*Asisitiza kutetea maslahi ya wanachama
Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital
Mgombea wa nafasi ya Urais katika Chama cha Wanasheria Tanganyika(TLS), Dk. Edward Hoseah amesema umefika wakati kwa chama hicho kufanya kazi kidigitali na kuachana na mfumo unaotumika hivi sasa.
Dk. Hoseah ameyasema hayo leo Jumanne Mei 10, 2022 jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na Mtanzania Digital ambapo amesema kuwa lengo ni kuona chama hicho kinapiga hatua zaidi katika nyanja ya utendaji kazi.
Amesefafanua zaidi kuwa katika kulitekeleza hilo iwapo ataingia madarakani kwa mara nyingine tena watakuwa na namba maalumu ya kuwasiliana na wananchama wao.
“Mahakamani wenzetu walishaanza kutoa huduma mtandaoni, kwa upande wetu TLS umefika wakati wa kuwa na Huduma Kiganjani tutakuwa na namba maalum ukipiga utakutana na taarifa zote kuhusu TLS.
“Hili nijambo ambalo tunatakiwa kwenda nalo kama ambavyo wenzetu duniani wamekuwa wakifanya,” amesema Dk. Hoseah.
Aidha, katika hatua nyingine Dk. Hoseah amefafanua kuwa kipaumbele chake imekuwa ni kutetea maslahi ya wanachama na kwamba iwapo atachaguliwa tena katika uchaguzi wa Mei 27, mwaka huu ataendelea kulitekeleza hilo.
“Jukumu langu kubwa la kwanza kama Rais wa TLS, ambalo ndiyo kipaumbele changu cha muda wote ni kutetea maslahi ya wanachama wetu, ikitokea Mwanachama wetu amewekwa ndani, tutahakikisha tunamtoa na hili nitalitekeleza iwapo nitachaguliwa tena,” amesema Dk. Hoseah.
TLS kinatarajia kufanya uchaguzi Mkuu katika nafasi ya Rais, Makamu wa Rais na Mweka hazina.
Uchaguzi huo unatarajiwa kufanyika Mei 27, mwaka huu jijini Arusha, ambapo tayari kampeni za wagombea urais zimeanza tangu Aprili 15 na zinatarajiwa kuhitimishwa Mei 26, mwaka huu siku ambayo pia utafanyika uchaguzi katika nafasi nyingine ukiwamo ya viongozi wa kanda.
Uchaguzi huo ni kwa mujibu wa katiba ya chama hicho ambao hufanyika kila baada ya mwaka mmoja.