PATACHIMBIKA ndilo neno linaloakisi ushindani mkubwa wa kisiasa unaotarajiwa kutokea baada ya pazia la kampeni za wagombea urais, ubunge na udiwani kufunguliwa rasmi leo.
Ushindani huo unatarajiwa kuwa mkali zaidi kuliko chaguzi zilizopata kufanyika huko nyuma na hali hii inachagizwa zaidi na uhalisia wa mazingira ya kisiasa ambayo yalianza kuonekana mapema kabisa kabla ya
kampeni kuanza.
Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambacho kimemsimamisha Dk. John Magufuli kugombea urais, ndicho kinachotazamwa kukumbana na upinzani mkali kutoka Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), ambacho kimemsimamisha Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa kuwania nafasi hiyo.
Lowassa, ambaye awali aliwania urais kupitia CCM lakini jina lake likakatwa kimizengwe na kuamua kuchukua uamuzi wa kujiunga Chadema, ataendesha kampeni zake chini ya uungwaji mkono mkubwa wa kisiasa
kutoka muungano wa vyama vinne vya siasa vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).
Vyama hivyo ni pamoja na Chadema yenyewe, Chama cha Wananchi (CUF), NCCR- Mageuzi pamoja na National League for
Democracy (NLD).
Pia ushindani huo wa Ukawa na CCM utafuatwa kwa nyuma na vyama vingine vya upinzani ambavyo vimesimamisha wagombea urais, ubunge na udiwani.
Vyama hivyo ni pamoja na United People’s Democratic Party (UPDP), Tanzania Labour Party (TLP).
Vingine ni Alliance for Democratic Change (ADC) na Alliance for Change and Transparency (ACT-Wazalendo) na CHAUMMA.
Hata hivyo, macho na masikio ya Watanzania yatajielekeza zaidi katika ushindani mkali wa kisiasa baina ya CCM na Ukawa, kuanzia ngazi ya urais hadi ubunge na udiwani.
Tayari kuna mtazamo uliowazi kwamba Dk. Magufuli na Lowassa ndio waliohodhi mbio za kuwania urais kutokana na nguvu za kisiasa walizonazo kupitia vyama vyao.
Kwa upande wa Lowassa, nguvu yake ya kisiasa imejipambanua kwa kupata mwitikio mkubwa wa wananchi, wakiwamo baadhi yaNmakada wa CCM waliomo ndani ya chama hicho na wale waliokitosa na kuungana naye
ndani ya jahazi la Ukawa.
Pia wakereketwa wa vyama vyote vine vinavyounda Ukawa pamoja na kundi la watu wasiokuwa na mfungamano wowote wa kisiasa.
Lowassa amekuwa ni mwanasiasa aliyevunja ama kuweka historia mpya ya kupata wafuasi wengi kwa kila jambo la kisiasa na kijamii alitendalo sehemu yoyote.
Ndani ya kipindi kifupi cha kuteuliwa kwake kuwa mgombea urais kupitia Ukawa, kumeshuhudiwa maelfu ya wananchi wakijitokeza katika mikutano ya kutambulishwa kwake.
Nguvu ya Lowassa katika siasa za uchaguzi mkuu wa mwaka huu zimekuwa na picha ya kuvuta hisia za watu na kusababisha maandamano ya maelfu ya wananchi mijini na vijijini, hadi kufikia mahali Jeshi la Polisi nchini kutumia nguvu ili kuzuia maandamano ya mashabiki wanaomuunga
mkono.
Wakati hali ikiwa hivyo kwa Lowassa, kwa upande wake mgombea
urais wa CCM, Dk. Magufuli amekuwa na mwitikio wa wastani kutoka kwa wananchi wanaomuunga mkono.
Hata hivyo, mwitikio huo umegawanyika katika mitazamo miwili, kwamba wapo wanaomfuata kwa mapenzi ya chama na wengine wanamuungamkono kama mgombea urais.
Dadisi za kisiasa zinatanabahisha hali hiyo inatokana na uhalisia wa kwamba mwanasiasa huyo hakujijenga kisiasa na kujiandaa vya kutosha
kupata dhamana aliyopewa na chama, lakini zaidi CCM inakabiliwa na changamoto ya kuchokwa.
Kwamba pamoja na kwamba wananchi hawana tatizo na utendaji wake, lakini kumekuwa na ugumu wa kiasi wa kubadili fikra za wengi kutoka
katika mtazamo wa utendaji na kumtambua kuwa ndiye mwanasiasa anayeweza kuleta mabadiliko katika serikali ijayo.
