NEW YORK, MAREKANI
BINGWA wa ngumi, Manny Pacquiao, ameweka wazi kwamba wamefikia makubaliano na mpinzani wake, Amir Khan, kwa ajili ya pambano lao linalotarajiwa kufanyika Aprili 23, mwaka huu.
Mazungumzo ya pambano hilo yaliendelea wiki iliyopita hasa kutafuta sehemu sahihi ya kufanyika kwa pambano hilo, awali walidai kuwa linaweza kufanyika mjini wa Bolton au Manchester nchini Uingereza.
Lakini hadi sasa, bado sehemu sahihi ya pambano halijawekwa wazi ila wapiganaji wenyewe wamethibitsha kufikia makubaliano ya kupigana baada ya mazungumzo yaliyomalizika juzi nchini Marekani.
Kupitia ukurasa wa Twitter wa Pacquiao, bondioa huyo aliweka wazi kuwa, wamefikia makubaliano sahihi na mpinzani wake, Khan, kufanyika kwa pambano mwishoni mwa Aprili.
“Tayari tumefikia pazuri katika makubaliano ya pambano dhidi ya Khan, uongozi wangu na ule wa Khan umeweka wazi, lakini sehemu husika ya kufanyia pambano hilo hadi sasa bado haijawekwa wazi, ila nadhani muda mfupi ujao patajulikana.
“Najua pambano litakuwa gumu kwa kuwa mpinzani wangu ana uwezo mkubwa, hivyo nafanya maandalizi kuelekea pambano hilo,” aliandika Pacquiao.
Hata hivyo, kwa upande wa Khan alithibitisha kukubali pambano hilo mara baada ya timu yake kupitia mikataba na kujiridhisha.
“Timu yangu baada ya kupitia mikataba ya pambano langu dhidi ya Pacquiao, nimeona niweke wazi kuwa, mipango ya pambano hilo imekamilika na litafanyika Aprili 23, lakini taarifa zaidi ya sehemu ya kufanyia bado haijajulikana ila itajulikana,” aliandika Khan.
Hata hivyo, Pacquiao aliwahi kusema anastaafu mchezo huo na kujikita katika mambo ya siasa ili aweze kuwasaidia watu wake wa nchini Ufilipino. Hatua hiyo ilifikia baada ya kufanyiwa upasuaji wa beki.