27.6 C
Dar es Salaam
Friday, January 3, 2025

Contact us: info@mtanzania.co.tz

NIMR yatakiwa kusaidia wataalamu tiba asili

Na Ramadhan Hassan, Dodoma

WAZIRI wa Afya,Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto, Dk. Doroth Gwajima ameitaka Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu hapa nchini (NIMR) kuweka mpango kazi wa kuwasaidia wataalamu wa tiba asili na mbadala kuziendeleza dawa zao.

Akizungumza jana Jijini Dodoma wakati akifunga maadhimisho ya kitaifa ya wiki ya siku ya tiba asili ya Mwafrika,Waziri Gwajima amesema lazima NIMR iweke mpango kazi ambao utawasaidia wataalamu wa tiba asili na tiba mbadala dawa zao ziweze kufika mbali na watu wengi wazijue.

“Tuweke azimio wale wote waliosajiliwa tuwawekee mpango kazi, lazima Watanzania wafaidike na hizi dawa naagiza NIMR hili lifanyieni tuone mnakwama wapi lazima dawa za asili zifike mbali ikiwezekana hata nje ya nchi unakuta mtu ana miaka 16 anahangaika na kibali tu sio sawa,”amesema.

Aidha,Waziri huyo  wa afya amewataka wataalamu wa tiba asili na tiba mbadala kupanda miti dawa ambayo itasaidia upatikanaji wa dawa kiurahisi.

“Sio kukata miti tu pandeni na nyie miti  dawa ili iwe rahisi kupatikana kwa dawa, pia itasaidia kutunza mazingira na itakuwa rahisi kutoa elimu ya miti dawa,”amesema.

Pia, amezitaka Halmashauri nchini kuweka mpango wa kupanda mashamba ya  miti ya dawa ambayo itasaidia upatikanaji wa dawa.

Aidha,amewataka wataalamu hao kufuata kanuni taratibu na sheria katika ufanyaji kazi wao kwani kuna baadhi wamekuwa wakifanya matendo ya aibu ambayo hayawapendezi watanzania.

“Nyinyi wataalamu kuna matendo mnayofanya ambayo sio mazuri natoa namba zangu hapa ukimwona mtaalamu anafanya ndivyo sivyo nipigie maana kuna mambo ya aibu yanaendelea huko kwenu,”amesema.

Awali akisoma risala,ya waganga wa tiba asili na tiba mbadala,Mjumbe wa Baraza la Waganga wa tiba asili na tiba mbadala, Elizabeth Lema amesema wanashauri dawa za tiba asili ambazo zimesajiliwa ziweze kuuzwa katika maduka ya dawa ya kawaida ili watanzania  wapate huduma hiyo.

Amesema wanaahidi  kutoa ushirikiano kwa Serikali ikiwamo kuwaweka wazi waganga matapeli lengo likiwa ni kutoa huduma ya kueleweka na kuaminika kwa watanzania.

Naye,Mkurugenzi wa Idara ya Tiba, Dk.Vivian Onandi amesema wameanza kuadhimisha siku hiyo mwaka 2003 katika viwanja vya Mwembeyanga Jijini Dar es salaam ambapo amedai mafanikio waliyoyapata ni pamoja na Watanzania wamekuwa na uelewa wa kusajili dawa,kukubalika kwa tiba asili pamoja na viwanda vya tiba asili kuongezeka.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
593,000SubscribersSubscribe

Latest Articles