FARAJA MASINDE-DAR ES SALAAM
Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) limesema kuwa kufikia mwaka 2020 nyumba zaidi ya 1,500 zitakuwa zimeunganishwa katika matumizi ya gesi asilia katika mikoa ya Dar es Salaam na Mtwara kutoka nyumba 458 za sasa.
Kauli hiyo ilitolewa mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika hilo, Dk. James Mataragio, wakati akiainisha mafanikio ya miaka minne ya shirika hilo ambapo alisema kuwa matumizi ya gesi asilia yameongezeka.
“Uzalishaji wa umeme kwa gesi asilia umeongezeka kutoka MW 553 mwaka 2015 hadi kufikia MW 892.7 mwaka 2019 ongezeko la asilimia 61, na sasa asilimia 57 ya umeme katika gridi ya Taifa unazalishwa kwa kutumia gesi asilia, tumeondoa tatizo la upungufu wa umeme wakati wa kipindi cha kiangazi.
“Pia usambazaji wa gesi asilia viwandani umeongezeka kwani jumla ya viwanda 48 vimeunganishwa kwenye mtandao wa gesi asilia katika Mikoa ya Dar es Salaam, Pwani na Mtwara kwani hadi sasa viwanda vitano kati ya hivi vimeunganishwa katika bomba kuu la TPDC.
“Tuko katika utekelezaji wa kuunganisha nyumba zaidi ya 1,500 kwa mikoa ya Dar es Salaam na Mtwara kupitia bajeti ya 2019/20 ikilinganishwa na nyumba 453 mwaka 2015,” alisema Dk. Mataragio.
Aidha, alisema kuwa kumekuwa na ongezeko la matumizi ya gesi asilia kwenye magari katika kipindi cha miaka minne ambapo hadi sasa kuna magari 305 yanayotumia huduma hiyojijini Dar es Salaam idadi ambayo amesema kuwa inatarajia kuongezeka zaidi.
“Ili kuchochea matumizi ya gesi asilia kwenye magari, kwa sasa TPDC inatekeleza ujenzi wa vituo vikubwa viwili vya CNG Dar es Salaam ambavyo vitawezesha usambazaji wa gesi asilia katika mfuko wa CNG kwa ajili ya magari na kuwa na vituo vya kujazia gesi asilia ambapo serikali imetenga Sh bilioni 14.2 kutekeleza mradi huo.
“Pia uzalishaji wa gesi asilia umeongezeka kutoka futi za ujazo milioni 37.18 kwa mwaka hadi kifikia milioni 57.84 kwa mwaka sawa na asilimia 36, huku tukifanikiwa kijenga mmtanfao wa kusabaza gesi asilia wenye jumla ya kilometa 38.25 ongezeko ambalo linatokana na kuongezeka kwa matumizi ya gesi kuzalishia umeme kinyerezi I na II jambo ambalo limefanikiwa kutokana na kuwapo kwa miundombinu mikubwa ya kuchakata nabkusafirisha gesi asilia, pia TPDC inamiliki kwa asilimia 100,” alisema.
Kuhusua mchango wa Shirka hilo kwa taifa katika kipindi cha miaka minne alisema kuwa imefanikiwa kuchangia Sh bilioni 243.05 huku matarajio yakiwa ni kufikia Sh bilioni 599.62 ifikapo mwaka wafedha 2023/24.
“Kwa kutumia gesi asilia tangu mwaka 2004 tumesaidia kuokoa Sh Trilioni 30.225 ambazo Sh Trilioni 27.6 zingetumika kuagiza mafuta kwa ajili ya kuzalisha umeme, hivyo katika kipindi cha mika minne tumeokoa Sh Trilioni 12.7.
“Pia ndani ya kipindi cha miaka minne tumefanikiwa kuanzisha kampuni Tanzi mbili amabzo ni GASCO inayojishughulisha na na usimamizi na uendeshaji wa miundombinu ya gesi asilia na TANOIL ambayo inajishughulisha na miradi ya mafuta kwa maana ya uagizajiwa mafuta nchini,” alisema Dk. Mataragio.
Katika hatua nyingine, alisema kuwa TPDC iko kwenye maandalizi ya kuchimba visima viwili (utafiti na uhakiki) ambavyo vitatumia Sh bilioni 202.6.
“Mategemeo yetu katika utafiti huu ni kugundua gesi asilia kiasi cha futi za ujazo trilioni 1.032 (TCF). Kisima hiki kitakuwa cha baharini na ni cha kwanza kwa TPDC,” alisema.