29.7 C
Dar es Salaam
Wednesday, August 17, 2022

Boris alivyoibuka na ushindi wa kihistoria

LONDON, UINGEREZA

TAYARI mshindi wa Uchaguzi Mkuu wa Uingereza, uliofanyika Desemba 12 amepatikana, ambapo kwa mara nyingine Boris Johnson anaendela kusalia madarakani akiwa Waziri Mkuu.

Katika matokeo yaliyotangazwa Ijumaa mchana, Johnson amekiongoza Chama chake cha Conservatives kunyakua ushindi wa kishindo dhidi ya mpinzani wake, Jeremy Corbyn wa chama cha Labour.

Katika uchaguzi huo, chama cha Johnson kimeshinda zaidi ya viti 326.

 Jonhson anasema hatua hiyo inaipatia serikali mpya fursa ya kuheshimu uamuzi wa kidemokrasia ya raia wa Uingereza ili kuliimarisha taifa hilo.

Awali, Chama cha Johsnon kilihitaji kushinda viti 326 ili kutangazwa kuwa mshindi lakini kilivuka idadi hiyo na kufikia 364.

Saa chache baada ya ushindi huo wa kishindo, Umoja wa Ulaya umetoa pongezi zao na kuhimiza mchakato wa kujitoa katika Umoja huo uidhinishwe haraka. Johnson amejipambanua mbele ya wanahabari kuwa zawadi pekee ya kuwapa wapiga kura wake ni kuwalipa imani yao na kusisitiza kwamba hadi kufikia Januri 31, 2020 nchi hiyo itakuwa tayari imejitoa kwenye umoja wa Ulaya ambao umekuwa mfupa uliowashinda wengi kwa kipindi kirefu.

“Serikali ya kihafidhina ya nchi hii imepatiwa madaraka makubwa zaidi ya kukamilisha mchakato wa Brexit, neno pekee ambalo naweza kusema ni kuwa sina cha kuwapa wapigakura wangu zaidi ya kuwalipa imani yao kwangu, lakini napenda nilithibitishe hili kuwa kazi iliyopo sasa sio tu kukamilisha mchakato wa Brexit bali pia kuiunganisha nchi yetu na kutanguliza mbele mahitaji muhimu ya Waingereza.

 “Mmetupatia kura zenu bila kujali kuwa nyie si wahafidhina,” Yalikuwa ni maneno ya Waziri Mkuu Johnson saa chache baada ya kujihakikishia ushindi mapema Ijumaa.

Katika uchaguzi huo, wapiga kura wengi ambao siyo wa chama cha Johnson walikiunga mkono chama hicho.

Wakati furaha hiyo ikiendelea kwa Johnson, upande wa pili wa mpianzani wake ambaye ni mwenyekiti wa chama cha Labour Corbyn ameweka wazi kuwa hatogombea tena wadhfa huo kutokana na pigo hilo la uchaguzi wa Desemba 12.

Boris Johnson

Uamuzi huo wa kiongozi wa Labour unajiri huku chama hicho kikikabiliwa na matokeo mabaya zaidi ya uchaguzi katika miongo kadhaa iliyopita.

Akingumza mjini London, Waziri Mkuu Johnson, anasema ni jukumu lake kuindoa Uingereza katika muungano wa EU. “Raia wanataka mabadiliko, hatuwezi kuwavunja moyo na hatutawavunja,” anasema Johnson.

Chama cha Conservative kimeshinda baadhi ya viti katika ngome za chama cha Labour, ambacho kimepoteza viti kaskazini mwa England, Midlands na Wales yakiwa ni maeneo yaliopiga kura ya Brexit katika kura ya maoni mwaka 2016.

Labour inatarajiwa kushinda viti 61 ikiwa ni chini ya viti ilivyoshinda mwaka 2017.

Baadhi ya maeneo bunge kama vile Darlington ama Workington, Kaskazini mwa England, yataongozwa na Mbunge wa Chama cha Conservative kwa mara ya kwanza katika miongo kadhaa- ama katika matukio ya Bishop Auckland na Blyth Vally kwa mara ya kwanza tangu viti hivyo kubuniwa.

Lakini kimeshinda kiti cha eneo bunge la Putney, kusini magharibi mwa London kutoka kwa Conservative.

Chama cha Uskochi cha kitaifa kimepata ushindi wake wa kwanza usiku wa kura, kikishinda eneo bunge la Rutherglen na Hamilton Magharibi kutoka kwa Chama cha Labor na Angus kutoka kwa Conservative.

Huku ikiwa imesalia eneo bunge moja la St Ives ili kutangazwa kwa matokeo rasmi chama cha Conservative kina wabunge 464.

