DURBAN, AFRIKA KUSINI
NYUKI walioingia kwenye injini ya ndege ya Shirika la Ndege la Mango la hapa walisababisha kuchelewa kwa safari za ndege mjini hapa.
Wataalamu wa nyuki waliitwa kuja kusaidia kuwaondoa nyuki hao karibu 20,000 kutoka injini ya ndege hiyo.
Mmoja wa wataalamu hao amesema tukio hilo si la kawaida na kuwa huenda nyuki hao walikua wakipumzika kabla ya kuelekea mahali pengine.
Ameongeza kuwa hawakua na mpango wa kuishi ndani ya injini iliyo na harufu kali.
Nyuki hao walijaa ndani ya injini hiyo kwa dakika 25 kabla hawajaondolewa na wataalamu, hali ambayo ilisababisha ndege zingine tatu kuchelewa kuondoka katika uwanja huo wa Kimataifa wa King Shaka.
Msemaji wa Shirika la Ndege la Mango, Sergio dos Santos amesema ”Sijawahi kuona kisa kama hiki katika kipindi cha miaka minane niliyohudumu katika shirika la ndege”