ELIUD NGONDO, MBEYA
WATU wasiojulikana wamevunja Ofisi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Wilaya ya Mbeya Mjini na kuteketeza kwa moto baadhi ya nyaraka muhimu zikiwemo fomu za wagombea ubunge wa viti maalumu.
Tukio hilo linatokea ikiwa ni siku chache tangu Ofisi za Chadema Kanda ya Kasikazini kuchomwa moto jijini Arusha wiki iliyopita.
Akizungumza na wandishi wa habari jana Mwenyekiti wa Chadema Wilaya ya Mbeya Mjini, John Mwambigia, alisema alipigiwa simu na katibu wa chama hicho wilaya alfajiri kuhusu kutokea kwa tukio hilo.
Alisema walipofika eneo hilo walikuta baadhi ya nyaraka na samani za ofisi hiyo zikiwa zimeteketea na hivyo akaliomba Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na vyombo vingine vya dola kufanya uchunguzi ili kubaini waliohusika na uhuni huo.
Alizitaja nyaraka zilizoteketea kuwa ni pamoja na vitabu vya kanuni za uchaguzi zilizokabidhiwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kwa ajili ya wagombea wa nafasi ya ubunge na madiwani.
Mwambigija alisema lengo la waliotekeleza tukio hilo ni kuteketeza fomu za wagombea udiwani na za mgombea ubunge wa jimbo hilo lakini kutokana na moto huo kuwahi kudhibitiwa fomu hizo zilipona.
“Nawaomba wanachama wenzangu wa Chadema, tusilipe kisasi kwa mtu yeyote hata kama tunawafahamu waliohusika, pengine walitaka tusiwe na wagombea udiwani na ubunge wa jimbo hili lakini wameshindwa,” alisema Mwambigija.
Alisema chama hicho kitashinda kwenye uchaguzi Mkuu wa Mwezi Oktoba mwaka huu katika jimbo hilo pamoja na Kata zote 36 za Jiji la Mbeya.
Hata hivyo alisema ofisi hiyo ni nyumba ya mtu na siyo ya Chadema na kwamba upande mwingine wa ofisi kuna watu wanaoishi na hivyo waliochoma walikusudia kuua pia watu.
Naye mtoto wa mmiliki wa nyumba hiyo, Anna Mwansasu, alisema ofisi hiyo imechomwa moto usiku wakati amelala.
Alisema kuna moshi unaingia ndani na alipofuatilia kujua ulikokuwa unatoka ndipo akabaini unatoka ndani ya ofisi ya Chadema.
Alisema alipoona moto ndani ya ofisi hiyo aliwapigia simu baadhi ya viongozi wa Chadema ambao walifika eneo la tukio na kushirikiana na majirani kuuzima moto huo kwa kutumia maji na kisha wakaanza kutoa nje baadhi ya vitu vilivyokuwa vimenusurika.
“Baadhi ya vijana waliokuwa wanaendesha bajaji walikuja tukashirikiana nao kuuzima moto na wakanishauri nizime umeme ili moto usishike nyumba nzima, nilifanya hivyo na sisi huko ndani hatujadhurika,” alisema Anna.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mbeya, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi, Ulrich Matei, alikiri kutokea kwa tukio hilo na kwamba jeshi hilo linaendelea na ufuatiliaji ili kuwabaini waliohusika kuchoma ofisi hiyo.
Hata hivyo alisema walibaini kuwa ofisi hiyo ilikuwa haina mlinzi na ndiyo maana wahusika walifanikiwa kutekeleza tukio hilo kwa kuanza kuvunja mlango.
Vile vile alisema uchunguzi wa awali ulibaini kuwa kulikuwa na hali ya kutoridhika kwa baadhi wa wanachama wa chama hicho juu ya uteuzi wa wagombea wa nafasi ya udiwani katika Jimbo hilo.