Labour 203, SNP 48, Liberal Democrats 11 huku chama cha DUP kikijipatia wabunge wanane.

Chama cha Sinn Dein kina wabunge saba, Plaid Cymru kina wabunge wanne nacho SLDP kikijipatia wabunge wawili.

Chama cha Green Party pamoja na kile cha Alliance vimejipatia wabunge mmoja mmoja.

Chama cha Brexit kilishindwa kujipatia hata kiti kimoja.

Waziri wa Mambo ya Mdani wa chama cha Conservative, Priti Patel, anasema serikali itahakikisha Brexit inafanyika kwa haraka kabla ya Christmas kupitia kuwasilisha miswada iwapo serikali yake itarudi mamlakani.

Waziri wa Mambo ya Mdani wa chama cha Conservative, Priti Patel

Huu ni uchaguzi wa Uingereza wa tatu chini ya miaka mitano na wa kwanza kufanyika mwezi Desemba katika kipindi cha miaka 100 na umetawaliwa na kura ya maoni ya 2016 ya kuondoka katika muungano wa Ulaya.

Johnson aliangazia ujumbe mmoja- kuhakikisha Brexit inafanikiwa- akiahidi kuiondoa Uingereza katika EU kufikia  Janurai 31, 2020 iwapo angepata wingi wa kura.

Chama cha Labour kilifanya kampeni ya kuongeza matumizi katika huduma za umma mbali na vituo vya afya.

Chama cha Liberal Democrats kiliahidi kufutilia mbali Brexit iwapo kiongozi wake Jo Swinson angechaguliwa kuwa waziri mkuu, lakini kura ya maoni ilitabiri kwamba ufuasi wao utapungua wakati wa kampeni.

Chama cha kitaifa cha Uskochi kilisema kwamba uungwaji mkono wao utaashiria kura ya maoni ya pili kufanyika.

Kiongozi wa SNP Nicola Sturgeon, alituma ujumbe wa twitter kwamba huku matokeo hayo yasiyo rasmi yakiashiria kwamba ulikuwa usiku mzuri kwa chama hicho.

Anaongeza kwamba kile kinachoonekana kuwa ‘kikubwa ni kidogo’.

Caroline Lucas, ambaye matokeo hayo yanaonyesha kwamba anatarajiwa kuwa mbunge pekee wa chama hicho cha Green Party, alituma ujumbe katika twitter akisema: “Iwapo matokeo haya ni ya kweli, basi ni pigo kubwa kwa hali yetu ya hewa kwa kizazi kijacho na demokrasia yetu.

Nigel Farage anasema chama chake cha Brexit kilipata kura kutoka kwa Leba katika maeneo bunge yaliyolengwa na chama cha Consercative ijapokuwa yeye mwenyewe aliharibu kura yake kwa kusema: ‘nisingeweza kukipigia kura chama cha Conservative.”

Fursa kwa Marekani 

Mapema Ijumaa viongozi kadhaa duniani walituma pongezi zao kwa chama cha Johnson kwa kuibuka na ushindi huo mnono akiwamo Rais wa Marekani Donald Trump.

Katika ujumbe wake wa salamu za pongezi, Trump alisema ushindi wa Johnson unamaanisha Uingereza na Marekani zitakuwa huru kufikia makubalino mapya ya biashara baada ya mchakato wa Brexit.

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Cheki, Andrej Babis, ameonya ushindi wa Johnson kwa kusema kuwa siyo habari njema hata kidogo kwa Umoja wa Ulaya.

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Cheki, Andrej Babis

“Hii ni habari mbaya kwa Ulaya, kwani ameshinda na sasa kwa bahati mbaya watatoka ndani ya Ulaya,” anasema Babis.

Mwenyekiti wa Baraza la Ulaya, Charles Michel, amempongeza Johnson na kusema Umoja wa Ulaya uko tayari kujadiliana kuhusu makubaliano ya biashara huru lakini amekwepa kusema kama yanaweza kufikiwa katika kipindi cha mwaka mmoja.

Historia fupi ya Johnson 

Jonson aliingia kwenye wadhfa wa Waziri Mkuu wa Uingereza akimrithi Theresa May, akiwa kiongozi wa chama cha Conservative baada ya kupigiwa kura na wajumbe 160,000.

Kwa mujibu wa taratibu za demokrasia ya Uingereza, kiongozi wa chama chenye uwakilishi mkubwa bungeni huwa waziri mkuu na hivyo baada ya kupigiwa kura za chama, Boris akashika hatua za juu za uongozi wa Uingereza.

Boris ametengeneza jina lake kwa kugawa mawazo ya watu na kuchochea migongano, awali akiwa mwanahabari na baadae mwanasiasa.

