BAADA ya Manchester City kutoka suluhu dhidi ya Norwich City, kocha wa timu hiyo, Manuel Pellegrini, amedai kwamba bado ana nafasi ya kutwaa ubingwa huo.
Klabu hiyo kwa sasa ipo nyuma kwa pointi tisa dhidi ya vinara Leicester City ambao wanaongoza wakiwa na pointi 60, lakini Pellegrini anaamini ana nafasi kubwa ya kutwaa ubingwa huo kutokana na michezo iliyobaki.
Manchester City wamejipatia pointi tatu katika michezo mitano ya mwisho, huku wakiwa wamebakiwa na michezo tisa kumaliza ligi msimu huu.
“Kila siku ukiwa unapoteza pointi inaumiza kichwa, lakini kikubwa ni kufikiria juu ya michezo inayofuata, kinachofuata sasa ni kufanya hesabu ili kuona uwezekano wa kuchukua ubingwa msimu huu.
“Hatupendezwi na matokeo kwa sasa kwa kuwa kila siku tunazidi kuongeza nafasi ya kuwafikia waliotangulia mbele, tulianza vizuri msimu huu lakini kwa sasa tumeyumba ila bado tuna nafasi ya kuendelea kufanya vizuri na kuchukua ubingwa msimu huu,” alisema Pellegrini.