27.5 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

TEMESA ondoeni magari mabovu yote- Waitara

Na Mwandishi Wetu, Dodoma

Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mwita Waitara, ameutaka Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA), kuhakikisha wanayatoa magari yote yaliyotelekezwa na wamiliki wake katika karakana zote nchini na kusababisha mrundikano ndani ya karakana hizo.

Kaimu Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA), Heriel Mteri akiwasilisha taarifa ya Wakala kwa Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mwita Waitara, wakati alipotembelea Wakala huo, jijini Dodoma

Akizungumza na Menejimenti ya Wakala huo, jijini Dodoma, Waitara amesema kuwa hatua hiyo itapelekea kupunguza msongamano katika karakana hizo na hivyo kupatikana kwa nafasi ili kuruhusu magari mengine kupata huduma kiurahisi.

“Magari hapa ni mengi na mlundikano ni mkubwa, mengine yanaonekana ni ya muda mrefu, hakikisheni mnayatoa na kuyapeleka kwa wenyewe ili kupunguza msongamano hapa na hata katika karakana zenu nyingine nchi nzima,” amesema Waitara.

Aidha, Waitara ameutaka Wakala huo kuboresha huduma zao nchi nzima ikiwemo kutatua mianya yote inayopelekea uhujumu na kupelekea utendaji wa kusuasua kwa watumishi wa Wakala huo.

“Hakikisheni kuwa mnapunguza gharama, mnatumia muda mfupi na vipuri sahihi katika utengenezaji wenu wa magari, mkifanya hivi mtapunguza malalamiko kutoka kwa washitiri wenu,” amesisitiza Waitara.

Aidha, ameagiza Wakala huo kuhakikisha wanatafuta njia sahihi ya kuhifadhi mafuta machafu yanayomwagika wakati wa utengenezaji wa magari ili kuhifadhi mazingira katika maeneo yao ya kazi.

Kuhusu suala la vivuko, Waitara ameutaka Wakala huo kuhakikisha kila kivuko kinajisimamia na kujiendesha kwa faida na kutaka Wakala huo kupitia upya tozo za nauli za vivuko nchini katika baadhi ya maeneo bila kuumiza wananchi.

“Huduma za Serikali hazitakiwi kufanywa kwa kubahatisha, kwa mfano katika Kivuko cha Nyamisati utaratibu wa safari na nauli haueleweki, wananchi wa huko wanalalamika sana, kaeni mlirekebishe hili, Serikali haitaki watu wababaishaji,” amefafanua Naibu Waziri huyo.

Kwa upande wake, Kaimu Mtendaji Mkuu wa Wakala huo, Heriel Mteri, amesema kuwa Wakala unakabiliwa na changamoto mbalimbali ikwemo wakala kuendesha baadhi ya vivuko vyenye mapato madogo na hivyo kushindwa kujiendesha vyenyewe na kupelekea Wakala kutoa ruzuku ya kuviendesha.

Ametaja changamoto nyingine kuwa ni uchakavu wa miundombinu na vifaa vya karakana ambapo amesema kuwa karakana hizo zimejengwa miaka mingi iliyopita hivyo kuhitaji ukarabati mkubwa.

Ameongeza kuwa, kwa sasa Wakala unatumia mfumo wa kisasa wa kubaini vipuri ambavyo sio halisi katika karakana zake zote ili kudhibiti udanganyifu ambao unafanywa na baadhi ya wafanyabiashara.

Naibu Waziri Waitara, amefanya ziara TEMESA jijini Dodoma, ili kujionea utendaji wa wakala huo na kuzungumza na Menejimenti  kuhusu namna ya kuboresha huduma katika Wakala huo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles