Ripoti ya ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kuratibu misaada ya dharura, OCHA, inasema mapigano ya kutumia silaha nzito na mashambulizi kutoka angani vimeendelea katika maeneo kadhaa ya mji mkuu wa Libya, Tripoli na viungani.
Ripoti inasema katika viunga vya Tripoli, katika maeneo ya Abusliem, Souq Jumaa na Hadbaa, makombora yamesababisha vifo vya watu sita wakiwemo wanawake wanne na kuwajeruhi watu wengine 20.
OCHA inasema tangu kuanza kwa vurugu, inakadiriwa kuwa watu 80 wamejeruhiwa na wengine 20 wamepoteza maisha lakini wale ambao wamethibitishwa ni wananchi 54 kujeruhiwa na wengine 14 kupoteza maisha.
Ripoti ya sasa imeonesha ongezeko la wanaokosa makazi kwa siku, ambapo zaidi ya watu 4,500 ni watu wapya waliopoteza makazi kiasi kinachoongeza idadi ya wakimbizi wa ndani kufikia 25,000.
Wananchi wengi waliokwama katika maeneo yenye mgogoro wamejikuta katika sintofahamu ya kutokujua ikiwa wabaki katika majumba yao au waondoke kwa sababu ya hali mbaya iliyoko huko nje ya mapigano na mabomu. Hali hiyo ya sintofahamu inazidi kuongezeka kwani chakula na mahitaji mengine muhimu vinazidi kupungua.
Mgogoro wa sasa umeongeza hatari zaidi kwa watu baada ya mgogoro wa miaka mingi, mgogoro wa kiuchumi na kijamii na upungufu katika huduma za kijamii ambazo tayari zimewaweka takribani watu 820,000 waakiwemo watoto 250,000 katika uhitaji mkubwa wa misaada ya kibinadamu.