22.8 C
Dar es Salaam
Thursday, April 18, 2024

Contact us: [email protected]

Magufuli aeleza meli 65 zilivyokwepa kodi

pombeNa Mwandishi Wetu, Chato

RAIS Dk. John Magufuli, amefichua zaidi madudu ndani ya Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA),  huku akieleza namna meli 65 zilivyoingia na kushusha mizigo bila kulipa ushuru wa Serikali.

Amesema meli hizo zilishusha mizigo katika Bandari ya Dar es Salaam na baada ya kupakua mzigo hiyo ziliondoka na kutokomea bila kujulikana zimekwenda wapi.

Kutokana na hali hiyo amesema sasa analazimika kuchukua hatua za kurejesha nidhamu kwa watumishi wa Serikali.

Kauli hiyo aliitoa juzi wilayani Chato, alipokuwa akihutubia katika mkutano wa hadhara, ambapo alisema ni jambo la aibu kwa nchi kuendelea kukosa mapato kwa uzembe wa watu wachache.

“Ndugu zangu tusipochukua hatua nchi itatushinda leo (juzi) pale Bandari zimeingia zaidi ya meli 65 zimeshusha mizigo na hazikuonekana. Hivi inawezekana vipi meli ishushe mizigo na kutokomea bila kulipa mapato ya Serikali.

“Meli zilileta mizigo zikashusha na zikapotea hivyo hivyo na Serikali ikakosa hela. Jamani ndani ya Serikali kuna madudu ya kila aina hivyo ninawaomba mniombee nimejitoa sadaka kwa ajili ya Watanzania,” alisema Rais Magufuli huku akishangiliwa.

Majipu bandarini

Waziri Mkuu, Kasim Majaliwa ameshafanya ziara katika Bandari za Dar es Salaam, Tanga na Mtwara ambako amebaini mambo mengi hayaendi vizuri hali ambayo amekuwa akilazimika kuchukua hatua mbalimbali ikiwemo kuwajibisha watendaji.

Chini ya mkakati wa Serikali ya awamu ya tano ya kutumbua majipu, Rais Dk. Magufuli alivunja bodi ya Bandari siku chache baada ya kupatikana kwa kontena ambazo hazikulipiwa ushuru.

Kampuni 43 ziligunduliwa kuhusika katika makontena hayo. Mwenyekiti wa Bodi, Profesa Joseph Msambichaka sanjari na Mkurugenzi Mkuu wa Bandari, Awadhi Massawe walivuliwa nyadhifa zao .

Pia Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchukuzi, Dk. Shaban Mwinjaka aliondolewa katika wadhifa huo. Waziri Mkuu, Majaliwa alipofanya ziara ya kushtukiza katika Bandari ya Dar es Salaam, aligundua kontena 329 zilipitishwa bila kulipiwa kodi kinyume cha utaratibu wa bandarini.

Waziri Mkuu, hivi karibuni alifanya ziara ya kushtukiza katika Bandari ya Tanga ambako pamoja na masuala mengine, alikuta tishari tatu zikiwa chakavu bila ya injini wakati serikali ilitoa fedha za ununuzi wa matishari ya kisasa.

Baada ya kubaini jipu hilo, alimwagiza Meneja wa Bandari ya Tanga, Henry Arika, kutoa maelezo kwa maandishi nani alihusika na ununuzi wa matishari hayo badala ya zile mbili zilizopaswa kuwapo ambazo Serikali ilitoa Dola za Marekani milioni 10.

Arika alijitetea kwamba tishari hizo ziliwasili nchini miaka minne iliyopita lakini zilianza kufanya kazi rasmi mwaka jana na kwamba yeye hana muda mrefu katika bandari hiyo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles