28.2 C
Dar es Salaam
Friday, November 15, 2024

Contact us: [email protected]

Njia uzazi wa mpango chanzo kushuka umri saratani ya matiti -Daktari

Aveline Kitomary- Dar es salaam

DAKTARI bingwa wa saratani kutoka Taasisi ya Saratani ya Ocean Road (ORCI), Heleni Makwani, amesema moja ya sababu za umri wa wanawake wanaougua saratani ya matiti kuendelea kushuka, ni matumizi ya njia za uzazi wa mpango katika umri mdogo.

Takwimu zilizotolewa na taasisi hiyo miaka 10 iliyopita zilieleza ongezeko la ugonjwa, lakini pia umri unaoathirika huku wagonjwa wakiongezeka kutoka 250/300 hadi 900 ikiwa ni mara tatu ya wagonjwa walioonwa katika kipindi cha miaka mitatu.

Licha ya hivyo, wastani wa umri wa waathirika kwa miaka 10 iliyopita ni miaka 64, lakini kwa sasa ni miaka 56, ikiwa ni miaka 7 chini ya umri wa kipindi cha nyuma.

Akizungumza na MTANZANIA wakati wa mahojiano maalumu Dar es Salaam jana, Dk. Makwani alisema sababu nyingine ya umri kushuka ni matumizi ya vyakula vya kusindikwa.

“Mabinti wengi sasa wanatumia vidonge na sindano kama njia ya kuzuia mimba, vidonge hivi na sindano vina vichocheo vya ‘estrogen’ ambayo huweza kusababisha uwezekano wa saratani ya matiti.

“Na ukizingatia hii ‘estrogen’ ni ‘artificial’ – si ya kutengenezwa na mwili, hivyo huongeza wingi wa kichocheo hiki ambao hauhitajiki mwilini na hivyo kwenda kuleta athari kwenye mwili kwa kutengeneza uvimbe ambao huchochewa haraka na ‘estrogen’.

“Wasichana wengi sasa hivi wanatumia dawa za dharura za kuzuia mimba baada ya kufanya mapenzi, hii ni hatari, kingine ni watoto wa kike kupenda zaidi kula vyakula vya kusindikwa, hii pia inaweza kusababisha upataji haraka wa saratani ya matiti,” alibainisha Dk. Makwani. 

Alisema wasichana wengi wenye umri mdogo wanaoathirika zaidi ni wale wanaoishi maeneo ya mjini.

“Wasichana wa umri mdogo wakipata saratani ya matiti wana hatari kubwa zaidi kuliko wanawake wanaofikia kikomo cha uzazi,” alisema Dk. Makwani.

Alieleza kuwa hata hivyo uelewa wa jamii unaendelea kuongezeka kwa kadiri siku zinavyoenda kutokana na utoaji elimu kuhusu saratani ya matiti na saratani kwa ujumla.

“Watu wengi wanaelewa dalili mbalimbali na idadi ya wanaojitokeza mapema inaongezeka, watu wameanza kujigundua baada ya kujua dalili za mwanzo hivyo kufanya watu kuanza kuwahi hospitalini,” alisema Dk. Makwani.

Alishauri wasichana kutumia njia ya kitanzi kuliko njia za dawa na sindano ili kuweza kuepuka madhara.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles