimweleza Katibu Mkuu huyo kwamba ifikapo kesho Novemba 8, mwaka huu, meli yenye uwezo wa kubeba tani 3,000 za mafuta, itafanyiwa majaribio ya mwisho kabla ya Ijumaa Novemba 9, kwenda bandari ya Dar es Salaam kupakia mafuta ambayo yatapelekwa Zanzibar.
Hata hivyo katika taarifa iliyotolewa kwa waandishi wa habari juzi na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Huduma za Maji na Nishati (ZURA) Haji Kali Haji, taratibu za kushushwa katika meli zimeshaanza ili kusambazwa vituoni.
Mkurugenzi huyo alisema kati ya lita hizo, lita 1,295,632 za petroli zitatumika Unguja na Pemba lita 400,000 zitasambazwa.
Kuhusu dizeli, alisema lita 2,047,914 zitasambazwa Unguja huku lita 250,000 zikipelewa Pemba ambako yanaweza kutumika kwa siku 11.
Alisema mafuta hayo yameingizwa nchini na meli ya MT East Wind inayotumiwa na Kampuni ya Zanzibar Petroliam Limited (ZP), ambayo inatarajiwa kurudi tena katika bandari ya Mombasa kupakia tani 1,500 za mafuta ikiwa ni sawa na lita 2,000,000 na itawasili Zanzibar Novemba 4 mwaka huu.
Alisema ZURA imesikitishwa na uhaba wa mafuta uliojitokeza ambao umewasababishia wananchi kukosa huduma za kawaida.
Hivyo kutokana na hali hiyo, ZURA imeyaagiza makampuni ya mafuta kuhakikisha yanasambaza mafuta kwa haraka na kurejesha huduma hiyo kwa wananchi na kuhakikisha inapatikana bila ya usumbufu.
ZURA pia imewaomba radhi wananchi kwa usumbufu uliojitokeza na kueleza kwamba inafuatilia kwa karibu matengenezo ya meli mbili zilizoharibika kuhakikisha upatikanaji wa mafuta nchini unarejea kama kawaida.