Na Mwandishi Wetu, Zanzibar
BENKI ya NMB katika kuhakikisha shamra shamra za Siku ya Kizimkazi zinafana, wametoa msaada wa vifaa vya hospitali na shule vyenye thamani ya jumla ya Sh Milioni 54 ili kuwapa tabasamu wakazi wa Kizimkazi katika kipindi hiki.
Akizungumza wakati wa kukabidhi sehemu ya vifaa hivyo ikiwemo mabati kwa ajili ya kuezeka vyumba vya madarasa, vitanda kwa ajili ya kinamama kujifungulia na vitanda vya wagonjwa wodini Afisa Mkuu wa Wateja binafsi na Biashara NMB, Filbert Mponzi alisema utoaji wa msaada huo umetokana na kawaida ya NMB kutenga sehemu ya faida kuirudisha kwa jamii.
Mponzi alibainisha kuwa mbali na misaada hiyo NMB wamekua wakitoa elimu ya kutunza fedha kwa wanafunzi wa shule mbali mbali, ambayo inawafahamisha namna ya kutumia na kutunza fedha kwa maisha ya baadaye.
“Itakumbukwa hii si mara ya kwanza kwa NMB kuwa sehemu ya sherehe za Siku ya Kizimkazi, lengo letu ni kuunga mkono maadhimisho haya kwa njia ya kuigusa jamii hasa katika upande wa afya na elimu,” alisema Mponzi na kuongeza:
“Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imekuwa mdau wa karibu na benki yetu, tumeona ipo haja ya kuwasaidia wananchi wa Zanzibar kwa kutoa sehemu ya faida tunayoipata kwa mwaka, mtakumbuka tulianza na wakulima wa Mwani pamoja na wavuvi kwa kuzingatia sera ya Rais wa Zanzibar, Dk. Hussein Ali Mwinyi kuhusu uchumi wa buluu na sasa tunaendelea elimu na afya,”.
Aidha katika sehemu ya msaada huo NMB imetoa jumla ya vitanda 42 ambapo kati ya hivyo vipo vya kujifungulia, vya kufanyia uchunguzi na vya kulalia wagonjwa wodini; vilivyoenda katika Vituo vya Afya saba ikiwemo Bumbwini, Walezo Jeshini, Kizimbani, Chuini, Mwera, Chwaka na Unguja Ukuu.
Vilevile mabati kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa vyumba vya madarasa yamepelekwa katika jumla ya shule tano ikiwemo shule tatu za Mkoa wa Kusini ikiwemo Kizimkazi, Makunduchi na Binguni, huku Mkoa wa Mjini Magharibi yamepelekwa katika shule mbili ikiwemo Shule ya Mbuzini na Mtoni Kigomeni.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Kusini Unguja, Rashid Hadid Rashid, ameipongeza benki ya NMB kwa misaada mbali mbali wanayoendelea kutoa kwa jamii ya wananchi wa Zanzibar.
“Wakati wote NMB wamekuwa na sisi, tunapowalalamikia kuhusu changmoto za wananchi kukosa huduma muhimu za kijamii, ikiwemo sekta ya elimu kukosekana kwa madarasa mazuri ya kusomea baadhi ya madarasa kuvujisha, hivyo hii misaada iliyoletwa itasaidia kwa kiasi kikubwa kuondosha changamoto hizo,” aliema Rashid na kusisitiza:
“Kinamama walikua wakipata tabu kipindi cha kujifungua, vitanda ambavyo wanatumia vimechoka, lakini wenzetu hawa NMB wametusaidia vitanda hivi kwa mkoa wetu, hivyo ni vyema kuvitunza,”.
Mkuu wa Wilaya ya Magharibi ‘A’ Mkoa wa Mjini Magharibi, Suzan Peter Kunambi akiwa katika Shule ya Mbuzini alisema walichokifanya Benki ya NMB ni kusaidia maendeleo ya nchi kwa kuwa ukisaidia sekta ya efya na elimu umesaidia maendeleo.
Alibainisha kuwa shule nyingi hazina madarasa ya kutosha hali inayofanya wanafunzi kusoma kwa taabu na wengine wanakaa chini huku walimu wakichelewa kurudi nyumbani.
“NMB mmetufanyia mambo makubwa, tulichelewa kuleta maombi lakini mmetujibu kwa wakati. Wilaya yetu ina vituo vua afya 14, vilikuwa katika hali mbaya sana, naamini msaada huu utatusaidia sana,” alisema Kunambi.
Aidha, akizungumza katika hafla ya makabidhiano ya mabati na vitanda vya hospitali katika Shule ya Mbuzini, (Cluster Manager), Abdallah Duchi alisema malengo ya benki hiyo ni kuhakikisha inaendana na kasi ya Rais wa Zanzibar, Dk. Hussein Mwinyi.
“Kwa kuwa NMB ni mdau wa serikali tunafanya kila juhudi katika asilimia moja ya faida tunayopata kila mwaka kuirudisha kwa jamii kwa kutatua changamoto mbalimbali za kijamii hasa elimu na afya,” alisema Duchi.
Alibainisha kuwa kwa upande wa Zanzibar Benki ya NMB imefanya kazi kubwa katika kukuza uelewa wa wanafunzi kwenye masuala ya kifedha kwa kutoa elimu ya kifedha kwa wanafunzi zaidi ya 40,000.