23.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, April 16, 2024

Contact us: [email protected]

Fili Karashani; Mbuyu wa uandishi ulioanguka

Na Kajubi Mukajanga

SAA 6:21 mchana wa Jumapili, Mei 10, mwaka huu nilizungumza na Kagina Karashani kuhusu maendeleo ya matibabu ya baba yake, Fili Karashani na mipango ya kumtembelea hospitali katika mazingira ya homa kali ya mapafu (Covid-19) yaliyofanya uongozi wa Hospitali ya Muhimbili (MNH) kuamua awe anaonwa na mtu mmoja tu kwa siku.

Alikuwa amelazwa Muhimbili kwa matatizo ya moyo ambayo yamekuwa yakimsumbua kwa muda wa miaka kadhaa.

Saa sita baadaye, 12:23, nikapokea simu ya Kagina: “Habari ni mbaya. Mzee amefariki.”

Nilimfahamu Fili Karugahale Karashani kama rafiki mcheshi, rafiki wa kifamilia, mtu wa masihara ambaye katika nyakati za furaha alinihakikishia kuwa ataandika wasifu wangu pindi nitakapofariki. Nilikuwa nikimjibu kuwa mimi ndiye nitakayeandika wa kwake. Na sasa nauandika.

Nilimfahamu pia kama mwanataaluma mahiri wa uandishi wa habari, na mkufunzi bora. Kabla sijawa Katibu Mtendaji wa Baraza la Habari Tanzania (MCT), tulizunguka nchi nzima kufundisha maadili ya uandishi, stadi za uongozi katika klabu za waandishi, mbinu za uandishi wa uchunguzi, uandishi wa habari za uchaguzi na uandishi wa makala.

Machi 30, 2012, Fili, kama anavyojulikana kwa wengi, alikuwa mtu wa kwanza kutunukiwa Tuzo ya Maisha ya Mafanikio katika Tasnia ya Habari (Lifetime Achievement in Journalism Award) ambayo alikabidhiwa na Rais mstaafu Jakaya Kikwete katika Ukumbi wa Diamond Jubilee. Tuzo hizo huandaliwa na MCT na washirika wake na hutolewa katika kilele cha Tuzo za Umahiri katika Uandishi wa Habari nchini, EJAT.

Alikuwa mmoja wa wanahabari Watanzania ambao usingeweza kuongelea uandishi wa habari uliotukuka bila kuwataja. Nguli huyu alikuwa katika taaluma hii kwa miongo mitano kama ripota, mwandishi wa makala, mhariri, mkufunzi, mtafiti na mtaalamu mshauri wa masuala ya habari hapa nchini na ughaibuni. Kwa maneno yake mwenyewe, alijinasibu: “I am a child of the Media” (Mimi ni mtoto wa Tasnia ya Habari).

Fili alianza maisha ya kazi kama msaidizi wa duka la vitabu mjini Dodoma mnamo mwaka wa 1960, ambapo alijenga tabia ya kujisomea, na baadaye kuandika. Akahudhuria warsha ya uandishi wa habari huko Kiomboi mkoani Singida, iliyoandaliwa na Christian African Writing Centre iliyokuwa na makao makuu Kitwe, Zambia na kumaliza akiwa mwanafunzi bora darasani. Ushindi huo ulimwezesha kupata udhamini wa kusomea cheti cha uandishi huko Kitwe, akiwa mmoja wa vijana 30 waliokusanywa kutoka kusini, mashariki na magharibi mwa Afrika. Baada ya kupata cheti chake akaajiriwa kama ripota katika magazeti ya Target na Lengo, ambayo yalikuwa ndiyo kwanza yameanzishwa kwa ushirikiano kati ya mabaraza ya Kikristo ya Kenya na Tanzania.

Miaka miwili baadaye, mwajiri wake akampeleka kusomea Diploma ya Uandishi iliyoandaliwa na taasisi ya kimataifa ya wahariri, International Press Institute. Kwa mara nyingine, Fili akawa wa kwanza katika darasa la wanafunzi 30 kutoka kusini na mashariki mwa Afrika. Wakati wa sherehe za mahafali, Mhariri wa Taifa Leo, linalochapishwa na Nation Media Group (NMG) ya Kenya akamfuata na kumweleza kuwa angependa kumpa kazi. Fili akakubali. Hiyo ilikuwa mwaka 1964. Miezi mitatu tu baadaye, wahariri wa Daily Nation, gazeti jingine la NMG, “wakamwiba” kutoka gazeti lao dada. Akaingia chumba cha habari cha gazeti lao la Kiingereza akiwa Mtanzania pekee.

Tangu hapo, Fili hakuwahi kutazama nyuma.

Kwa Fili, ukweli na usahihi (truth and accuracy) ndiyo msingi wa uandishi wa habari. Mhariri wake wa Habari pale Daily Nation, Mike Chester, alikuwa kati ya watu waliosaidia kumfinyanga Fili kuwa gwiji wa taaluma hiyo. Chester hakuwa na masihara kazini na kwake, stori ilikuwa haijakamilika bila kujibu maswali “kwa nini” na “kwa jinsi gani”.


