Oscar Assenga , Tanga
BENKI ya NMB, imewadhamini watoto 80 wenye vichwa vikubwa na mgongo wazi wapate matibabu yao, ikiwamo kufanyiwa operesheni wakiwa hospitalini.
Hayo yalisemwa hivi karibuni na meneja wa benki hiyo, tawi la Madaraka mkoani Tanga, Elizaberth Chawinga wakati wa maadhimisho ya watoto wenye kichwa kikubwa na mgongo wazi duniani iliyofanyika jijini hapa .
Alisema katika kuadhimisha mwezi wa huduma kwa wateja, benki hiyo iliamua kugharamia matibabu na upasuaji.
Alisema mchakato huo ulianza mwezi wa saba na watoto tayari walikwisha kufanyiwa operesheni na benki hiyo imegharamikia na wamewakilpia bima ya afya ya mwaka mzima kupata matibabu.
“Jukumu letu ni kurudisha faida kwenye jamii,tumeona namna ya kuwafariji watoto,tumekuwa tunazunguka nao kuhamasisha dhana potofu kuhusu moto kwenye kichwa kikubwa na mgongo wazi,”alisema.
Alisema wameona waanze na idadi hiyo, wakiamini itaongezeka.
Katibu Tawala Msaidizi wa Mkoa wa Tanga, Idara ya Uchumi na Uzalishaji, Benedict Njau aliipongeza benki hiyo kutokana na kufanya kazi nzuri ya kuunga mkono juhudi za serikali kwenye sekta ya afya.
Aliitaka taasisi inayohusika na watoto kuhakikisha wanawaunga mkono benki hiyo kwa kufungua akaunti kwa ajili ya michango.