*Ni mashirika ya umma wanayolipana mishara minono
Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
SIKU moja baada ya Rais Dk. John Magufuli, kusema kwamba Serikali inafanya marekebisho ya viwango vya mishahara kwa watendaji wa mashirika ya umma, hatimaye MTANZANIA imebaini viwango mbalimbali vya mishahara wanavyolipana vigogo katika mashirika hao.
Katika mashirika hayo, baadhi ya vigogo hulipana viwango vikubwa vya mshahara, ambapo kigogo mmoja hulipwa Sh Sh milioni 36 kwa mwezi na wengine hufikia kiwango cha Sh milioni 40 kama alivyoeleza Rais Magufuli juzi.
Akizungumza na wananchi wa Chato, Dk. Magufuli alisema watu hao wanaolipwa kiwango kikubwa cha mishahara wamekuwa wakiishi kama malaika na sasa ni lazima washushwe ili waishi kama shetani.
Chanzo cha kuaminika kutoka ndani ya Serikali kiliambia MTANZANIA kuwa, ulipwaji wa viwango vikubwa kwa watendaji wa mashirika ya umma umetengeneza tabaka kubwa la wenyenacho na wasionacho.
Uamuzi huo wa Rais Magufuli, umetajwa kuwa huwenda ukaleta heshima na utu kwa Watanzania, kwani baadhi ya taasisi na mashirika ya umma watendaji wake wa ngazi za juu wameonekana kulipana mishahara ya kufuru.
“Kuna taasisi watendaji wa ngazi za juu wamekuwa wakilipwa mishahara minono zaidi ambapo kwa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), hulipana Shilingi milioni 24 kwa mwezi pamoja na marupurupu,” kilisema chanzo chetu.
Taasisi nyingine zinazolipwa kiwango kikubwa kwa watendaji wake ni Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF), Sh milioni 36, Shirika la Umeme nchini (Tanesco), Sh milioni 36.
Mashirika mengine ambayo yanaongoza kwa kulipana kiwango kikubwa ni Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), Sh milioni 36 na Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) ambapo watendaji wa juu hulipwa Sh milioni 36.
Mbali na taasisi hizo pia timu ya waatalamu ya Rais Magufuli inaangalia taasisi kama za Mpango wa Matokeo Makubwa sasa (BRN), Mamlaka ya Hifadhi za Taifa (Tanapa), Ngorongoro, Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH).
Taasisi nyingine ni Benki ya Rasilimali Tanzania (TIB), Shirika la Maendeleo la Petroli (TPDC), Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (Nida), Bodi ya Bima ya Amana, Shirika la Maendeleo la Taifa (NDC) na Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC)
Hatua ya Rais Magufuli kupitisha panga na kuweka uwiyano wa mishahara kwa watendaji wa taasisi hizo unaelezwa kuwa utaisaidia uwajibikaji na usawa kwa watendaji.
“Kwa mfano kwa sasa zipo taasisi nyingine hupandishiana mishara kila wakati, unakuta mfagiaji analipwa hadi Shilingi milioni Moja, wakati katika sekta nyingine kama walimu wanaambulia Shilingi 400,000 kabla ya makato.
“Hatuwezi kujenga Taifa la wenye nacho na wasio nacho kwa mfumu huu na ikiwa Serikali italitekeleza hili kama Rais Magufuli alivyoamua ni wazi sasa tutapiga hatua mbele zaidi,” alisema mtoa habari huyo.
Azivaa bodi
Kiongozi huyo wa nchi, alishangazwa na baadhi ya bodi za wakurugenzi kushindwa kufanyakazi zao kwa mujibu wa sheria na badala yake wamekuwa na kazi ya kupandisha mishahara kwa viongozi.
Alisema kutokana na hali hiyo anashangazwa na bodi hizo kila kukicha zimekuwa zikifanya kazi ya kupandisha mishahara pamoja na kufanya vikao nje ya nchi.
Kutokana na hali hiyo, Rais Magufuli ameunda timu ya wataalamu ambayo imeanza kufanya kazi ya upunguzaji wa mishahara mikubwa kwa watendaji wakuu wa mashirika ya umma.
“Tena hawa wakurugenzi ndio wanaongoza kwa kulipwa fedha nyingi na hata kwenda kufanya vikao ulaya, ninasema hapa kwamba suala hili litaanza kushughulikiwa katika bajeti ya hivi karibuni,” alisema Rais Magufuli.
Juzi akiwa wilayani Chato, Rais Magufuli, alisema wapo watendaji wanalipwa Sh milioni 40 kwa mwezi na wengine wanalipwa Sh 300,000.
Alisema tayari ameunda timu ya wataalamu ambayo inafanya kazi ya kupunguza mishahara hiyo na kufikia Sh milioni 15 kwa mwezi ili asipatikane Mtanzania anayelipwa zaidi ya kiwango hicho.
“Tunafanya hivi ili nyingine tuziteremshe kwa watu wa chini na yule atakayeng’ang’ania kwamba lazima alipwe Sh milioni 40 aache kazi tuweke mtu mwingine,” alisema Rais Magufuli.
Hata hivyo Rais Magufuli, alishangazwa na watu namna wanavyolipana kile alichokiita mishahara ya ajabu kwa kushirikiana na bodi ambazo wakati mwingine huzihonga fedha ili zipandishe mishahara yao.
“Kuna watu wanaishi kuliko hata malaika lazima tuwashushe waishi kama shetani,” alisema Rais Magufuli.
Pamoja na hali hiyo kiongozi huyo wa nchi alianika madudu aliyoyakuta ndani ya Serikali ikiwemo mmoja wa mfanyakazi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), kulipwa mishahara ya watu 17 na kuagiza mfanyakazi huyo afikishwe mahakamani.
Pamoja na hali hiyo alisema wapo watumishi wanaolipwa mishahara mikubwa ambayo inafikia hadi Sh milioni 40 kwa mwezi, ambayo sasa itapunguzwa na kuweka kima cha juu cha mshahara usiozidi Sh milioni 15.
Dk. Magufuli alisema Serikali yake imejiandaa kuboresha maslahi ya wafanyakazi kwa kupunguza kodi kutoka asilimia 11 ya sasa hadi asilimia 10 au 9 (single digit) kuanzia bajeti ijayo.
“Kuhusu tatizo la wafanyakazi hewa, uhakiki mdogo uliofanywa hivi karibuni, umebaini wafanyakazi hewa 1,680 waliokuwa wakilipwa shilingi bilioni 1 na milioni 800 na kwamba ni matarajio kuwa uhakiki unaofanywa nchi nzima utaisaidia Serikali kubaini wafanyakazi hewa wengi zaidi na kunusuru fedha nyingi zaidi za Watanzania.
Alisema anashangazwa na hatua ya baadhi ya watu kuishi kama malaika huku wengine wakiishi kama masheteni, jambo ambalo alisema halina nafasi katika Serikali yake.
“Nyiye mliokuwa mnaishi kama malaika, sasa zamu yenu kuishi kama mashetani,” alisema Dk. Magufuli huku akishangiliwa na umati wa wananchi waliohudhuria katika mkutano huo.