Na ASHA BANI-DAR ES SALAAM
ALIYEKUWA Mwenyekiti wa Mtandao wa Wanafunzi Tanzania (TSNP), Abdul Nondo, hatimaye amesema kuwa ameruhusiwa kurudi kuendelea na masomo yake Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Januari 4, mwaka huu.
Nondo ambaye alikuwa akikabiliwa na kesi ya udanganyifu, alishinda kesi hiyo iliyokuwa ikimkabili katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Wilaya ya Iringa.
Akithibitisha kurudi kwa Nondo chuoni, Naibu Makamu Mkuu wa Chuo (Taaluma), Profesa Bonaventure Rutinwa alisema anatakiwa kurudi shule na taratibu zote zilishakamilika licha ya kwamba aliwaachia walimu wengine katika ofisi ya taaluma.
“Tayari kweli tulipokea barua yake na mimi niko likizo anatakiwa kuanza chuo afike ofisini maagizo yote niliacha kwa msaidizi wangu Rose Ufoo,” alisema Profesa Rutinwa kwa njia ya simu akiwa Bukoba mkoani Kagera.
Kwa mujibu wa Nondo mara baada ya hukumu ya Mahakama ya Iringa kutoka na kumkuta hana hatia alitakiwa kurejea shule kwa ajili ya kumalizia muhula wake wa masomo ya mwaka wa tatu.
Akizungumza na MTANZANIA jana alisema baada ya kuonekana hana hatia wakili wake Jebra Kambole, alifanya mchakato wa kuandika barua kwenda kwa Makamu Mkuu wa Chuo, akiambatanisha na nakala ya hukumu.
“Baada ya kuandika barua hiyo niliendelea kufuatilia majibu ila ikawa bado ipo inafanyiwa kazi. Ikipita kwa Naibu Makamu wa Elimu (DVC-Academic) hadi kwa mkuu wa Idara ya Masomo ya Shahada, baadaye ikaenda kwa Mwanasheria wa Chuo kwa muda wote takribani wiki tatu naambiwa inafanyiwa kazi,” alisema alieleza Nondo .
Alisema baadaye walijibiwa kuwa nakala ya hukumu aliyopeleka chuoni hapo haikuwa ya halali ilikuwa sio halisi (Original) hivyo hawakuweza kuiamini kama imetolewa na mahakama ama laa.
“Baadaye nilikwenda tena Iringa kuichukua hukumu Original kwa Wakili wangu Chance Luoga , akanipa hukumu yenye muhuri wa mahakama , hivyo nikaileta wakili wangu Kambole ikabidi aiandikie barua tena akiambatanisha na hiyo hukumu na kuipeleka chuoni,” alisema.
Aliendelea kueleza kuwa baada ya kuipeleka alifuatilia majibu lakini akaambiwa bado inafanyiwa kazi .