NA MWALI IBRAHIM, DAR ES SALAAM
KOCHA Mpya wa Simba, Patrick Phiri, anatarajia kutua leo nchini na kukabidhiwa mikoba ya aliyekuwa kocha wa timu hiyo, Mcroatia Zdravko Logarusic, aliyefungashiwa virago vyake mwishoni mwa wiki iliyopita.
Phiri anatarajia kuwasili majira ya saa 8 mchana kwa ndege ya Shirika la Ndege la Fastjet akitokea nchini kwao Zambia.
Akizungumza na MTANZANIA jana, Rais wa Klabu ya Simba, Evans Aveva, alithibitisha ujio wa kocha huyo leo, huku akidai kuwa walikuwa wanaendelea kumalizia mipango ili aanze safari.
“Kweli kocha anawasili kesho (leo) na hapa tunafanya mpango wa tiketi yake ya ndege, kuhusu suala la mkataba atakapowasili ndiyo tutakaa naye na kuamua kuingia mkataba wa mwaka mmoja au miwili,” alisema.
Phiri ni kocha mwenye historia nzuri na klabu hiyo msimu wa ligi kuu wa 2009/2010, ambapo aliweza kuisababishia timu yake hiyo kutwaa ubingwa wa ligi hiyo bila kufungwa mchezo hata mmoja.
Licha ya kuweka rekodi hiyo, lakini pia amewahi kunyakuwa ubingwa wa ligi kuu mara mbili akiwa na timu hiyo ambapo pia timu yake hiyo ilikuwa mabingwa 2004/2005, baadaye aliamua kuiacha Simba kwa sababu zake binafsi na kumpa mikoba kocha Milovan.
Hata hivyo, Phiri atakabidhiwa timu ikiwa tayari imeshafanya usajili wa baadhi ya wachezaji, huku ikiwa inawaangalia wachezaji watatu, Modo Kiongera wa Kenya, Jerome JJ wa Botswana na Osumani Mane wa Senegal, ambapo atachagua mchezaji mmoja atakayesajiliwa na klabu hiyo ambayo inatarajia kuweka kambi Zanzibar.
Licha ya Simba kufanya mabadiliko ya Kocha Mkuu, lakini benchi la ufundi litabaki vile vile ambapo atasaidiana na kocha Selemani Matola.