MAPUTO, MSUMBIJI
KIONGOZI wa Kanisa Katoliki duniani, Papa Francis amekamilisha ziara yake nchini Msumbiji.
Papa amewasihi viongozi wa kisiasa na kiuchumi wa nchi hiyo yenye utajiri mkubwa wa mali ghafi wasikubali kuhongwa na watu kutoka nje.
Jana Papa Francis aliitembelea hospitali wanakoshughulikiwa watu walioambukizwa virusi vya Ukimwi, na kuongoza misa mbele ya watu 60,000 katika uwanja wa michezo wa mjini Maputo.
Katika vituo vyote hivyo viwili, Papa Francis alitilia mkazo mada nne muhimu katika ziara yake hiyo ambazo ni amani, kupambana na umaskini, rushwa na ulinzi wa mazingira. Baada ya Msumbiji, kiongozi huyo wa Kanisa Katoliki amepangiwa kuvitembelea pia visiwa vya Madagascar na Mauritius.