Rais Jakaya Kikwete akimkabidhi mwandishi mkongwe Fili Karashani Tuzo ya Maisha ya Mafanikio katika Tasnia ya Habari mwaka 2011, katika tuzo za (EJAT) zilizoandaliwa na Baraza la Habari Nchini Tanzania (MCT).Kushoto ni Mwandishi wa siku nyingi Khamis Ben Kiko

Kati ya kazi alizofanya wakati huo ni pamoja na kuripoti machafuko ya kijamii, ukame na njaa huko Wajir, mpakani mwa Kenya na Somalia. Baadhi ya stori alizoandika zilimuudhi aliyekuwa Waziri wa Kilimo wa Kenya wakati huo, Jeremiah Nyagah. Lakini ukweli na usahihi ukamwokoa, hakufanywa chochote.

Aliandika pia matatizo ya wananchi huko Baringo, jimboni kwa Daniel arap Moi, wakati huo akiwa Makamu wa Rais na Waziri wa Mambo ya Ndani. Mzee Moi hakupendezwa sana na stori za Fili na akaagiza aletwe kwake. Alipofika, akamtazama Fili kwa mshangao toka chini hadi juu na kumaka, “Oh, huyu ndiye Karachani – nilidhani ni Mhindi! Kwenda!”

Awali, lengo lilikuwa kumsweka korokoroni. Ukweli na usahihi vikamwokoa.

Tom Mboya alipouawa, Fili ndiye aliyeliandikia Daily Nation mkasa huo.

Mwaka 1967, akahamishiwa Dar es Salaam kwa mwaka mmoja na kuendelea kupeleka Nairobi stori kemkem. Asilimia kubwa ya stori za Tanzania zilizochapishwa ukurasa wa mbele wa Daily Nation wakati huo ziliandikwa na Fili.

Aliporudi Nairobi, Fili alikwea vidato toka ripota hadi mwandishi mkuu wa habari za Bunge, akawa pia mwanasafu, na baadaye Mhariri-usu/Msanifu Habari (Sub-editor). Alikuwa pia akiandika safu kuhusu masuala ya Tanzania katika gazeti hilo lililoongoza kwa mauzo Afrika Mashariki.

Baadaye akaacha kazi na kujiunga Chuo Kikuu cha Dar e Salaam na kupata shahada yake ya kwanza mwaka 1978, kisha shahada ya uzamili kutoka Chuo Kikuu cha Queens, Canada, mwaka 1981.

Baada ya chuo kikuu, Fili akajiunga na gazeti la Daily News kabla ya kuwa mkufunzi katika Chuo cha Uandishi wa Habari Tanzania (TSJ). Akiwa mkufunzi, akawa pia akiandikia majarida na taasisi za nje likiwamo jarida maarufu la Africa Now na Shirika la Inter Press News Agency (IPS). Kwa bahati mbaya, jambo hili lilitafsiriwa na wakubwa wake kuwa ni “kufanya kazi mbili”, japo kwake yeye aliona ni njia ya kuwaonyesha wanafunzi kwa vitendo jinsi uandishi bora ulivyo. Alipoona anasakamwa sana, akaacha kazi na mara moja IPS wakamchukua na kumpa kazi Roma, Italia na baadaye wakampeleka Harare, Zimbabwe, kama Mkuu wa Kituo (Bureau Chief).

Aliporudi Tanzania 1989 akawa Mhariri mwanzilishi wa Business Times, akiwa na kina Rashid Mbuguni, Narendra Joshi, Ali Chimbyangu na Richard Nyaulawa.

Mwaka 1991, Fili aliajiriwa kama Mhariri wa Southern Africa Economist jijini Harare kabla ya kurudi Dar es Salaam na kuwa mhariri mwanzilishi wa The Guardian na baadae Sunday Observer.

Mnamo 2004 hadi 2005, alikuwa The Citizen kama Mhariri wa Mafunzo.

Katika miaka ya mwisho ya maisha yake, Fili ambaye waandishi wengi wamepitia mikononi mwake akiwa mhariri na mwalimu, aliendelea kutoa mafunzo ya uandishi, hususan uandishi wa habari za uchunguzi, makala na maadili. Alitoa pia huduma kama mtaalamu mshauri wa masuala ya habari, huku akichangia katika majarida ya kitaaluma yakiwamo Scribes la MCT na The Global Journalist la Shule Kuu ya Uandishi wa Habari ya Chuo Kikuu cha Missouri, Marekani.

Vitabu alivyoandika au kushiriki kuandika ni pamoja na: To Write or Not to Write – Ethical Concerns in Journalism; Poverty Reporting – A Manual for Tanzanian Journalists; Media Ethics: Duties and Responsibilities; Feature Writing Manual na Investigative Journalism Practice in Tanzania.

Fili alipata kuwa Katibu Mkuu wa Chama cha Wanahabari wa Kenya (Kenya Union of Journalists) na katika miaka yake ya mwisho alikuwa mwenyekiti wa Kituo cha Habari, Tanzania Press Centre kabla ya kupatwa na matatizo ya kiafya.

Fili Karashani alizaliwa Agosti 23, 1938 mjini Dodoma. Baba yake alikuwa Yakobo Kagina, Mchungaji wa Kanisa la Anglikana na mama yake aliitwa Blandina.

Fili na mkewe, Geraldina, walijaaliwa watoto watano: Magezi, Baraka, Kagina, Koku na Bahati. Baraka, aliyechukua kazi ya baba yake ya uanahabari, alishatangulia mbele ya haki. Fili pia ameacha wajukuu nane.

Mungu ailaze pema roho ya marehemu Fili Karugahale Karashani — Amina.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles