Na GUSTAPHU HAULE
-PWANI
KIKOSI cha vijana zaidi ya 50 maarufu kama Panya road ambao kwa sasa wanajiita Kizazi jeuri wakiwa na silaha mbalimbali yakiwemo mapanga, visu, bisibisi, nondo na mikuki, juzi usiku walifunga mitaa kadhaa katika Kijiji cha Mwandege wilayani Mkuranga na kupora mali ikiwamo fedha na kisha kuwajeruhi watu kadhaa ambao ni wafanyabiashara wa maeneo hayo.
Walioshuhudia tukio hilo walisema baadhi ya wananchi walilazimika kufunga nyumba zao wakihofia maisha yao.
Walidai vijana hao wadogo wadogo walivamia maduka ya wafanyabiashara katika maeneo yajulikanayo kama Mtaa wa Kariakoo tenki la maji, zaidi ya kumwaga bidhaa za watu walipora fedha na wale waliokuwa wakikaidi walijeruhiwa kwa mapanga.
“Hawa vijana ukiwaona ni wadogo sana, lakini walikuwa wengi sana wamebeba mapanga na silaha nyingine na inavyoonekana kuna kundi la vijana wa Kariakoo hapa Mwandege ndio waliopanga tukio hili kwa vile wahusika wengi wao ni wageni wanatokea maeneo jirani ya Kongowe vicheji na Kiberewele.” Alisema Juma Salum mkazi wa Mwandege ambaye alikimbia baada ya kuwaona vijana hao wakivamia madukani.
Inaelezwa vijana hao walivamia biashara ya mama mmoja mjane ambaye alikuwa akiuza vipande vya kuku, baadhi walivitafuna na vingine walivimwaga wakimwamuru aondoke katika eneo hilo.
Juma alisema baadaye kundi hilo lilivamia bar moja iliyopo katika eneo hilo na kuvunja chupa za bia, huku nyingine wakinywa, kuharibu viti, masanduku ya vioo yaliyohifadhiwa chips na kisha kupora fedha, redio na televisheni.
Alisema vijana hao pia walimvamia baba mmoja ambaye alikuwa akipita eneo hilo akiwa kwenye pikipiki ambapo kabla ya kumchoma kisu na kumjeruhi kwa mabapa ya upanga, walimpora pochi ndogo ya mfukoni (wallet) iliyokuwa na kiasi kadhaa cha fedha.
“Walilenga kumpora pikipiki yake lakini walishindwa kuiendesha baada ya kugoma kuwaka, hawakuishia hapo walivamia duka la ‘Muha’ na kumwaga bidhaa zake na kupora fedha cha kushangaza walikimbilia moja kwa moja nyumbani kwake na kuiba kuku aliokuwa anafuga na wengine kuwaua,” alisema Juma.
Shuhuda mwingine, Kibena Hamdani, mkazi wa Mwandege naye alisema vijana hao walivunja kioo cha kabati na kisha kumrushia chupa mama mmoja mjamzito aliyekuwa akifanya biashara katika mtaa huo.
Alisema mama huyo alikumbwa na kadhia hiyo wakati akijaribu kunusuru fedha zake alizozihifadhi kwenye duka lake.
“Ilikuwa ni hatari sana, hawa watoto ni hatari, walivamia hadi msikitini na kuwavaamia waumini waliokuwa wakiswali sala ya tarawehi wakijifanya wanapiga kelele za wizi wakati wao ndio wezi,” alisema.
Halikadhalika kundi hilo lilimjeruhi fundi cherehani ambaye alishonwa nyuzi saba baada ya kuwazuia wasichukue vichwa vyake vya cherehani ambavyo walivipora kwa nguvu vikiwamo vitambaa vingi vya wateja.
Wakizungumza na MTANZANIA Jumamosi jana baadhi ya wananchi waliokumbwa na msukosuko huo kwa masharti ya kutotaja majina yao gazetini wamelalamikia vitendo hivyo wakiwatuhumu baadhi ya wazazi kwa kuwafuga watoto wao ambao wamekuwa wakishiriki katika vitendo vya uhalifu.
Wananchi hao wameliomba Jeshi la Polisi Mkuranga kufanya doria mara kwa mara katika maeneo hayo kwa vile matukio ya kupora watu yamekuwa yakijitokeza mara nyingi.
MTANZANIA Jumamosi tayari limedokezwa kuwa msako mkali unaendelea kuhakikisha vijana hao wanapatikana ili sheria ichukue mkondo wake.
Ofisa mmoja wa polisi kutoka Mkuranga ambaye si msemaji wa jeshi hilo, amesema changamoto kubwa iliyopo kwa wananchi wa eneo hilo ni kwamba wahusika wakikamatwa hawafiki mahakamani kutoa ushahidi.
Kwa upande wake Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Kibiti, Onesmo Lyanga, alipoulizwa kuhusu tukio hilo alisema hana taarifa lakini atafuatilia ili kuwabaini vijana hao