Baada ya kuchukua hatamu za uongozi wa chama, wengi walimbeza kuwa hana ujuzi wa kutosha kukiongoza chama hicho.

Tangu mwanzo alijipambanua kama mtu mwenye shaka na Muungano wa Ulaya.

Ni mzaliwa na jijini New York nchini Marekani, baba yake akiwa mwanadiplomasia na mama yake msanii.

Babu yake alikuwa ni mwandishi wa habari wa Kituruki, aliyekulia nchini Marekani, Uingereza na Ubelgiji kabla ya familia yake kurejea rasmi nchini Uingereza.

Amesoma Eton, shule maarufu zaidi ya wavulana nchini Uingereza na huko ndipo dalili za tabia na mtu gani angekuwa zilianza kuonekana.

Kuanzia hapo, akaenda Chuo Kikuu cha Oxford na kuchaguliwa kuwa rais wa chama cha midahalo cha chuo hicho.

Tabia yake ya kuchochea malumbano ilionekana wazi akiwa mwandishi.

Alitimuliwa kazi katika gazeti la The Times baada ya kughushi nukuu.

Baada ya hapo, akaajiriwa kuwa ripota wa jijini Brussels wa gazeti linaloogemea mrengo wa chama cha Conservative la The Daily Telegraph.

“Uandishi wake ulichanganya kwa umaridadi uhalisia na mambo ya kubuni dhidi ya Umoja wa Ulaya,” anaeleza mhariri msaidizi wa BBC wa habari za siasa, John Pienaar.

Habari alizoandika zilizaa mjadala mkubwa na mashambulizi dhidi ya Umoja wa Ulaya ambayo baadae alikuja kuyaendeleza kama mwanasiasa.

Lakini baadhi ya waandishi wenzake walimtuhumu kwa kutokuwa mwaminifu kwa taaluma yake.

Hapo awali, nchini Uingereza alikuwa mwandishi wa makala katika gazeti la The Telegraph na baadae mhariri wa gazeti la mrengo wa kulia, The spectator.

Lakini aliliongezea mashabiki gazeti hilo na wasifu wake katika vyombo vya habari ukakua na akaanza kuonekana katika kipindi cha kila siku cha “Have I Got News For You?” ambacho washiriki hujaribu kufanya ucheshi kuhusu habari za wiki.

Mwaka 2001, alikuwa Mbunge, akikiwakilisha chama cha Conservative katika Wilaya ya Henley-on-Thames, karibu na Oxford.

Katika uchaguzi wa mwaka 2007 kama Meya wa London ndio uliompaisha kwa kasi kubwa katika jukwaa linalojulikana ulimwenguni.

Wakati macho yote duniani yakiiangalia mji ambao ulikuwa mwenyeji wa mashindano ya olimpiki ya mwaka 2012, Jonson alikuwa balozi wa michezo hiyo, ingawaje hayakuandaliawa na City Hall.

Moja ya programu zake maarufu za usafiri alizozianzisha ni uliojulikana kama mpango wa kuendesha baiskeli ”Boris Bike”, na ulianzishwa Julai, 2010.

Lakini wakati Johnson akiwa amerudi bungeni baada ya kushinda kiti katika uchaguzi wa mwaka 2015 na mbele ya kura za maoni za Brexit, Msimamo wa Johson katika suala hili ulikuwa bado haueleweki.

Aliandika nakala katika gazeti akiitaka Uingereza iondoke Umoja wa Ulaya na nakala nyingine anayoitaka Uingereza ibaki katika umoja huo.

Lakini alikuja kuamua kuunga mkono hoja ya Uingereza kutoka Umoja wa Ulaya, kitendo kilichomfanya kwenda kinyume na kiongozi wa chama chake, David Cameron.

Baada ya ushindi wa kutaka Uingereza kutoka EU na Cameron kujiuzulu, Johnson aliweka wazi malengo yake ya kutaka kuchukua nafasi yake kama kiongozi wa chama cha Conservative.

Lakini, Theresa May, aliweza kuibuka mshindi badala yake na wagombea wengine wote walijitoa kugombea nafasi hiyo kabla ya upigaji kura kuanza, Lakini kama shukran kwa Johnson kwaajili ya nafasi yake kama bingwa wa Brexit, akateuliwa kuwa kuwa Katibu wa Mambo ya Nje.

Tangu kiongozi wa chama hicho na hata Waziri Mkuu, hajawahi kukubali kuondoka Umoja wa Ulaya bila makubaliano yoyote.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
198,905FollowersFollow
550,000SubscribersSubscribe

Latest Articles