Afrika Kusini yachukuliwa hatua

0
1009

JOHANNESBURG, AFRIKA KUSINI

MASHAMBULIZI dhidi ya wageni ambayo yamekuwa yakifanywa mara kwa mara na raia wa Afrika Kusini safari hii yameonekana kuchukuliwa kwa uzito mkubwa na mataifa mbalimbali barani Afrika ambayo raia wake huendesha shughuli zao nchini humo.

Mbali na  viongozi na wanamuziki kutangaza kususia baadhi ya shughuli zinazofanyika nchini humo, pia hatua zilizochukuliwa na raia wa nchi kama Nigeria na Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Congo ya kushambulia kampuni kubwa za Afrika Kusini zilizowekeza katika nchi hizo, zimeonekana kupeleka ujumbe mzito.

Wakati Afrika Kusini ikitangaza kuufunga ubalozi wake wa nchini Nigeria kwa muda na kumrudisha balozi wake nyumbani baada ya raia wenye hasira kuushambulia, uamuzi wa marais kama Muhammadu Buhari wa Nigeria na Paul Kagame wa Rwanda kutangaza kutoshiriki Mkutano wa Kimataifa wa Uchumi nao umetoa taswira hiyo hiyo.

Juzi Serikali ya Tanzania ilitangaza kusitisha wa muda huduma ya usafiri wa ndege zake nchini Afrika Kusini hadi hali ya usalama nchini humo itakapotengamaa.

Mashambulizi hayo pia yameonekana kuzivuruga zaidi nchi mbili, Afrika Kusini na Nigeria.

Raia wa Nigeria ndio walihusishwa zaidi katika ghasia za ubaguzi wa wageni mara baada ya ghasia za ubaguzi zilipoanza mjini Johanesburg

Hatua hiyo inajidhihirisha zaidi  baada ya Afrika Kusini kufunga ubalozi wake nchini Nigeria , huku nalo taifa hilo likifunga vituo vyake vya biashara vilivyopo Afrika Kusini.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Afrika Kusini amekiri  ghasia hizo ni aibu kwa taifa lake.

“Serikali yetu inajutia ghasia dhidi ya maduka yote yanayomilikiwa na wageni ama Waafrika katika mataifa mengine wanaoishi nchini Afrika kusini, kilisema chombo cha habari cha SABC kikimnukuu waziri Naledi Pandor.

Nchini Zambia, kituo maarufu cha redio kimesema kuwa hakitapiga tena muziki wa Afrika kusini kupinga mapigano ya ubaguzi ambayo yanaendelea nchini humo .

“Hot FM imesitisha kupiga muziki aina yoyote ulioimbwa na msanii wa Afrika Kusini,” Kiliandika kituo hicho katika ukurasa wake wa Facebook.

“Mataifa yote ya Afrika yalisimama mstari wa mbele kuisaidia Afrika Kusini walipokuwa na shida,” redio hiyo ilisema ikinukuu Umoja wa Afrika.

Wakati wa mapigano dhidi ya ubaguzi wa rangi, makao ya chama tawala cha Afrika Kusini(ANC) yalikuwa Zambia .

“Afrika ni moja ingawa sasa wenzetu Afrika Kusini ndio wameamua kuleta ubaguzi tena,

Tunapinga uvamizi wa chuki za kibaguzi dhidi ya ndugu zetu unaoendelea katika katika nchi hiyo .”

Siku ya Jumatano , maduka kadhaa katika mji mkuu wa Zambia, Lusaka yalifungwa wakati wanafunzi walipoingia barabarani kuandamana kupinga vurugu zinazoendelea Afrika Kusini.

Hadi sasa takriban watu 423 wamekamatwa kutokana na ghasia za uporaji mjini Johannesburg.

Nchini Congo pia wiki hii yalifanyika maandamano mjini Kinshasa kupinga ghasia za uporaji dhidi ya raia wa kigeni.

Raia hao wa DRC wanasema kwamba kile kinachoendelea Afrika Kusini sio kitu kizuri kabisa ndio maana wameamua kwenda kwenye ubalozi wa nchi hiyo kuonyesha hisia zao.

“Si kweli kwamba ndugu zetu wanaoishi Afrika Kusini wanaoiba kazi zao, hiyo sio kweli kabisa. Tunawaomba waache wanachokifanya sisi wote ni ndugu.

“Sheria yao inaruhusu watu wafanye kazi kwao, hawapasi kutufanyia sisi hivyo sisi ni ndugu na tuliwasaidia sana Afrika Kusini wakati wanapambana na ubaguzi wa rangi, nchi zote za Afrika zilisaidia, kwa nini sasa iwe hivi…” alisema raia mmoja wa Congo.

Mwaka 2007 baadhi ya raia wa Kisomali walijihami dhidi ya uvamizi wowote wa Wageni mjini Pretoria katika eneo la Marastabad nchini Afrika Kusini.

Kundi hilo lilikuwa linakabiliana na kundi jingine la raia wa Afrika kusini lililoongoza ghasia dhidi ya wahamiaji.

Hatahivyo maafisa wa polisi waliingilia kati na kuwatimua kwa kutumia ndege aina ya helikopta pamoja na risasi za mipira.

Takriban watu wawili walijeruhiwa na risasi hizo za mipira wakati polisi walipokuwa wakitawanya maandamano dhidi ya wageni nchini humo.

Mpiga picha mmoja alipigwa risasi mbili za mipira mgongoni alipokuwa akirudi nyumbani kutoka shule.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here