Na Mwandishi Wetu, Mwanza
Katika kuhakikisha sekta ya wachimbaji wadogo wanapata mitaji na kukuza biashara zao benki ya NMB imelenga kutoa mikopo itakayofikia Sh bilioni 133 hadi mwishoni mwa mwaka huu kwa kundi hilo.
Hadi sasa benki hiyo tayari imekwishatoa mikopo ya Sh bilioni 63 kwenye sekta ya wachimbaji wa madini kuanzia mwaka 2019 huku ikiwa na uwezo wa kukopesha Sh bilioni 250 hadi 260 kwa mchimbaji mmoja.
Hayo yamebainishwa leo Ijumaa Julai 23, 2021 jijini hapa na Mkuu wa Idara ya Biashara wa NMB, Alex Mgeni, wakati akizungumza kwenye uzinduzi wa klabu ya madini ya kanda ya ziwa uliyolenga kuwakutanisha wadau wa madini zaidi ya 150 na benki hiyo ili kujadili namna bora ya kuboresha shughuli za wachimbaji kwa kuwapa mitaji yenye masharti na riba nafuu.
Mgeni amefafanua kwamba wanatoa pia mkopo wa vifaa vya kufanyia kazi kama gari la kubeba vifusi ambapo mkopaji analipa asilimia 30 na benki inalipa asilimia 70 .
“Kwa kuwa lengo letu ni kuwainua wachimbaji ili weweze kukuza biashara zao tumegundua wanakabiliwa na changamoto ya dhamana, tumeanza kufanya mchakato ili wawe wanatumia leseni zao kama dhamana na mkopo wetu ni wa riba nafuu sana kila mkopaji anaporejesha kiwango cha riba kinapungua kulingana na fedha iliyobaki,”amesema.
Upande wake Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mandisi Robart Gabriel, aliwataka wachimbaji wa mikoa ya kanda ya ziwa kuchangamkia fursa hiyo kwa kuweka taarifa sahihi za utendaji kazi katika maeneo yao ili wakidhi vigezo vya kukopesheka.
“NMB msiwe na hofu kopesheni wachimbaji wanaokidhi vigezo vya kukopesheka, madini yapo ya kutosha katika mikoa ya kanda ya Ziwa, nimepata bahati ya kuhudumu katika mikoa mitatu ya kanda hi , Geita, Mara na Mwanza naelewa kabisa uwepo wa rasilimali hiyo, changamoto kubwa inayowakanili wachimbaji wetu ni mitaji.
“Kwa kuwa madini yapo kinachotakiwa ni wavunaji wa kuyatoa ardhini na wenyewe wapo wanahitaji nyenzo ili waweze kuyatoa ardhini, soko lipo la uhakika linafahamika pia tunao wataalamu wa jiolojia ambao watawahakikishia uwepo wa madini katika eneo la mchimbaji anayetaka mkopo bila kupiga ramli hivyo naamini kwa kuwapa mikopo kundi hili mtasaidia sana ukuaji wa uchumi,” amesema Mhandisi Gabriel.
Amesema sekta ya madini inachangia pato la taifa kwa asilimia 5.2 lengo la Serikali ni kuboresha mazingira ya kundi hilo ili ifikapo mwaka 2025 liweze kuchangia asilimia 10.
Kwa upande wake Rais wa Shirikisho la Vyama vya Wachimbaji Wadogo wa Madini Tanzania (Femata), John Bina, amesema wanaweza kukopesheka maana wamekuwa wakiendesha biashara zao kwa mikopo ya watu binafsi ambayo ina riba kubwa.
“NMB ijenge imani kwa wachimbaji wadogo tutakopa na tutarejesha vizuri, bila mkopo huwezi kufanikiwa kuchimba tumekuwa tukiendesha biashara zetu kwa kukopa kwa watu binafsi maarufu kama kota niwahakikishie kwa siku tunakopa si chini ya bilioni 10 na tunarejesha.
“Sekta yha madini itawapatia faida kubwa NMB kwa sababu ni security ya nchi kwa mfano saizi kuna janga la ugonjwa wa korona, bidhaa nyingi zitashuka bei lakini madini hayawezi kushuka bei, maeneo ya kuchimba yapo ya kutosha changamoto tuliyonayo ni mitaji na teknolojia ambavyo sasa mnaenda kututatulia asanteni sana.
“Nawasihi wachimbaji wadogo waamini kwamba hakuna utajiri bila mkopo hivyo kila mgodi unaomilikiwa na wachimbaji wadogo uhakikishe unachangamkia fursa hiyo ambayo tumeitafuta kwa muda mrefu, naamini wachimbaji wakipata mikopo kilio cha ukosefu wa mitaji kitaisha,”amesema Bina.
Mmoja wa wachimbaji wadogo, Sarah Lusambagula, , amesema mikopo hiyo itasaidia kuongeza pato la nchi kwa kuwa leseni za uchimbaji zitaongezeka maana watu wengi watavutiwa na uchimbaji kwa sababu watakuwa na uhakika wa kupata mitaji.
Pia mikopo itasaidia kuchimba madini yenye kiwango bora kwa sababu wataweza kununua vifaa vya uchimbaji na watajiongezea vipato wao na taifa kwa jumla.
“Kwanza riba za NMB zinalipika kwa jinsi nilivyowasikiliza kila unaporejesha mkopo kiwango cha riba nacho kinapungua, naamini mikopo hiyo itakuwa ni kichocheo cha watu kuingia katika uchimbaji tofauti na ilivyokuwa awali ambapo watu wengi waliogopa kupoteza maisha kwa sababu hakuna vifaa bora vya uchimbaji tutafanya kazi kwa ukamilifu na kujiamini pia tutarejesha bila shida,”amesema.