26.9 C
Dar es Salaam
Friday, January 3, 2025

Contact us: info@mtanzania.co.tz

Nitahakikisha wakulima hawadhihakiwi

Na ANDREW MSECHU

KUNA taarifa zisizokuwa nzuri. Nimekuwa nikifuatilia kwa karibu mwenendo wa wakulima, soko na bei ya korosho mkoani Mtwara, malalamiko ya wakulima ni ishara kwamba wanaisoma namba.

Malalamiko ya wakulima wa korosho si ya kwao peke yao, kwa kuwa wakulima wa pamba, kahawa na wengine wa mazao ya biashara wamekuwa na kilio hicho hicho kwa miaka yote, ambacho kimeendelea hata baada ya Serikali ya Awamu ya Tano kushika hatamu.

Ninakumbuka namna Serikali hii ilivyoahidi kuhakikisha wakulima wanasaidiwa, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akieleza mara kadhaa kuwa mazao ya biashara ni sehemu ya siasa, akirejea kaulimbiu ya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere wakati wa Azimio la Arusha, kuwa ‘Siasa ni Kilimo’.

Mara kadhaa, Majaliwa amekuwa akifanya ziara katika maeneo yanayoongoza kuzalisha mazao ya biashara na hata mazao ya chakula, akijaribu kuonesha kwamba Serikali yake inajali na kutambua ‘shida’ za wakulima, hivyo iko tayari kushirikiana nao katika kuziondoa.

Taarifa inayonishtua ni ya wiki hii, ambayo inaeleza kuwa mnada wa korosho wilayani Newala na Tandahimba katika Mkoa wa Mtwara umevunjika mbele ya Naibu Waziri wa Kilimo na Umwagiliaji, Omary Mgumba baada ya wakulima kukataa kuuza korosho ghafi katika mnada wa wazi wa kwanza uliofanyika Kijiji cha Makukwe, Wilaya ya Newala.

Taarifa hiyo iliyoachapishwa na gazeti hili inaeleza kuwa wakati wa mnada huo kulikuwa na kampuni 15 zilizotuma zabuni za kununua korosho ghafi kwa bei ya juu ya Sh 2,717 kwa kilo moja na bei ya chini ikiwa ni Sh 1,711.

Wakati wanunuzi hao wakitaka kununua kwa bei hiyo, msimu uliopita wa mwaka 2017/18 katika mnada wa kwanza, kilo moja ya korosho ilinunuliwa kwa Sh 3,850 na katika minada iliyofuata ilifikia hadi zaidi ya Sh 4000 kwa kilo kutoka bei elekezi ya Sh 1450.

Kwa msimu wa mwaka huu wa 2018/19, mazingira yanabadilika ambapo sasa wanunuzi wanatakiwa kufika wenyewe katika minada wakiwa na barua za zabuni tofauti na misimu iliyopita ambayo walikuwa wakipeleka barua katika vyama vikuu na kusubiri minada.

Baada ya wakulima kukataa kuuza korosho zao, Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Gellasius Byakanwa ananukuliwa akiwapongeza na kusema wamefanya uamuzi sahihi kwa kuwa wanunuzi wamekuwa wakiwaibia kwa kuwapangia bei ya kununua zao hilo.

“Wingi wa wanunuzi waliofika hapa haukuwa wa kawaida kwani wengine walifika kuangalia bei ya korosho hali ambayo ilionesha wana uhitaji wa bidhaa hiyo.

“Kwa hiyo, nawapongeza wakulima kwa kusimamia thamani ya korosho yetu kwani hata tathimini niliyoifanya wakati barua zikisomwa, inaonesha wanunuzi walikuwa wamepanga bei.

“Kwa kweli mmenifurahisha sana kwani mahitaji ya korosho ni makubwa.

“Pamoja na kwamba leo mnada haukufanyika, bado naamini watakuja tu, yaani hakuna namna, korosho zetu ni bora hatuwezi kulima sisi na kuzihudumia kwa gharama kubwa halafu wanunuzi watupangie bei ya kuuza, haiwezekani,” ananukuliwa.

Huyu anasahau kwamba bei elekezi iliyopangwa na wakala wa Serikali, kamba ni Bodi ya Korosha kupitia kikao chake cha Septemba mwaka huu kilichokaa Mtwara, yeye akiwa sehemu ya Serikali ilithibitisha bei ya msimu wa 2018/19 kuwa Sh 1550, hivyo bei ya Sh 2717 iliyofikiwa katika mnada huo ilikuwa juu ya bei elekezi.

