25.9 C
Dar es Salaam
Monday, November 25, 2024

Contact us: [email protected]

NYERERE HAKUWAHI KUJUA KUENDESHA GARI

Na Markus Mpangala,

KITABU chetu cha leo ni “Mlinzi Mkuu wa Mwalimu Nyerere,” kimeandikwa na Peter D. Bwimbo na kuchapishwa na kampuni ya Mkuki na Nyota. Kina nambari ISBN 9789987-753-32-1. Peter D. Bwimbo alikuwa afisa usalama wa taifa hivyo kuwa mlinzi mkuu wa Mwalimu Nyerere lilikuwa suala la utaratibu.

Mwandishi anatuachia kumbukumbu kuhusu maisha ya Mwalimu Nyerere na masuala ya ulinzi na usalama pamoja na maisha ya nyakati za ukoloni na baada serikali mpya ya Tanganyika (Tanzania) changamoto, mafunzo na maasi ya kijeshi ya mwaka 1964.

Kitabu hiki kinaeleza maisha ya makachero ama vyombo vya dola vinavyofanya kazi usiku na mchana kuhakikisha viongozi wetu wanaishi kwa amani na utulivu.  Pamoja na changamoto za kuwalinda wananchi nchini kuanzia Special Branch (Idara ya Usalama wa Taifa kabla ya ukoloni) ambayo baadaye ilibadilishwa na kuitwa TISS (Tanzania Intelligence and Security Service).

Matukio muhimu yanayotajwa ndani ya kitabu hiki, “Kwa hiyo kazi ya kuwaelemisha wananchi kwa njia ya mikutano ya hadhara kuhusu masuala ya siasa na faida ya kujitawala ilikuwa ngumu sana iliyohitaji Mwalimu Nyerere na wenzake kujitolea kusafiri kwa shida umbali mrefu na kwa njia mbaya vijijini na mijini wakati mwingine kwa miguu kuwafikia wananchi mahali walipo. Aidha, wananchi nao wakati mwingine waliogopa kuhudhuria mikutano hiyo kwa hofu ya uwezekano wa kukamatwa na vyombo vya serikali ya kikoloni hata kama mikutano hiyo kwa bahati ilipewa vibali,” (Uk. Uk. 24).

Mwandishi anasema kulikuwa na nyakati ngumu za kupigania uhuru na baada ya wakoloni kuondoka. Baadhi ya maofisa wa kizungu walichukizwa na kupatikana kwa uhuru wakaamua kutotoa mafunzo yoyote.

“Maofisa Wazungu katika Special Branch (Idara ya Usalama) kabla hawajarudi kwao kufuatia program ya Africanisation (neno hilo lilitumiwa hivyo hivyo katika Kiswahili kuwa frikanaizesheni), hawakutayarisha mwongozo wowote ingawa kitengo hiki walikianzisha wenyewe. Kwa hiyo, wakati nakabidhiwa kushika madaraka haya nilielezwa tu na Tim Hardy kwamba nitaongoza kitengo hiki cha ulinzi wa waziri mkuu Julius Nyerere kuanzia mwezi Agostia 1961,”(Utangulizi uk.XI).

Aidha, “Tanganyika ilipata serikali ya madaraka ya ndani tarehe 3 Septemba 1960, wakati huo mimi bado nikiwa masomoni Uingereza. Baada ya TANU kushinda katika uchaguzi na kupata idadi kubwa ya wajumbe katika Barazala la Kutunga Sheria (Legco) Mwalimu aliteuliwa na Gavana kushika wadhifa wa waziri mkuu (Chief Minister) Special Branch wakati huo ilikuwa chini ya Jeshi la Polisi,” (Uk. 29)

Hii ina maana kuwa kabla ya Uhuru kamili, Tanganyika ilianza kwa kupewa serikali ya madaraka ya ndani (Internal self Government). Kwenye suala la kuwalinda viongozi, anasema “Ulinzi wa Mwalimu Nyerere kwa ujumla haukuwa rahisi, ikilinganishwa na ulinzi wa viongozi wengine, kwa sababu alijiamini kuhusu maisha yake ya kisiasa kiasi cha kutokuwa na wasiwasi,” (Uk.33).

Nyerere alikataa sanamu yake kuweka katikati ya jiji. “Mara baada ya uhuru, Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam wakati huo walitaka sanamu yake itengenezwe ichukue nafasi ya ile ya asakri wa vita mwenye bunduki na singe katika maungano ya Mtaa wa Samora, Azikiwe na Makunganya, alikataa kata kata kwa maelezo kuwa sanamu kama hizo hazifai katika nchi zinazozingatia demokrasia na kuongozwa kwa utaratibu wa kupokezana madaraka muda unapokwisha,” (Uk.39).

Mnamo Januari 22, 1962, Mwalimu Nyerere alipotangaza kujiuzulu wadhifa wake wa uwaziri mkuu  kwa madai hakuwa akisikilizwa na serikali ya wakoloni. Baada ya kujiuzulu, alimteua Rashid Kawawa kuwa Waziri Mkuu (Uk.45).

Kuhusu maisha binafsi, kwa mfano, kabla ya uhuru palikuwa na Mwafrika mmoja tu nchini Tanganyika aliyekuwa na Digrii ya Masters aliyoipata mwaka 1952, miaka tisa kabla ya uhuru. Kulikuwa na madaktari Waafrika 12 pamoja na wahandisi Waafrika wawili wakati ambapo idadi ya watu wote nchini Tanganyika wakati huo ilikadiriwa kuwa milioni nne. Idadi hii ya wasomi nchini Tanganyika wakati huo alitajwa na Mwalimu Nyerere jijini Brasilia, Brazil tarehe 18 septemba 1996 katika hotuba yake aliyotoa kuhusu hali ya Afrika katika kipindi cha kuelekea karne ya 21. Mtu pekee Tanganyika aliyekuwa na digrii ya masters alikuwa yeye Mwalimu Nyerere lakini kwakuwa hakuwa mtu wa majivuno hilo hakulitaja,” (Uk.55).

Linalovuta hisia zangu ni hili, “Yeye mwenyewe Mwalimu Nyerere ameongoza nchi hii kwa muda mrefu lakini kadri ninavyofahamu, hakuweza kumiliki hata gari moja hadi anang’atuka kutoka ngazi ya urais wala hakujifunza kuendesha gari, bali alijua kuendesha Baiskeli,” (Uk.60).

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles