WIKI iliyopita Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), lilimtangaza rasmi kocha Amy Ninje, kuwa mkurugenzi wa ufundi wa taasisi hiyo yenye dhamana ya kusimamia mchezo huo nchini.
Ninje ambaye ana leseni ya Chama cha Soka Engand (UEFA), amekabidhiwa jukumu hilo ambalo awali lilikuwa linashikiliwa na Salum Madadi.
MTANZANIA tunampongeza Ninje kwa kuteuliwa kushika wadhifa huo wa ukurugenzi wa ufundi ambao ndio msingi hasa wa mipango yote ya maendeleo ya soka katika nchi yoyote.
Tunaamini kwamba, elimu yake, uzoefu wake katika soka kuanzia akiwa mchezaji mpaka kocha utamsaidia kutimiza majukumu yake kwa ufasaha ili hatimaye soka la Tanzania liweze kupiga hatua kubwa, baada ya kushindwa kufanya hivyo kwa miaka mingi.
Jambo la msingi ambalo tunamkumbusha Ninje ni kwamba, soka la Tanzania linachangamoto nyingi ambazo kwa miaka mingi zimeonekana kushindwa kupata tiba sahihi, hivyo ukiwa mkurugenzi mpya wa ufundi, Watanzania wanapenda kuona mabadiliko.
Miongoni mwa changamoto hizo ni kukosekana kwa mfumo mzuri wa uendelezaji wa soka la vijana.
Ukweli ni kwamba, ili kupiga hatua ya maendeleo katika mchezo wa soka ni lazima uwepo mfumo sahihi na unaofanya kazi ya kuendeleza soka la vijana.
Kwa Tanzania hili limekuwa tatizo kubwa, matamko na hotuba nyingi zimekuwa zikitolewa kuhusiana na umuhimu wa soka la vijana lakini utekelezaji wa mpango huo umekuwa ukiishia midomoni.
Mfano mzuri ni katika Ligi Kuu Tanzania Bara ambayo moja ya vigezo vya kushiriki ni klabu kuwa na timu ya vijana.
Hata hivyo, klabu nyingi zimekuwa zikifanya udanganyifu kwamba zinamiliki timu za vijana, lakini ukweli ni kwamba hazina vikosi hivyo.
Na hata zile zilizonazo zimekuwa zikilazimika kuwatumia wachezaji pale tu zinapotakiwa kufanya hivyo, lakini hazina bajeti ya kuzihudumia wakati wote.
Utaratibu wa TFF unazitaka timu za vijana za klabu za Ligi Kuu kucheza mechi ya utangulizi kabla ya vikosi vikuu kupambana.
Hata hivyo, klabu inayoshindwa kupeleka uwanjani kikosi chake cha vijana hutozwa faini.
Kimsingi hili la faini haliwezi kuwa tiba na suluhisho la tatizo lililoko katika soka letu, badala yake kinachotakiwa kufanywa ni kutilia mkazo klabu kumiliki timu kali za vijana.
Hili ndilo ambalo Ninje anapaswa kulifanyia kazi kama njia sahihi zaidi itakayosaidia kulitoa soka la Tanzania hapa lilipo na kulipeleka mahali pengine.
Zaidi ya hapo, Ninje anapaswa kuwa muwazi ikiwa ataona kuna mahala anakwama au kuna mtu anamkwamisha badala ya kuwa kimya na kusubiri hadi mambo yamharibikie na lawama ziende kwake.
TFF kwa upande mwingine ambao ndio bosi wa Ninje, inapaswa kutenga bajeti ya kutosha ambayo itamwezesha mkurugenzi wa ufundi kutekeleza majukumu yake bila vikwazo.