29.2 C
Dar es Salaam
Sunday, January 5, 2025

Contact us: info@mtanzania.co.tz

NMB KINARA HUDUMA ZA FEDHA KATIKA MABADILIKO

Na Shermarx Ngahemera,

WAHENGA wanasema mcheza kwao hutunzwa yaani yule anayechapa kazi kwa ufanisi hupata akitakacho na kupongezwa na wadau wake.

NMB imekuwa kama kawaida siku hizi kupata tuzo za kila namna ikiwa ni kutambua juhudi inazofanya kama benki katika kutekeleza yale yaliyo mbeleni kwake kwa jitihada ya kushirikisha kila mtu katika mifumo ya fedha.

Kwa kifupi benki ya NMB ni benki ya baadaye inayoishi sasa kama inavyoonekana kwa wengi ikiwamo Euromoney, jarida linaloongoza duniani katika masuala ya masoko  ya fedha ambalo limeichagua NMB Plc kwa mwaka huu kuwa ndiyo benki bora Tanzania  ikiwa ni mara yake ya tano mfululizo na katika Afrika  ni Benki Bora katika mabadiliko katika bara hili.

Euromoney katika kauli yake imesema kuwa Tuzo ya Ubora Uliopitiliza kwa mwaka huu iliamuliwa na Mameneja  wa Benki zaidi ya 600 kutoka nchi mbalimbali na Uingereza ambao walikutana jijini London, Uingereza.

“NMB leo ni benki inayofanya kazi na si benki iliyopo tu. Maamuzi magumu hufanyika kuhusu mitaji, biashara na watu. Katika mchakato mzima NMB imeendelea kupata faida na kulipa  magawio kwa wanahisa wake yanayoongoza katika sekta hiyo,” inasema  kauli ya Euromoney.

Clive Horwood  ni Mhariri wa jarida hilo ambaye kwa niaba ya Jarida hilo, lilijinasifu juu ya ubora wa chaguo lao kwa kuainisha vigezo vyake  vya maamuzi.

“Benki zinazoshinda tuzo zetu kwa kiasi kikubwa  zimefanya  maamuzi makubwa kuhusu mikakati ya wao wenyewe. Hapo usoni benki itakuwa ni kuhusu unachofanya na kile ambacho hufanyi. Mwaka huu benki zilizofanikiwa ni zile ambazo zimeainisha  kile  cha msingi kinachofanya wafanikiwe, nguvu zake  ambazo zimesababisha biashara ijengwe juu yake,” alisema Horwood.

Ubunifu na kufikiwa

Akichangia kuelezea mafanikio hayo, Mkurugenzi Mtendaji wa NMB Plc, Ineke Bussemaker, anasema habari hiyo njema ya tuzo ni matokeo  ya bidhaa za kibenki za kiubunifu,  matumizi ya teknolojia  na uwekezaji katika biashara ya benki kidijitali  na ikichangiwa  na mtandao mpana  wa matawi na kufikika kwa wateja na ATM  nchi nzima na hivyo  kuweza kuhusisha  kifedha watu wa matabaka yote na wa vipato tofauti.

“Kutatua matatizo ya wale ambao hawajafikiwa na mabenki inataka uwekezaji, ubunifu na uwezo wa kuwaleta pamoja wadau wote muhimu katika malipo na huduma nyingine za kibenki.  Hivi sasa, sisi ni watu muhimu sana katika uhusishi watu katika masuala ya kifedha katika Tanzania na tutaendelea kuleta ufumbuzi wa kibenki kwa ajili ya watu wengi,” alisema Ineke.

Alisema anafurahi kuona na kutambua kuwa ushindi huo  wa tuzo kama Benki Bora  katika mabadiliko Afrika na ile ya Benki Bora Tanzania  ni ushaidi tosha kuwa juhudi za NMB Plc zinatambulika kwa marefu  na mapana si nchini tu bali hata nje ya mipaka yake na eneo zima la bara hili.

Benki hiyo iko mstari wa mbele katika utekelezaji wa azimio la Maya ambalo linadai kuwe na juhudi za makusudi kuwaingiza kwenye mfumo wa fedha wote wale ambao hawamo kwa kuwatengenezea bidhaa za kibenki zinazolingana na uwezo wao na kuweka mbele zaidi huduma kuliko faida kwa benki husika. Ni mtazamo wa kiutu zaidi ili waweza kufaidika na masuala ya mfumo rasmi wa fedha ikiwamo mikopo na ujasiriamali.

Upanuzi wa shughuli

Ineke aliwashukuru wadau wote wakiwamo wateja, wafanyakazi na wawekezaji kwa kuwezesha upatikanaji wa tuzo hiyo kubwa na kuendelea kutoa ahadi ya kutumikia wateja wote kwa bidii na bila ubaguzi.

Ukiacha uongozi na ukiada wake, NMB ndiyo benki kubwa kuliko zote  kwa maana ya rasilimali  ikiwamo mtandao wa matawi zaidi ya 200 na nyingine bado zinaendelea kufunguliwa na wateja milioni 2.5 na vitoa pesa (ATM) 700 nchi nzima  na mtandao wa mawakala  zaidi ya 2,000 wakiwezeshwa na makampuni mbalimbali ya simu za mkononi.

Kuonesha ukali wa mashindano hayo tukichukulia mwaka huu kama mfano takwimu zinaonesha kuwa ni kinyang’anyiro kikali kwani benki 1,500 ziliingiza machapisho yao katika mpango wa tuzo  na wenye vipengele lukuki zikiwamo  zile za dunia tuzo 20, tuzo za maeneo 50 na Benki Bora kwa nchi 100.

Tuzo hii ya Euromoney inakamilisha ubora wa mwaka huu kwani katika maonesho ya Sabasaba NMB Plc imeibuka mshindi katika kitengo cha huduma za kifedha kwenye Maonesho ya Kimataifa ya Biashara ya 41, maarufu kama Sabasaba mwaka huu.

Ushindi huo ulitangazwa katika hafla ya ufungaji wa maonesho ya Sabasaba kwa mwaka huu yaliyodumu kwa siku 12.

Mgeni rasmi Waziri wa Viwanda, Biashara na Masoko wa Zanzibar, Balozi Amina Salum Ali, alisema NMB imeibuka mshindi kwa sababu ya kutoa huduma nzuri na kuwa na bidhaa ambazo zinalenga kuinua wananchi wa rika zote.

Akizungumza wakati wa kupokea tuzo  hiyo Ofisa Uhusiano wa Jamii wa Benki ya NMB, Doris Kilale, alisema mwaka huu NMB ilikuja na huduma za kibenki ambazo zilikuwa zinapatikana katika kila kona ya uwanja huo wa maonesho.

Alisema pia walikuwa na huduma ya benki inayotembea ambayo kwa muda wote wananchi walikuwa wanapata huduma ya kuweka na kutoa fedha.

- Advertisement -

Related Articles

1 COMMENT

  1. Ni uwongo mtupu
    NMB inajifanya inapata “faida” kwa sababu serikali inalazimisha fedha kuwekwa huko. Mishahara na pensheni ya serikali inalipwa kupitia NMB tukitaka tusitake
    Halafu wateja wa NMB wanakatwa makato kibao kama kamisheni na gharama zisizo na mashiko. K.M. ukitaka salio lazima ulipe, kila mwezi unakatwa ledger fees etc etc. Hakuna benki hapa nchini inayokwepua kamisheni kama hii NMB

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
593,000SubscribersSubscribe

Latest Articles