29.2 C
Dar es Salaam
Saturday, November 30, 2024

Contact us: [email protected]

Petit Afro: Afro Dance inaoondoa ‘stress’ Ulaya

CHRISTOPHER MSEKENA

PETIT Afro ni miongoni mwa majina makubwa kwenye sanaa ya kucheza muziki Afrika na bara la Ulaya kutokana na umahiri wake wa kudansi mitindo ya Kiafrika kwa kutumia muziki wenye vionjo na ladha za Afrika.

MTANZANIA limefanya mahojiano na Petit Afro, dansa nyota kutoka Tanzania anayefanya shughuli zake nchini Holland, Hispania na nchi nyingine za Ulaya.

MTANZANIA: Kwanini uliamua kuingia kwenye sanaa kama dansa na sio mwanamuziki au mwigizaji?

MTANZANIA: Toka zamani nilikuwa napenda  kuimba, kucheza na kuigiza ila kwenye suala la kucheza na kuigiza ndio nilikuwa naweza kuliko kuimba.

Ndio maana kwenye video zangu za dansi mara kwa mara huwa naweka maigizo ya vichekesho kidogo. Hivi karibuni nilitoa pia wimbo wa komedi unaitwa Nyonga, nilichagua kudansi kwa sababu ndio kitu ambacho naweza kuliko hivyo vingine.

MTANZANIA: Umefanya sanaa ya dansi kwa muda gani na kuna mafanikio yoyote umeyapata ambayo kijana mwingine anaweza kuiga kutoka kwako?

Petit: Mimi nimedansi toka nikiwa mdogo ila toka nimeanza kufanya kazi ya kufundisha sasa ni mwaka wa nane, mafanikio mengi tu nimepata. Nafundisha watu ‘dansi’ ndani na nje ya nchi.

Nimeshinda shindano la Everybody Dance Now nchini Holland, nimetumbuiza kwa Malkia wa zamani wa Holland, nimetumbuiza na P Square, nimeweza kuwa na mahusiano ya kikazi na wasanii wakubwa kama Diamond Platnumz, Rayvanny, P Square, Yemi Alade, Jay Martin na wengine wengi wa huku Ulaya ambao ni wakubwa pia.

MTANZANIA: Kwanini uliamua kuwafundisha zaidi watoto kuliko watu wazima?

Petit: Kwa sababu ya mimi mwenyewe nilivyo, watu wanasema nina ucheshi fulani basi ikatokea tu watoto wakaanza kunipenda na madarasa yangu ya watoto yakawa yana jaa zaidi.

Harafu pia watoto wana muda mwingi wa kujifunza kwahiyo wakawa wanakuja kila wakati tofauti na wakubwa mara nyingi wapo kazini ila nafundisha wote wakubwa na watoto.

MTANZANIA: Kuna tofauti yoyote ya kufundisha watoto na watu wazima?

Petit: Mtoto inakuwa rahisi kidogo kwa sababu mtoto hajishtukii akiwa anakosea stepu, yaani mtoto yeye hata hajali, yeye anacheza tu ilimradi anafurahi. Kutokana na hivyo watoto wanakuwa mwisho wa siku watajua kucheza kwa sababu hawaogopi kufanya makosa.

Watu wazima mara nyingi wanaogopa kukosea, ikitokea wamekosea mara mbili mara tatu anaanza kujishtukia wengine wanaacha au wanasema ‘aah utu uzima tena’ au ‘aah mi mzito’.

MTANZANIA: Mwaka jana ulisema unakuja na mpango wa kufungua madarasa kwenye nchi za Tanzania, Uganda, Afrika Kusini na nyinginezo, je mpango umeishia wapi?

Petit: Huo mpango bado ninao, mwaka jana nilikuja Afrika kuangalia mazingira na mambo yanavyokwenda pia kuzungumza na wadau mbalimbali.

Corona ikiisha nitakuja kuanzisha mradi wangu wa kwanza Tanzania pia nina mpango wa kufanya ziara nchini Marekani.

MTANZANIA: Kuna changamoto gani unapata katika kukuza mitindo ya kucheza ya Kiafrika kwenye bara la Ulaya?

Petit: Changamoto inakuja pale baadhi ya watu weusi wa huku hawapendi kuona wazungu wakicheza Afro Dance, wengi wanasema wazungu wanaiba tamaduni zetu. Mimi ninacho amini kuwa dansi ni kitu cha furaha na cha kila mtu. Huwezi amini wazungu wanapenda sana dansi zetu na ndio wapo mstari wa mbele kutusapoti na ndio wanalipa kuja kujifunza.

MTANZANIA: Unadhani kwanini Afro Dance inapendwa kwenye mataifa ya Ulaya?

Petit: Ujue huku Ulaya nchi nyingi watu wana stresi, sasa hii Afro Dance na Afro Music imekaa kiraha raha ndio maana wanapenda, yaani wanapunguza stresi halafu ni kitu ambacho wao hawana, wazungu wanapenda kujaribu vitu vipya.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles