24.5 C
Dar es Salaam
Wednesday, November 30, 2022

Contact us: [email protected]

Warembo hawa, wanastahili saluti

jack-and-matata

Na CHRISTOPHER MSEKENA,

UKWELI unaendelea kubaki palepale kuwa mwanamke amekuwa akichukua nafasi kubwa kwenye maisha ya jamii nyingi hapa nchini na nchi nyingine za Afrika.

Hizi si zama za mwanamume kumtumikisha mwanamke, bali ni wakati wa mwanamke na mwanamume kushirikiana ili kuchochea maendeleo ya familia na nchi kwa jumla.

Wapo mastaa ambao baada ya kujulikana na kutamba wanajisahau kabisa na kukaa mbali na jamii ambayo kimsingi wanapaswa kuitumikia.

Hapa kwenye Juma3tata tunakuletea orodha ya warembo wenye mchango mkubwa kwenye jamii kwa kutumia ukubwa wa majina yao katika kusaidia jamii zenye mahitaji.

Wapo wengi, lakini listi hii inawahusisha wale waliong’ara zaidi, kwa upande wa warembo pekee, tukiweka pembeni sanaa nyingine.

HAPPINESS MILLEN MAGESA

Alivaa taji la Miss Tanzania mwaka 2001, shavu lililomfanya apate dili kwenye Kampuni ya Ice Model ya Afrika Kusini. Alifanya kazi ya mitindo kwa miaka nane kabla ya Kampuni ya Ford Models ya New York, Marekani kumsainisha mkataba ambako mpaka sasa anapiga michongo yake huko.

Amefanya mengi kwa jamii, lakini alama ya ukaribu wake na jamii ameiweka kwenye kampeni kwa wasichana wa Afrika juu ya ugojwa wa maumivu wakati wa hedhi (Endometriosis) kitu kilichomfanya mwaka jana kupata tuzo ya heshima ya Global Good iliyotolewa na waandaaji wa BET.

Mbali na hilo, amejenga shule mkoani Mtwara ambayo ni maalumu kwa ajili ya watoto wenye mahitaji. Anastahili pongezi kwa hakika.

TAUSI LIKOKOLA

Huyu aliibuka baada ya kutwaa Taji la Miss Universe mwaka 2007. Ni mrembo aliyefanikiwa kupitia tasnia ya mitindo anayeishi nchini Marekani akifanya kazi mbalimbali za mitindo.

Tausi hajaisahau jamii ya Kitanzania, mara kadhaa huwa anarudi  nchini na kutoa misaada kwenye vituo vya watoto yatima na kusaidia waathirika wa ugonjwa wa Ukimwi. Ni mwandishi wa vitabu ambavyo vinatoa mchango mkubwa kwa jamii yake.

FLAVIANA MATATA

Flaviana Matata, naye anatokea Miss Universe lakini huyu alikwenda mbali zaidi baada ya kufanikiwa kutinga fainali ya ‘World Miss Universe 2007’ na kufanikiwa kuibuka nafasi ya sita mpaka mwisho wa mashindano yaliyofanyika huko Mexico City, Mexico.

Ni miongoni mwa warembo ambao kwa kiasi kikubwa wamechangia jamii ifahamu umuhimu wa kusaidia watoto yatima na wanaoishi kwenye mazingira magumu.

Mbali na michango mingine mingi anayotoa mlimbwende huyu, Flaviana anamiliki Taasisi ya Flaviana Matata Foundation ambayo imekuwa ikisaidia kutoa elimu kwa watoto wa kike.

HOYCE TEMU

Huyu ni Miss Tanzania mwaka 1999. Baada ya kutwaa taji hilo,  alipata nafasi ya kuwa Afisa Uhusiano wa Umoja wa Mataifa na hapo ndipo wigo wa kuendelea kuwasaidia Watanzania wenye mahitaji kama vile wazee, watoto, walemavu, wagonjwa na wengine ulipoongezeka.

Kupitia Kipindi cha Mimi na Tanzania, kinachorushwa na Channel Ten, mlimbwende huyu amefanikiwa kuwakutanisha watu wenye mahitaji mbalimbali na jamii ambayo imechanga fedha za matibabu na kadhia nyingine.

Wapo mashuhuda kadhaa ambao wameteseka kwa maradhi mbalimbali kwa muda mrefu na kukata tamaa, lakini walipokutana na Hoyce, walifanyiwa upasuaji nchini India na sasa maisha yao yanaendelea kuwa yenye matumaini.

JACQUELINE NTUYABALIWE

Safari ya umaarufu wake, ilianza mwaka 2000 baada ya kushinda Taji la Miss Tanzania na baadaye kuipeperusha bendera ya Tanzania Miss World, mwaka huo.

Mwaka 2004 alizidi kujizolea umaarufu zaidi baada ya kuingia kwenye muziki wa Bongo Fleva, ambapo akaibuka na jina jipya la ‘K-Lyn’. Alipata kiki ya ajabu alipotoa wimbo wa ‘Nalia kwa Furaha’ aliomshirikisha Bushoke na baadaye kuachia nyingine kama ‘Crazy Over You’.

Mara kadhaa amekuwa mstari wa mbele kusaidia jamii ya watu walemavu akishirikiana na mume wake, Dkt. Reginald Mengi. Ni miongoni mwa warembo walio mstari wa mbele kutetea haki za wanyama kama vile faru na tembo.

NANCY SUMARI

Licha ya kuwa na umri wa miaka 29 tu, ameweza kufanya mambo kadhaa muhimu kwenye jamii yake na alipata jukwaa pana la kuyafanya hayo mara baada ya kutwaa taji la Miss Tanzania mwaka 2005 na Miss World Africa mwaka huo.

Nancy amejikita kwenye tasnia ya habari, ni Mkurugenzi Mtendaji wa Tovuti ya Bongo5. Mrembo huyu anasema, mwaka huu amedhamiria kutoa elimu kwa wazazi kuhusu namna ya kuwatengeneza watoto wakue wakiwa na uelewa mpana na kujitambua.

Mwezi Juni, mwaka huu, Nancy alifunga ndoa na mpenzi wake wa siku nyingi Luca Neghesti na hafla kufanyikia jijini Arusha.

HAPPINESS WATIMANYWA

Orodha hii inakamilishwa na mshindi wa Shindano la Miss Tanzania mwaka 2013/14, Happiness Watimanywa ambaye ameipeperusha vyema bendera ya nchi yetu kwenye mashindano ya urembo ya dunia mwishoni mwa mwaka jana.

Happiness aliingia Kumi Bora ya warembo kwenye shindano la ‘Miss World People’s Choice’, sababu ikiwa ni mchango wake katika kutoa elimu kwa wanawake wanaoishi vijijini juu ya ugonjwa wa Fistula.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
205,436FollowersFollow
558,000SubscribersSubscribe

Latest Articles