Tofauti na mwitikio anaoupata Lowassa, ambaye kwa muda mrefu si
yeye tu, bali hata upande alikokwenda kumebeba dhana na matumani
ya kuleta mabadiliko, jambo ambalo limemfanya aonekane tishio dhidi ya
CCM.
Kutokana na hilo, CCM kinadaiwa kuandaa mbinu mbalimbali ili kudhoofisha nguvu hiyo ya kisiasa anayoipata
Waziri Mkuu huyo wa zamani.
Inaelezwa kwamba, hali hiyo ndiyo inayotajwa kuulazimu uongozi wa chama hicho kuunda timu ya watu 32 ya kampeni kwa ajili ya kumkabili
mwanasiasa huyo.
Ndani ya timu hiyo wapo watu kama Samuel Sitta, Makongoro Nyerere, Bernard Membe, Dk. Harrison Mwakyembe, Steven Wassira na January
Makamba, ambao kwa pamoja misimamo yao ya kisiasa imekuwa
wazi ya kumpinga ama imejijenga katika mtazamo wa uadui dhidi ya Lowassa.
Mbali na timu hiyo, pia CCM kimeunda kamati maalumu itakayokuwa
na jukumu la kumshughulikia Lowassa katika mtazamo hasi ndani ya kipindi chote cha kampeni.
Tayari picha na video za propaganda dhidi za Lowassa ambazo zinahusishwa kuandaliwa na kamati hiyo zimeanza kusambazwa kwenye mitandao mbalimbali ya kijamii hapa nchini.
ILANI
Jambo jingine ambalo linabeba umuhimu mkubwa na pengine litatazamwa kwa ukaribu na wapiga kura katika uchaguzi huu ni ilani za vyama vinavyopambana katika kinyang’anyiro hiki.
Tayari CCM imekwisha ainisha mambo makuu manne ambayo itakwenda
kushughulika nayo iwapo itapatiwa nafasi nyingine ya kuongoza.
Mambo hayo ni pamoja na kupambana na umaskini, ajira kwa vijana,
ulinzi na usalama na kupambana na rushwa kwa kuanzisha mahakama
maalumu.
Katika jambo hili CCM itakabiliwa na upinzani mkali kuanzia kwa mgombea wake wa urais hadi majimboni, hasa kutokana na kwenda kinyume cha matarajio ya wengi kuhusiana na kauli mbiu yake ambayo iliitumia katika chaguzi za mwaka 2005 na 2010 ya Maisha bora kwa kila Mtanzania, lakini pia ikitekeleza baadhi ya ahadi na nyingine ikishindwa.
Ukawa na Lowassa ambaye kwa miaka mingi amekuwa akibeba ajenda
ya elimu, tatizo la ajira kwa vijana na kupambana na umaskini, ajenda ambazo sasa zinaonekana kupokwa na CCM, nayo itapimwa kulingana na
ilani yao.
Mwaka 2010 moja kati ya mambo yaliyovuta hisia za wapiga kura wengi
kiasi cha kukivuruga CCM ni ilani ya Chadema, ndani yake ikiwa na ahadi
ya upatikanaji wa Katiba Mpya, jambo ambalo licha ya Rais Jakaya Kikwete
kuonekana kutaka kulishughulikia, lakini limemshinda.
Jambo jingine ni suala la elimu bure, ambapo CCM imeamua kulichukua
na kulifanyia kazi, lakini utekelezaji wake umekuwa ni wa mashaka.
Pia suala la kushusha gharama za vifaa vya ujenzi ili kila Mtanzania awe na uwezo wa kujenga nyumba bora.
Â
WABUNGE, MADIWANI
WANAORUDI
Uchaguzi huu pia unaweza kuwa mtamu au mchungu, hususan kwa wagombea wa ngazi za ubunge na udiwani ambao wanarudi kuwania nafasi
hizo kwa mara nyingine.
Kwa wagombea ambao walishindwa kutekeleza ahadi zao sawasawa na zaidi bila kuwa na sababu za msingi, wanaweza kujikuta wakikabiliwa na
changamoto kubwa tofauti na wale waliotekeleza ahadi zao.
Lakini pia hilo linaweza kuwakuta
wagombea wengine ambao wanarudi lakini wametekeleza ahadi zao na wale wanaoingia kwa mara ya kwanza.
Upo uwezekano pia wapiga kura wakawaangusha katika sanduku la kura kwa sababu ya ama kukumbwa na kashfa au kwa makosa yaliyofanywa na vyama vyao.