Wakulima wanaona bei elekezi na hata iliyofikiwa kwenye mnada huo wa kwanza si saizi yao kwa hiyo Bodi ya Korosho imeshindwa kuheshimu na kujali mahitaji ya soko, ambapo wakulima wanaeleza kuwa hawawezi kuuza korosho zao kwa Sh 2,717 kwa kilo wakati wakibangua wanauza kwa Sh 17,000 kwa kilo na kwa msimu uliopita waliuza korosho ghafi hadi kwa zaidi ya Sh 4000 kwa kilo.

Naibu Waziri Mgumba anasema wakulima wanapaswa kuandaa korosho katika ubora unaofaa sokoni kwa kuwa ubora mdogo husababisha bidhaa kuwa na bei ndogo akiwataka wakulima kutunza ubora ili kuliongezea thamani zao hilo kwa kuwa litahitajika zaidi katika soko la dunia.

Mwenendo wa mnada huu unanikumbusha mjadala mkali uliotokea wakati wa mapendekezo ya bajeti ya mwaka 2018/2019 kuhusu zao la korosho, ambayo katika mapendekezo yake, yaliondoa ruzuku ya asilimia 65 iliyokuwa inaenda kwenye Mfuko wa Maendeleo wa Korosho na badala yake, ilipelekwa kwenye mfuko mkuu wa Serikali.

Nainakumbuka namna wabunge mikoa ya Kusini walivyosimama kidete kupinga mabadiliko hayo, ambamo mmoja wao, Nape Nnauye (Mtama) alisema hawayaungi mkono.

Ninakumbuka namna mjadala huo ulivyotumika kueleza hofu ya wakulima na wadau wa korosho kupitia kwa wawakilishi wao bungeni, wakieleza kuwa kilio cha wakulima hasa ni kuhusu uhakika wa pembejeo, ambazo mara ya kwanza walikuwa wakizipata kwa njia ya ruzuku lakini sasa kwa kuondolewa kwa ruzuku hiyo na kupelekwa katika ‘fuko kuu la Serikali’ kutaleta shida ya upatikanaji wa pembejeo.

Wakati mjadala huo ukiendelea, wadau wa korosho walisema wanaona kuwa Serikali ilitakiwa kutoa elimu na kuwaandaa kuwa wanatakiwa kununua mwenyewe na hofu kubwa ipo kwa wakulima wadogo.

Mwaka jana zao la korosho limeweza kuleta mapato makubwa katika taifa na sasa linatangazwa kuanzishwa katika maeneo mengine 17.

Matukio ya mwaka huu yanatokea wakati kampuni 66 zikiripotiwa kuchukua leseni ya kununua korosho ikiwa ni ongezeko la asilimia 22 kutoka kampuni 54 kwa msimu uliopita huku utaratibu wa minada ukiwa umepangwa kufanyika kila wiki kutegemea korosho zitakavyokusanywa kutoka kwa wakulima kwenda maghalani.

Kwa mwenendo huu, nina hakika nina nafasi ya kufanya tofauti katika kuhakikisha jasho la wakulima wa Tanzania wanaheshimika na kurejeshwa kwa thamani ile ile.

Iwapo nitakuwa katika nafasi yenye mamlaka ya juu katika kusimamia haki na wajibu, nitahakikisha wakulima wote wa korosho kule katika mikoa ya Kusini, wa kahawa katika mikoa ya Kaskazini Mashariki, Kaskazini Magharibi na Nyanda za Juu Kusini wanapata faraja kwa kuwawezesha kufikia malengo yao kupitia uimara wa bei za mazao yao.

Nitafanya tofauti kwa kuhakikisha kuwa wakulima wa pamba katika mikoa ya kanda ya ziwa wananufaika na pamba yao, nitahakikisha bei ya pamba yao, waliyoilima kwa jasho lao inawanufaisha na kuwawezesha kurejesha gharama zao kwa kuuza mazao yao kwa bei yenye tija.

Nitafanya tofauti kwa kuhakikisha heshima ya wakulima ambao ndiyo wavuja jasho wenye manufaa kwa taifa inarejea, kwa kuwasaidia kuzalisha kisasa na kuwa na matokeo mazuri katika kazi zao, hatua itakayowezesha taifa pia kunufaika na kustawi.

Nitafanya tofauti kwa kuhakikisha watendaji wanaopokea maagizo yangu wanatambua nafasi zao, kwa kusimamia bodi zinazohusika na mazao kuhakikisha zinatoa maamuzi kwa masilahi ya wakulima na sitatoa nafasi kwa watendaji wangu kuanza kuwa ‘bendera fuata upepo’ kama ilivyotokea kwa kiongozi huyu wa mkoani ambaye amejikuta akiwasifu wananchi kukataa bei ambayo iko juu ya bei elekezi ya Serikali, baada ya kuona msimamo wa wananchi dhidi ya bei hizo zisizokidhi mahitaji.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
593,000SubscribersSubscribe

Latest Articles