*Mbowe asema hawatarudi nyuma licha ya hujuma
Na MWANDISHI WETU -DAR ES SALAAM
MBUNGE wa Singida Kaskazini, Lazaro Nyalandu (CCM), yuko Kenya kukamilisha mipango wa kumhamishia Marekani kwa matibabu zaidi, Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu (Chadema), aliyelazwa hospitalini Nairobi akitibiwa majeraha ya risasi.
Lissu ambaye pia ni Mwanasheria Mkuu wa Chadema na
Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), alishambuliwa kwa risasi na watu wasiojulikana Septemba 7, mwaka huu mjini Dodoma, amelazwa chumba cha uangalizi maalumu (ICU) katika Hospitali ya Nairobi.
Nyalandu jana aliandika katika ukurasa wake wa Instagram na Facebook akisema amerudi Nairobi kushiriki juhudi za kumhamishia Lissu Marekani.
“Tumekuwa Hospitali ya Nairobi tukisubiri madaktari watoe ripoti ya mwenendo wa matibabu ya Lissu kwa ajili ya kuwapatia madaktari bingwa wa Marekani na kuona uwezekano wa Lissu kupatiwa rufaa kwa matibabu zaidi nje.
“Lakini bado kalamu zao ni nzito kuandika ripoti hii siku ya tatu tangu tuahidiwe. Binafsi nimerudi Nairobi tangu jana (juzi) kushiriki maandalizi ya uwezekano wa kumhamishia Lissu Marekani kwa ajili ya huduma yenye ubora zaidi.
“Endapo madaktari wa Nairobi wangeridhia. Kesho asubuhi (leo) nitarejea hospitalini kusikiliza kauli ya mwisho ya madaktari kuhusu ripoti hiyo,” aliandika Nyalandu.
Nyalandu amekuwa mbunge wa kwanza wa CCM kujitokeza hadharani kwenda Nairobi na hata kuhamasisha michango ya matibabu ya Lissu kwa wakazi wa Singida na Watanzania wengine huku akisistiza watu kuendelea kumuombea.
Mbali na Lissu, katika siku za karibuni, Nyalandu amejipatia sifa za pekee baada ya kuwapeleka Marekani kwenye matibabu, wanafunzi watatu wa Shule ya Lucky Vincent ya Arusha walionusurika kwenye ajali ya barabarani iliyosababisha vifo vya wanafunzi 32, walimu wawili na dereva.
Mbowe atoa maneno mazito
Akihojiwa na Radio Idhaa ya Kiswahili ya Ujerumani (DW) juzi, Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe alisema kazi ya upinzani Tanzania hivi sasa ni ngumu hasa katika utawala wa serikali ya awamu ya tano.
“Kazi ya upinzani ni ngumu hasa katika zama za utawala wa awamu ya tano ambao unaonekana hautambui na kuthamini mchango wa wapinzani kama walivyokuwa watangulizi wengine.
“Licha ya vitisho na kila aina ya hujuma tunazofanyiwa kamwe hatuwezi kurejea nyuma, bali tutafanya kazi zetu kwa tahadhari kubwa kuliko ilivyokuwa miaka iliyopita ambayo tulikuwa na uhuru mkubwa wa kujieleza na Serikali kuyafanyia kazi mambo tunayosema.
“Huwezi kuendesha nchi bila kuruhusu ukosoaji, iwe kutoka upinzani au kwenye chama unachokiongoza.
“Unapowazuia watu wasipumue na kutoa madukuduku yao, unatengeneza hasira kubwa ndani ya jamii,”alisema Mbowe.
HALI YA LISSU
Kuhusu afya ya Lissu, Mbowe ambaye pia ni Mbunge wa Hai alisema kupona kwa mbunge huyo wa Singida Mashariki ni mpango wa Mungu.
“Nawaomba Watanzania wenzetu waendelee kumuombea kwa Mungu na kuchangia gharama za matibabu kwa kuwa gharama zake ni kubwa ambazo chama pekee hakiwezi kuzimudu bila ya misaada kutoka kwa watu mbalimbali.
“Unajua, ahueni humtokea mgonjwa taratibu taratibu na ndivyo inavyotokea kwa Lissu ingawa sisi wote tuna hamu apone mara moja aje aendelee kupigania haki za wanyonge kama alivyokuwa akifanya.
“Sisi tunatoa taarifa za maendeleo ya Lissu kulingana na madaktari wanavyotuambia.
“Hatuwezi kusema chochote nje ya wataalamu hao kwa kuwa ndiyo wenye ujuzi wa kumtibu na kujua maendeleo ya mgonjwa husika,”alisema kiongozi huyo wa Kambi ya Upinzani Bungeni.