BERLIN, UJERUMANI
KIUNGO mshambuliaji wa klabu ya Arsenal, Mesut Ozil, amewakosoa nyota wa zamani wa timu hiyo ambao wamekuwa wakiisema vibaya mara kwa mara na hawatoi sapoti.
Nyota huyo mwishoni mwa wiki iliyopita alikuwa na timu yake ya Taifa ya Ujerumani katika michuano ya kuwania kufuzu Kombe la dunia, huku wakishinda mabao 2-1 dhidi ya Jamhuri ya Czech.
Ozil alitumia ukurasa wake wa Instagram kuwashambulia nyota hao wanaoisema vibaya Arsenal wakati wakipewa nafasi ya kufanya uchambuzi na kuizungumzia.
Baadhi ya nyota wa zamani ambao wamekuwa wakiishambulia klabu hiyo ni pamoja na Ian Wright na Martin Keown, huku wakidai kwamba kila msimu klabu hiyo inazidi kuwa mbaya.
“Ni furaha kuona Septemba hii nikiwa kwenye kikosi cha timu ya Taifa ya Ujerumani kuelekea michezo ya kufuzu Kombe la Dunia, tayari tumeweza kushinda mabao 2-1 dhidi ya Jamhuri ya Czech.
“Kwa siku chache zilizopita baadhi ya wachezaji wenzangu wa timu ya Taifa waliniuliza juu ya mambo yanayoendelea ndani ya klabu ya Arsenal, walikuwa wanazungumzia hasa majanga yanayosemwa kwenye vyombo vya habari na wachezaji wa zamani wa timu hiyo.
“Nimeamua kutumia ukurasa wangu wa Instagram kuungana na wewe ambao upo karibu na mimi, naomba niseme kwamba lazima tuwe na furaha hata kama tumeanza msimu kwa kuyumba kidogo, lakini lazima tuanze kuwa na furaha.
“Miaka minne iliyopita nilikamilisha uhamisho wangu katika dakika chache za mwisho kutoka Real Madrid, kocha Arsene Wenger alinishawishi vizuri nikaweza kukubali, alinieleza historia kubwa ya timu pamoja na baadhi ya wachezaji wake nyota aliowafundisha kama vile Bergkamp, Vieira na Pires. Kocha huyo aliniambia jinsi atakavyonifanya kuja kuwa mchezaji mkubwa, hicho ndicho kitu ambacho wachezaji wanapenda kuja kukisikia katika maisha yao.
“Kwa upande wangu nipo tayari kukosolewa kutokana na kile ninachokifanya, nimekuwa nikisikia kwamba nina matumizi mabaya, sina mwili wa ushawishi, siwezi kupambana nikiwa uwanjani, hayo ni baadhi ya maneno ambayo yanazungumzwa juu yangu.
“Baadhi ya maneno hayo yanasemwa na wale ambao hawanijui, wengine ni wale wachezaji wa zamani waliofanikiwa kwenye soka hata wale wasiofanikiwa ndani ya klabu hii, ni vizuri mastaa hao wakaamua kuacha kuzungumza mambo ambayo si ya msingi na wakaipigania timu iweze kufanya vizuri,” alisema Ozil.
Mchezaji huyo alihusishwa kutaka kuondoka ndani ya kikosi hicho katika kipindi hiki cha majira ya joto, huku akiwindwa na klabu mbalimbali pamoja na Barcelona, lakini hadi usajili unafungwa wiki iliyopita amesalia kwenye kikosi hicho.