Na CLARA MATIMO – MWANZA
JAMII imetakiwa kujenga utaratibu wa kuwatembelea wafungwa na kuwapa mahitaji mbalimbali pamoja na kuwaombea ili waboreshe hali ya maisha yao wawapo gerezani.
Wito huo umetolewa jijini Mwanza na muhudumu wa kiroho katika Gereza la Butimba, Padri Bernadini Mtuli, alipozungumza katika magereza hayo baada ya wadau mbalimbali kutoa msaada wa vyakula kwa wafungwa wa gereza hilo ili nao waweze kusherehekea sikukuu ya mwaka mpya.
Padri Mtuli alisema baadhi ya watu huwaona wafungwa kama si binadamu wanaostahili kuishi katika jamii jambo ambalo si sahihi kwani na wao wanastahili kuheshimiwa na kupewa huduma zote.
“Tusiwaone wafungwa kama ni watu ambao ni wa ajabu na hawatakiwi katika jamii, hawa ni ndugu zetu, wengine ni ndugu wa damu pia wote tumeumbwa na Mungu mmoja hivyo tuendelee kuwathamini na kuwatembelea na tuthamini utu wao kwamba wako hapa kwa kipindi kifupi ama kirefu kwa ajili ya kujirekebisha.
“Mara nyingi tumeona kwamba wanapomaliza vifungo vyao na kurudi katika jamii kweli wanakuwa wamejirekebisha na wanaendelea kushirikiana vyema na wanajamii wenzao kwa hiyo tuendelee kuwasaidia hasa pale wanapohitaji msaada wetu,”alisema Padri Mtuli.
Mkuu wa Gereza la Butimba, Idd Mbaga, alisema wafungwa wana haki zao za kisheria ikiwemo haki ya kupata matibabu na chakula ndiyo maana jeshi la magereza limetoa vibali maalum kwa madhehebu mbalimbali ya dini ili yaweze kurudisha nyoyo zao ambazo zimepondeka na kuwasaidia kwa maombi na mahubiri warudi katika mstari.
Alisema lengo ni kuwafanya wanapomaliza vifungo vyao waweze kujumuika na jamii kuleta maendeleo katika familia zao na taifa kwa ujumla.
Mwenyekiti wa mashirika yasiyo ya kiserikali mkoani Mwanza, Gozbert Mutta, alisema wameweza kuwapelekea wafungwa hao vyakula mbalimbali kwa ajili ya sikukuu ya mwaka mpya.
Diwani wa Kata ya Butimba, John Pambalu, alisema ipo haja kwa jamii kuwatembelea wafungwa na kuwajulia hali maana wao ni sehemu ya jamii na wanahaki ya kutembelewa.