Na Damian Masyenene, Shinyanga
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Wilaya ya Kahama mkoani Shinyanga, imebaini uchinjaji holela wa mifugo katika Manispaa ya Kahama na kumshauri Mkurugenzi wa Manispaa hiyo kuzifunga machinjio zote zinazoendeshwa kienyeji.
Katika ripoti yake iliyotolewa jana na Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Shinyanga, Hussein Mussa, taasisi hiyo imebaini kuwa nyama za nguruwe zinachinjwa bila ya kukaguliwa na Maafisa Mifugo, huku nyama zinazozikwa kwa kutozingatia taratibu za uchinjwaji zikifukuliwa na kuuzwa.
Akitoa ripoti hiyo, Mussa amesema kuwa TAKUKURU wilaya ya Kahama ilipokea taarifa juu ya uwepo wa tuhuma na malalamiko ya uchinjaji wa nyama katika Manispaa ya Kahama ambao haufuati taratibu na Kanuni za uchinjaji.
Hatua hiyo inasabanisha nyama kuingizwa katika maeneo ya kuuzia kitendo ambacho ni hatari kwa afya za watumiaji wa nyama hizo.
Aidha taarifa ilieleza kuwa mifugo hasa nguruwe mara nyingine huchinjwa ikiwa tayari imeshakufa ama kutokaguliwa na Maafisa Mifugo.
“Baada ya kupokea taarifa hiyo, Takukuru Kahama kwa mujibu wa jukumu la uzuiaji rushwa kama lilivyoainishwa katika Kifungu cha 7 cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Na. 11 ya Mwaka 2007.
“Tulianzisha uchunguzi na ufuatiliaji na kuweza kubaini nyama iliyohifadhiwa katika jokofu la Ofisi ya Mifugo Manispaa ya Kahama ambayo ilithibitika mnyama huyo kuchinjwa akiwa tayari amekufa na ilikamatwa ikiwa tayari kwa muuzaji wa Kitimoto aliyepo katika eneo la Mbulu Manispaa ya Kahama.
“Aidha uchunguzi uliweza pia kubaini eneo la machinjio ya nyama za nguruwe lilipo Nyakato Kahama ambapo tuliweza kujiridhisha kwa kuona eneo ambalo lilifukiwa na kuzikwa nyama ya nguruwe iliyochinjwa kinyume na taratibu usiku wa Aprili 10,2021 ikiwa imefukuliwa na kupelekwa kusikojulikana,” ameeleza.