Na Nora Damian, Mtanzania Digital
Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) kina mpango wa kumuajiri mmoja wa wanafunzi wake wa kike aliyefanya vizuri katika Shahada ya Hisabati ili kuwavutia wengine kupenda masomo ya sayansi.
Fursa hiyo ya ajira imetangazwa na Mkuu wa chuo hicho Profesa Zacharia Mganilwa, wakati wa maadhimisho ya siku ya wanawake duniani ambapo chuo hicho kiliandaa kongamano maalumu la wanawake.
Amesema wanahawamasisha watoto wa kike kusoma masomo ya sayansi ikiwemo hisabati na tayari timu ya wataalamu wa chuo hicho imekwenda katika mikoa ya Lindi na Mtwara kuwahamasisha.
“Juzi nilikuwa nasaini vyeti nikakuta kuna mwanafunzi anaitwa Joyce amepata ‘First Class’ inapotokea mwanafunzi wa kike kupata daraja la kwanza Shahada ya Hesabu kwanza ni furaha kubwa…huyu hatuwezi kumuachia lazima tumpe mkataba.
“Tutakapompatia ajira badala ya kwenda wababa peke yao kuhamasisha watoto wa kike kusoma masomo ya sayansi tukimpeleka na huyu wanakuwa wanaona mfano mzuri,” amesema Profesa Mganilwa.
Amesema pia wanajivunia kuwa na walimu wengi wa kike ambapo wengine wanaongoza idara mbalimbali zikiwemo idara ya kompyuta na idara ya sayansi na hisabati.
Mkuu huyo wa chuo amewaasa wazazi na watoto wa kike kuyapa uzito masomo ya sayansi kama mengine kwani yana wigo mpana wa ajira.
“Tunahitaji wanasayansi wa kike wengi tusiishie tu kwenye siasa kwamba 50 kwa 50, inatakiwa iende kila nyanja,” amesema.
Profesa Mganilwa pia amewataka wazazi wawaandae kisaikolojia watoto wao pindi wanajiunga na elimu ya juu ili kuepuka viashiria vya hatari kama rushwa ya ngono.
“Anapotaka kujiunga na elimu ya juu ni vizuri wakawaanda kisaikolojia kwamba mazingira atakayoenda kupambana nayo ni pamoja na ya rushwa ya ngono, hivyo anakuja akiwa amejiandaa na sisi kama menejimenti za vyuo tunawapa mbinu mbalimbali ikiwa ni pamoja na kutoa taarifa endapo atakwazwa kwenye maeneo hayo.
“Tunawasisitiza wanataaluma watambue mbali ya kuwafundisha wanafunzi wana jukumu pia la uzazi na ulezi hivyo wawape msaada wa kitaaluma,” amesema.
Naye Naibu Mkuu wa chuo hicho (Fedha, Mipango na Utawala), Dk. Zainab Mshana, amesema hakuna kitu ambacho mwanamke hawezi kufanya na kwamba muhimu kuwe na mipaka.
“Tamaduni tulizonazo si kikwazo zinatufanya kuheshimiana hazijachukua mikono yetu au akili zetu, tujitahidi kutumia nguvu tuliyonayo kujituma na kufanya kile tunachoweza hakuna kazi ambayo imewekwa kwa mwanamke au mwanamume peke yake,” amesema Dk. Zainab.
Katika kongamano hilo mada mbalimbali zilijadiliwa kama vile mchango wa mwanamke katika kuelimisha na kuzuia rushwa, afya ya akili kwa mwanamke, Virusi vya Ukimwi na magonjwa yasiyo ya kuambukiza.