Na Clara Matimo, Mwanza
Ili kuhakikisha wafanyabiashara wa ndani wanapata fursa ya kupeleka bidhaa zao kwenye masoko ya nje ya nchi wamepewa mafunzo yatakayowasaidia kufahamu vikwazo visivyo vya kikodi waweze kuyafikia masoko hayo kwa urahisi.
Mafunzo hayo ya siku tatu yaliyoanza Mei 9 hadi 11, mwaka huu yanatolewa jijini hapa na Kituo cha Biashara za Kimataifa (ITC) kupitia Mradi wa Kuwajengea uwezo Wajasiriamali katika kuongeza thamani na kupata masoko ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki pamoja na Soko la Ulaya, (Markup).
Akizungumza na Mtanzania Digital, Mratibu wa mradi huo, Safari Fungo, amesema mafunzo hayo ni matokeo ya utafiti walioufanya wa kuangaliani namna gani taratibu ambazo sio za kikodi zinaleta changamoto kwenye biashara hapa nchini na kubaini mambo mbalimbali ikiwemo vikwazo na fursa kwa wafanyabiashara kuingiza bidhaa ndani ya nchi au kwenda nje ya nchi.
“Katika tafiti hiyo tulibaini mambo mengi sana moja ya mambo ambayo yalionekena ni changamoto ya vifungashio, uwezo wa wafanyabiashara kukidhi mahitaji ya soko hasa katika maeneo ya ubora na viwango.
“Utafiti huo tuliufanya miaka miwili iliyopita kwa kushirikiana na serikali kupiti Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara tuliuzindua Aprili 14, mwaka huu baada ya kuuzindua tuliona ni busara yale yaliyopatikana kwenye tafiti yaweze kushuka chini kwa watanzania, tunakwenda sehemu mbalimbali hapa nchini tumeanza na mikoa ya kanda ya ziwa,” alisema Fungo na kuongeza.
Malengo yetu ni mawili, kuwajengea uwezo wadau katika masuala ya biashara kutoka sekta za uma na binafsi kwenye masuala ya kibiashara waweze kupata mbinu ya kujua masoko, mahitaji ya masoko ni yapi(market access) ili wafanyabiashara watumie taarifa hizo kwa wafanyakazi wa serikali wawasaidie jumuiya ya wafanyabiashara waweze kufanya biashara vizuri na kuhakikisha yale majibu ya kwenye tafiti yanawafikia wadau mbalimbali,”alisema.
Baadhi ya washiriki wa mafunzo hayo akiwemo Leopord Lema na Bakari Kadabi, walisema wanakumbana na changamoto mbalimbali ikiwemo kupeleka bidhaa zao sokoni nje ya nchi bila kuwa na taarifa za kutosha hivyo wamepata fursa ya kujua kwa uhakika vitu vinavyohitajika pamoja na gharama zisizo za kikodi.
“Miongoni mwa changamoto tulizonazo ni kukosa taarifa, hatuna kabisa taarifa ya kujua misingi ya biashara inaendaje kidunia hivyo mafunzo haya yatatusaidia exporters na importers kurahisisha jinsi ya kufanya biashara baina ya nchi yetu na nyingine,”alisema Kadabi ambaye ni Mwenyekiti wa Chama cha Wavuvi Tanzania, (Tafu).
Mkufunzi wa mafunzo hayo Mwalimu Mwandamizi kutoka Chuo kikuu cha Dar es Salaam, Dk.Petro Magai, alisema mafunzo hayo yatatoa fursa kwa wafanyabiashara kuongeza uelewa kuhusu masoko.
Meneja wa Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo Vidogo(Sido), Mkoa wa Mwanza, Bakari Songwe, alisema:
“Sisi sido kama wadau muhimu katika utoaji wa mafunzo mbalimbali kwa wajasiriamali tutasambaza elimu hii kwa wajasiriamali wetu waweze kunufaika na kupata taarifa mbalimbali zinazohusu biashara ya kimataifa,”.