Na Mwandishi wetu, Mwanza
Benki ya NMB imezindua huduma ya Mikopo ya pikipiki za miguu miwili na miguu mitatu kwa wakazi wa kanda ya ziwa na kuahidi kutumia zaidi ya Sh bilioni 5 kutoa mikopo kwa vijana zaidi ya elfu 75 nchini.
Akizungumza katika uzinduzi wa mikopo hiyo kwa vijana waendesha bodaboda na bajaji jijini Mwanza, Afisa Mtendaji Mkuu wa benki ya NMB, Ruth Zaipuna aliwataka wanufaika kujitokeza na kuchagamkia fursa hiyo.
Alisema ikiwa vijana na watu wengine waliojiunga katika umoja wa waendesha bodaboda na bajaji watajitokeza na kuchangamkia fursa hiyo, NMB inaweza kuongeza kiwango cha utoaji mikopo.
Ruth alisema kwa mara ya kwanza walizindua huduma hiyo jijini Dar es Salaam mwezi wa nne mwaka huu na kwamba jana waliingia jijini Mwanza ili kuhakikisha vijana wanatumia fursa hiyo kupata mikopo na hivyo kujiajiri wenyewe.
“Hatutaki mikopo hii iwe mizigo kwenu bali baraka kwenu na NMB imedhamiria kufika katika mikoa mingine hapa nchini kwa ajili ya utoaji wa mikopo hii,”‘ alisema Ruth
Afisa Mtendaji huyo wa NMB alisema, hatua ya utoaji wa mikopo hiyo ni ombi la serikali la kuomba wasaidie vijana kupata mikopo ya bodaboda na bajaji na kwamba wameamua kulitekeleza kwa vitendo.
Kwa upande wake, Mkuu wa kitengo cha wafanyabiashra wadogo wa NMB, Filbert Mponzi akizungumza katika uzinduzi wa mpango huo, alisema benki hiyo imeandaa mfumo wa malipo ya Master Boda QR utakaomuwezesha mteja kumlipa bodaboda nauli.
Alisema ili kupata mkopo wa bodaboda lazima kila mwanachama wa umoja wa waendesha bodaboda afungue akaunti ya NMB na kuanza kuingiza fedha anayolipwa na wateja kama nauli walau kuanzia miezi mitatu.
Aidha, alisema kila mwezi wanatoa mikopo ya wajasiliamali hapa nchini inayofikia Sh bilioni 40.
Kwa upande mwingine, aliwaomba Watanzania kujiunga katika vikundi na kufungua bima ya mkono wa pole ambayo itawasaidia wanapopata misiba katika familia zao.
Alisema kiwango cha kila mwanachama katika kikundi anatakiwa Sh. 2000 kwa mwezi na kwamba ikiwa atafariki NMB itatoa Sh. milioni 5.
Aidha, alisema bima hiyo pia itahusisha mwanachama kufiwa na mke na watoto ambapo pia NMB itatoa rambirambi.
Katibu wa waendesha bodaboda mkoani Mwanza, Samue Antony akizungumza katika uzinduzi huo alisema wameweza kuunganisha vijana 100 waliokuwa wakitumia madawa ya kulevya na sasa wamekuwa watu wema ambao wanashirkiana nao.
Aliomba NMB kuendelea kuwapa elimu kuhusu namna bora ya matumizi bora ya fedha watakazopata kupitia vyombo hivyo ili waweze kunufaika.
Akizindua mpango hu wa mikopo, Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Salum Kalli aliwahakikishia usalama waendesha bodaboda na bajaji muda wote watapokuwa kazini.
Aidha, aliwataka kuheshimu mikopo watakayopatiwa ili iweze kuwasaidia na kusaaidia makundi mengine ya kijamii katika jiji la Mwanza na maeneo mengine.