Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
Benki ya NMB imetoa msaada wa viti 60 na meza 60 vyenye thamani ya Sh milioni 14 kwa walimu wa Shule za Msingi Mtambani iliyopo Kata ya Tabata na Mgeule iliyopo Kata ya Chanika waweze kufanya kazi katika mazingira mazuri.
Akizungunza wakati wa kukabidhi msaada huo katika Shule ya Msingi Mtambani, Meneja wa NMB Kanda ya Dar es Salaam, Donatus Richard, amesema lengo ni kuhakikisha tatizo la meza na viti katika shule hizo linakuwa ni historia.
“Tunaunga mkono juhudi za maendeleo za nchi na Serikali, changamoto ya elimu kwetu ni kipaumbele kikubwa ndiyo maana tumeona tusirudi nyuma katika kutatua changamoto hii. Tumekuwa tukitenga asilimia moja ya faida yetu tunayopata kila mwaka kusaidia jamii kwenye elimu, afya na majanga mbalimbali,” amesema Richard.
Kwa upande wake Mkuu aa Wilaya ya Ilala, Ng’wilabuzu Ludigija, ameishukuru benki hiyo kwa msaada huo kwani utasaidia kutatua changamoto ya viti na meza katika shule hizo.
“Tunatambua Serikali imekuwa ikitoa elimu bila malipo tumekuwa na watoto wengi na kwa miundombinu tuliyokuwa nayo tumekuwa na upungufu wa madarasa, madawati, matundu ya vyoo kwa kiasi kikubwa. Lakini kwa kutambua umuhimu wa meza na viti kwa walimu wetu niwapongeze NMB na niwaombe msituchoke pale tutakapoendelea kuwaletea maombi,” amesema Ludigija.
Naye Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Mtambani, Elizabeth Paul, amesema shule hiyo yenye wanafunzi 1,085 ina walimu 28 na imekuwa ikifanya vizuri kitaaluma licha ya changamoto mbalimbali walizonazo.
“Tumeendelea kushirikiana kwa kuzingatia mafiga matatu yaani mzazi, mwalimu na mwanafunzi ili kuhakikisha lengo la elimu linafikiwa na hii imeleta mafanikio makubwa kwani kwa miaka mitatu mfululizo wastani wa shule umepanda ambapo mwaka 2018 ulikuwa 135.1, 2019 (135.5) na 2020 (139.5),” amesema Mwalimu Elizabeth.