Na THERESIA GASPER-DAR ES SALAAM
KOCHA mkuu wa timu ya Simba, Joseph Omog, amesema sasa anaweza kuufikiria mchezo ujao wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya watani wao wa jadi Yanga, baada ya kikosi chake kupata ushindi wa kishindo mbele ya Majimaji FC.
Simba juzi ilipata ushindi mnono wa mabao 4-0 dhidi ya Majimaji katika mchezo uliopigwa Uwanja wa Taifa Dar es Salaam, ambapo kocha huyo raia ya Cameroon, ametangaza kuanza kuifungia kazi Yanga.
Akizungumza na MTANZANIA jana, Omog alisema baada ya kutoa kipigo kikali, sasa wanaanza kujipanga kwa pambano la kukata na shoka la Jumamosi, huku akidai kikosi hicho tayari kimetua mkoani Morogoro.
Alikiri kuwa mchezo huo utakuwa mgumu kwa pande zote kutokana na kila timu kuhitaji ushindi wa pointi tatu muhimu.
Naye kocha msaidizi wa timu hiyo, Mganda Jackson Mayanja, alisema matokeo ya ushindi mnono waliyoyapata dhidi ya Majimaji, yataongeza hamasa kwa wachezaji na mashabiki wa timu hiyo kuelekea pambano hilo.
“Tumefurahi kwa matokeo haya yanayotufanya tuendelee kufanya vizuri ligi kuu, lakini kazi kubwa iliyobaki ni kuutazama mchezo mwingine unaotukabili mbele yetu dhidi ya Yanga ambao utakuwa wa ushindani wa hali ya juu.
“Hakika huu ni ushindi wa faraja kwetu, kwani wachezaji wangekuwa kwenye wakati mgumu sana kama tungekosa ushindi kisha tukaanza maandalizi ya kupambana na mahasimu wetu,” alisema Mayanja.
Wekundu hao wa Msimbazi wanatarajia kukutana na mahasimu wao Yanga kwa mara ya kwanza tangu kuanza kwa msimu huu wa ligi, huku wakiwa wamepania kulipiza kisasi cha kufungwa na ‘Wanajangwani’ hao msimu uliopita.
Matokeo ya mchezo wa juzi yaliiwezesha Simba kuendelea kushika usukani wa Ligi Kuu Tanzania Bara baada ya kufikisha pointi 16.
Wakati huo huo, kocha msaidizi wa timu ya Majimaji, Petter Mhina, alisema kipigo cha Simba kitakuwa cha mwisho kwa kikosi chake kwani hawataruhusu nyavu zao kutikiswa tena kutokana na wachezaji kupata mahitaji muhimu waliyokuwa wameyakosa.
“Awali timu ilikuwa inakabiliwa na ukata, hali iliyochangia kushindwa kufanya vyema katika michezo yote iliyopita, lakini sasa hatutakubali kufungwa tena,” alisema Mhina.