Na MWANDISHI WETU-DAR ES SALAAM
WATANZANIA wametakiwa kuchangamkia fursa ya nyumba za Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF) ili waweze kuishi kwenye makazi bora na kwa bei nafuu.
NSSF imesema nyumba hizo 99 zote zipo Dungu, Kigamboni, Dar es Salaam, na tayari zimekamilika, ambapo 55 zimepangishwa kwa wananchi mbalimbali, 10 zimekabidhiwa kwa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya Kigamboni na 16 zimekabidhiwa kwa wakuu wa idara wa Halmashauri ya Kigamboni.
Akizungumza wakati alipofanya ziara ya kutembelea mradi huo mwishoni mwa wiki, Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, William Erio, alisema nyumba 15 zilizobaki zinapangishwa kwa wananchi mbalimbali wenye uhitaji kwa bei nafuu.
“Nawaomba Watanzania kuchangamkia fursa ya uwepo wa nyumba hizi ambazo zinauzwa na kupangishwa ili waishi kwenye makazi bora ambayo NSSF inayatoa,” alisema Erio.
Alisema mradi wa nyumba hizo umeshakamilika tangu mwishoni mwa mwaka jana, kutokana na maelekezo ya Rais Dk. John Magufuli.
“Nyumba hizi ni nzuri kama mnavyoziona wenyewe hapa, hivyo kila mwananchi anayehitaji kupanga anakaribishwa,” alisema Erio.
Alifafanua kuwa bei ya upangaji wa nyumba hizo ambayo imepitishwa na Mthamini Mkuu wa Serikali kodi ni kati ya Sh 250,000 hadi 500,000, ambapo mteja anaweza kulipa kwa mwezi, miezi mitatu hadi mwaka kutegemeana na aina ya nyumba.
Aidha, alisema pamoja na hayo kuna service charge ya Sh 100,000.
Meneja wa Miliki wa NSSF, Augustino Paul, aliwataka wananchi kuchangamkia nyumba ambazo ziko Kigamboni na Toangoma kwani bei yake ni nzuri kwenye kupangisha.
Kwa mujibu wa meneja huyo, Shirika lina nyumba 76 zilizoko Toangoma ambazo zinauzwa na kupangishwa kwa wananchi.
Alisema nyumba hizo zinapangishwa kati ya Sh 350,000 na 400,000 kwa mwezi.
Agustino alisema kuwa shirika hilo pia lina nyumba 33 zilizopo Mtoni Kijichi zinazopangishwa kati ya Sh 400,000 na 500,000.