NA MWALI IBRAHIM NA JULIET MORI (TUDARCO)
MWAMUZI Israel Nkongo anayetambulika na Shirikisho la Soka Duniani (FIFA), anatarajiwa kuamua mchezo wa Ngao ya Jamii kati ya Azam na Yanga, utakaochezwa Jumamosi hii, Uwanja wa Taifa Dar es Salaam.
Nkongo ana historia kubwa na mechi hiyo kwani aliwahi kuchezesha mechi ya ligi ya miamba hiyo Machi 2012, lakini mchezo huo ulioishuhudia Azam ikitoka kifua mbele kwa kushinda 3-1, ulimalizika kwa Nkongo kupata mkong’oto kutoka kwa wachezaji wa Yanga, baada ya kuwaonyesha kadi nyekundu wachezaji wa Yanga, Nadir Haroub ‘Cannavaro’ na Haruna Niyonzima, hali iliyoamsha vurugu kubwa kutoka kwa mashabiki na wachezaji hao.
Hali hiyo ilipelekea Kamati ya Ligi ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), kutoa adhabu kwa wachezaji watano wa Yanga na timu kupigwa faini ya Sh 500,000 kutokana na washabiki wake kufanya vurugu kwenye mechi hiyo Machi 10, 2012, pia klabu hiyo ilipigwa faini ya Sh 500,000 kwa mujibu wa Kanuni ya 25(d) baada ya kuoneshwa kadi kuanzia tano kwenye mechi hiyo.
Kutokana na vurugu hizo, Cannavaro alifungiwa mechi sita za Ligi Kuu na kupigwa faini ya Sh 500,000 baada ya kuoneshwa kadi nyekundu kwa kosa la kumshambulia mwamuzi, Israel Nkongo kwenye mechi hiyo, huku wachezaji wengine wa Yanga walioadhibiwa kutokana na mechi hiyo ni Nurdin Bakari alifungiwa mechi tatu na faini ya Sh 500,000, Omega Seme alifungiwa mechi tatu na faini ya Sh 500,000, Jerryson Tegete aliyefungiwa miezi sita na faini ya Sh 500,000, wakati Stephano Mwasika, alifungiwa mwaka mmoja na faini ya Sh milioni moja.
Lakini Kamati hiyo ilimpongeza aliyekuwa nahodha wa Yanga, Shadrack Nsajigwa na aliyekuwa mshambuliaji wa timu hiyo, Hamis Kiiza, kwa kuwa mstari wa mbele kuzuia wenzao kumshambulia mwamuzi, ilimpongeza pia aliyekuwa Kocha Mkuu, Kostadin Papic kwa kukemea vurugu zilizofanywa na wachezaji wake.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Ofisa habari wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Baraka Kizuguto, alisema mwamuzi huyo atasaidiwa na Samwel Mpenzu (Arusha), Josephat Bulali (Tanga), mwamuzi wa akiba ni Hashim Abdallah (Dar es Salaam) na kamisaa wa mchezo huo ni Deogratius Rwechungura kutoka mkoani Mara
Alitaja viingilio vya mchezo huo kuwa ni Sh 7,000 kwa viti vya rangi ya kijani, bluu na rangi ya chungwa, VIP B na C Sh 20,000 na VIP A Sh 30,000 ambapo tiketi zitaanza kuuzwa siku ya mchezo maeneo ya uwanja huo.
Wakati huo huo, Ofisa habari wa klabu ya Azam, Jaffar Iddi, amesema wapo katika maandalizi ya mwisho ya mchezo huo lakini watawakosa wachezaji wao Michael Balou ambaye ni majeruhi na Allan Wanga ambaye yuko kwao msibani.
“Tumejiandaa kikamilifu na tunaendelea kujiandaa lakini tutawakosa wachezaji hao wawili kutokana na matatizo tofauti, lakini wachezaji wengine wako fiti na tuna imani tutashinda,” alisema.